Alhamisi, 18 Septemba 2025

JAJI MWARIJA ATOA RAI KWA MACHIFU KUWA MABALOZI WA UTOAJI ELIMU YA MAHAKAMA

·  Jaji Kiongozi naye asema Machifu wana mchango mkubwa katika usuluhishi wa migogoro

   Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija ametoa rai kwa Machifu nchini kuendelea kuwa mabalozi wa utoaji elimu ya Mahakama kwa jamii.

Mhe. Mwarija alieleza hayo tarehe 16 Septemba, 2025 wakati Machifu kutoka Mikoa ya Kusini walipomtembelea Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Jaji Mwarija alisema kuwa, suala la utoaji elimu ya Mahakama ni muhimu kuzingatiwa ambapo alisema, “kuna desturi moja ya watu wetu, mtu anayeshinda kesi ananyamaza kimya, anayeshindwa anapiga kelele kwahiyo ukiona Mahakama inalaumiwa mara nyingi ni wale ambao wameshindwa kesi kwa mujibu wa sheria kabisa lakini wale walioshinda hawatokezi wakisema kuna haki mahakamani, kwa hiyo sasa nyie kwa vile mpo karibu zaidi na jamii ni muhimu mlisemee hilo na kuelimisha jamii ili kujua kuwa Mahakama inafanya kazi kwa mujibu wa sheria.”

Mhe. Mwarija alisema, sasa hivi, Mahakama ina Mahakimu hadi wa Mahakama za Mwanzo ambao wana Shahada za Sheria kwahiyo wapo karibu zaidi na kule ambako Machifu wapo hivyo inapotokea kwamba wanahitaji kujifunza kuhusu jambo fulani hasa kuhusu masuala ya haki inawezekana kwa wakati wowote.

Aliongeza kwa kuwaomba Machifu hao kuendelea kuwa macho ya Mahakama na kushiriki kutoa baadhi ya mitazamo hasi ya jamii kwa Mhimili huo. 

Akizungumzia kuhusu Kongamano la Machifu wa Mikoa ya Kusini, Mhe. Mwarija amewapongeza Machifu hao na kusema kwamba wamefanya vizuri na kurudisha mshikamano baina yao na kwamba Mahakama pia ipo tayari kushirikiana nao.

Kadhalika, Mhe. Mwarija aliwasihi Machifu hao kuendelea kusimamia maadili ya vijana kwa kuwa yanaporomoka kwa kiasi kikubwa.

“Maadili ya vijana kwakweli yanaporomoka sana labda sio vijana tu lakini hata watu wazima kwa hiyo sasa kazi ya Machifu inazidi kuwa ni ya muhimu sana na naunga mkono kama mlivyosema mtambulike kisheria, nadhani Jaji Mkuu yupo kwenye nafasi nzuri ya kusaidia kuhimiza hili ili mamlaka husika ziweze kusaidia katika hili,” alisema Jaji Mwarija.

Aidha, Mhe. Mwarija aliwapongeza Machifu hao kwa kuwa na maono mpaka ya kuanzisha Asasi ambapo alisema kwamba ni hatua nzuri kwani Machifu wa sasa wanakwenda kulingana na mazingira ya sasa tofauti na wale wa zamani.

“Niseme tu kwamba ugeni huu ambao umetutembelea ni wa baraka sana na muhimu pia kwetu Mahakama kwa sababu ya majukumu ya Machifu wanakuwa sehemu ya wadau wetu wa haki kwa sababu wanasimamia maadili ya jamii, utamaduni na hata kulinda mazingira,” alisema Jaji Mwarija.

Akitoa neno wakati wa mazungumzo kati ya Machifu hao na Jaji Mkuu, kwa upande wake Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani alisema kuwa mchango wa Machifu katika kuhakikisha kwamba jamii zinakaa kwa amani na usalama ni mkubwa na haupaswi kuupuzwa.

“Sisi kama Mahakama tumeanza kushirikiana nao japo si kwa ukubwa sana lakini tumeanza kuwatambua, Kituo chetu kile cha Usuluhishi Mahakama Kuu Dar es Salaam kwa miaka kama miwili sasa mfululizo kimekuwa kikiwatambua Viongozi wa jadi na Machifu wanaofanya vizuri kwenye usuluhishi,” alisema Jaji Kiongozi.

Aliongeza kwa kutoa mfano wa mwaka jana Mahakama ilipata Machifu wawili ambapo mmoja ni Chifu wa Morogoro (Kingalu) ambaye anafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye usuluhishi na mwingine ni wa Lindi ambaye kwa kiasi kikubwa alifanya usuluhishi kusababisha Mahakama ya Mwanzo kukosa kesi.

“Kwakweli usuluhishi ambao ndio hasa Viongozi wetu wa asili na Machifu wamekuwa wakiufanya una nafasi kubwa sana ya kuleta utulivu tofauti kabisa na sisi tunavyosikiliza mashauri, sisi tunaposikiliza mashauri mmoja tu atashinda na mwingine atashindwa hakuna nafasi ya kutoka sawa ‘draw’ na hiyo inatengeneza uadui, aliyeshindwa atatengeneza uadui kwa Hakimu lakini pia kwa yule aliyeshinda,” alisema Mhe. Dkt. Siyani.

Kadhalika, Jaji Kiongozi alisema kwamba, Machifu wanafanya kazi kubwa ambayo inatakiwa kutambulika zaidi kwa kuwa historia ya nchi pia inaonesha mchango wao hivyo ni muhimu kuangalia namna ya kuwatumia vizuri zaidi bila kuleta mgongano wa majukumu.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Siyani alitoa rai kwa Machifu hao kuendelea kutoa elimu na kuangalia namna ambavyo wanaweza kufanya kazi zao katika mazingira ya sasa bila kuleta mgongano ya kuonesha kwamba pengine wanaingilia majukumu ya Mahakama au kuingilia majukumu ya Mabaraza ya Kata.

Machifu hao kutoka Mikoa ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara, Iringa, Morogoro, Njombe, Rukwa, Songwe na Mbeya waliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Akida Wabu (AWADEF), Prince Ibrahim Samata ambaye pamoja na mambo mengine alimueleza Jaji Mkuu kwamba lengo la kuanzisha Shirika hilo kuwa ni kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa Tanzania, uhifadhi na utunzaji wa mazingira, utawala bora, kukuza maendeleo endelevu na kuwezesha kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya Watanzania.

“Tumepanga kufanya Semina ya kuwajengea uwezo Machifu wa Mikoa hiyo ya kusini ambayo itakusanya Machifu takribani 200 kutoka kwenye mikoa hiyo tisa ili pamoja na mambo mengine kuwajengea uwezo katika masuala ya uongozi, masuala ya maadili, masuala ya malezi na makuzi na kuwaongezea uelewa juu ya mifumo ya Taasisi mbalimbali zinavyofanya kazi ikiwemo Mahakama kama Chombo cha haki ambacho kimeendelea kuaminiwa na Watanzania tangu enzi hizo na enzi hizi,” alisema Prince Samata.

Ugeni wa Machifu hao umekuwa na faida kwa Mahakama kufuatia Mahakama kupatiwa ardhi ya hekari 56 wilayani Ikungi ambayo imetolewa na Chifu Adamu Gwau wa Wilaya hiyo na Machifu wengine wa Mikoa ya Kusini nao wameahidi kutoa ardhi kwa Mahakama kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ili kuwafikia wananchi hadi katika ngazi za Kata.

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija akizungumza na sehemu ya Machifu kutoka Mikoa ya Kusini (hawapo katika picha) wakati Machifu hao walipomtembelea Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania tarehe 16 Septemba, 2025 ofisini kwako Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akizungumza na sehemu ya Machifu kutoka Mikoa ya Kusini (hawapo katika picha) wakati Machifu hao walipomtembelea Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania tarehe 16 Septemba, 2025 ofisini kwako Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mazungumzo kati ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Machifu kutoka Mikoa ya Kusini yakiendelea wakati Machifu hao walipomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma tarehe 16 Septemba, 2025.
Mazungumzo yakiendelea.

 
Picha ya pamoja na Machifu. Katikati ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija, wa pili kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, wa kwanza kushoto ni Chifu Mkuu wa Wayao Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Maendeleo ya Akida Wabu (AWADEF), Chifu Saad Wabu Mussa Mitondo II na wa kwanza kulia ni Chifu wa Wilaya ya Ikungi-Singida, Bw. Adam Gwau.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni