Alhamisi, 18 Septemba 2025

‘UPATANISHI CHACHU YA KUONGEZA IMANI YA WANANCHI KWA MAHAKAMA’

Na ARAPHA RUSHEKE,Mahakama Kuu Dodoma.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) hivi karibuni kiliandaa mafunzo kwa Majaji, Mahakimu na washiriki wengine lengo likiwa kuwajengea uelewa mpana katika kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa njia ya usuluhishi wa migogoro.

Mafunzo hayo ambayo yalifanyika jijini hapa yalifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na kusisitiza kuwa ufanisi wa upatanishi ni chachu ya kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama.

Jaji Masabo aliwashukuru washiriki wote waliokuja kutoka maeneo mbalimbali nchini, akisisitiza kuwa mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa njia ya usuluhishi wa migogoro.

Aidha, alitoa shukrani kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, kwa uongozi wake thabiti katika kuhakikisha upatikanaji wa haki unaimarishwa kupitia programu za kuongeza uwezo wa watumishi wa Mahakama.

Vilevile alikishukuru Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  kinachoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo kwa kuratibu mafunzo hayo na mengine mengi.

Mafunzo hayo yalifadhiliwa na GIZ Tanzania, ambao pia wameunga mkono uandaaji wa mwongozo wa mafunzo na shughuli nyingine za kuimarisha mfumo wa utoaji haki.

Mafunzo ya upatanishi ni mwendelezo wa mafunzo ya msingi yaliyofanyika mwezi Julai na Agosti, ambapo maafisa 26 walipata ujuzi kutoka kwa Majaji Bingwa wa Upatanishi kutoka Ujerumani na yanakusudia kuwajengea washiriki uwezo wa kuwa wakufunzi kwa wengine katika maeneo yao.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo walikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Zainab Mango na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akiongea jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usuluhishi yaliyofanyika jijini Dodoma.


Meneja wa utekelezaji wa utawala wa sheria (GIZ), Bw. Mohamet Brahim akitoa salam wakati ufunguzi wa mafunzo hayo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzani,a Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki kutoka Shinyanga wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzani,a Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki waliohudhuria ufunguzi wa mafunzo hayo.

 

Meneja wa utekelezaji wa utawala wa sheria (GIZ), Bw. Mohamet Brahim akifurahia jambo wakati ufunguzi wa mafunzo hayo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni