· Jaji Mkuu asema ipo haja ya kufanya marekebisho ya Kanuni za uchaguzi
· Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman ashiriki kutoa uzoefu kuhusu mashauri ya uchaguzi
· Jumla ya washiriki 381 wanufaika na mafunzo hayo
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dodoma
Mafunzo ya Namna Bora ya
Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yaliyokuwa yakitolewa kwa Majaji, Naibu
Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya nchini
yamehitimishwa leo, huku Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju
akishauri kwamba Kanuni za Uchaguzi zifanyiwe marekebisho ili kuwawezesha
Majaji na Mahakimu kusikiliza ipasavyo mashauri hayo.
Akizungumza leo tarehe 18
Septemba, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo hayo yaliyohusisha washiriki wa kundi la
mwisho la Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Masaju amesema majadiliano mbalimbali
pamoja na changamoto zilizowasilishwa na washiriki wa Mafunzo yameonesha kuwa,
kanuni hizo zina mapungufu na hivyo kuwa na haja ya kuzifanyia mabadiliko.
“Niwashukuru kwa kukubali
kufanya mabadiliko ya kanuni hizi zinazotungwa na Jaji Mkuu, tumepata ushauri
mzuri hapa na Jaji Mkuu Mstaafu ametushauri maeneo ya kuangalia , tuna pa
kuanzia na wawezeshaji wetu ni mahiri na ninyi wenyewe ni mahiri mna ustadi
mkubwa kwenye maeneo haya na hili tutalifanya kabla ya tarehe ya uchaguzi
wenyewe na litakuwa zoezi shirikishi lakini maboresho ya mwisho yatakayotolewa lazima
yapate kibali cha Mahakama maana sisi ndio wenye ile sheria na mwenye mamlaka
ya kuitunga ile sheria ni Jaji Mkuu,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa,
lengo la kufanyia marekebisho kanuni hizo ni kwa sababu ni sheria za uchaguzi
zimekusudia kufikia lengo la wananchi la kupata Serikali ambayo itawajibika
kwao kwa ajili ya ustawi wao wananchi kama inavyotajwa kwenye Ibara ya 8 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine
inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na inayofuata
haki ya kijamii na kwamba mamlaka ya Serikali hiyo yatapatikana kutoka kwa
wananchi.
‘.... Na kwamba wananchi
ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote
kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii na lengo kuu la Serikali ikiwa ni
ustawi wa wananchi na Serikali ikiwajibika kwa wananchi,’ amenukuu Mhe. Masaju
akirejea Ibara ya 8 ya Katiba.
Ameongeza kuwa, lengo
lingine la kufanya maboresho kwenye kanuni hizo ni kuleta uwazi zaidi katika
kupata tafsiri sahihi ya migogoro ya uchaguzi inayoletwa mahakamani na kujua kama
uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Amesema kuwa, katika
mazingira kama hayo, Mahakama ambayo ina jukumu la kutunga kanuni za kusimamia
mashauri ya uchaguzi lazima ijiridhishe kama kanuni hizo zinakidhi matarajio ya
wananchi ili watu wanaokuwa na mashauri ya uchaguzi mahakamani yaamuliwe kwa
namna ambayo wanaridhika kwamba maamuzi hayo yamefanyika kwa kuzingatia Katiba
na Sheria za nchi.
Ameeleza kuwa, baadhi ya changamoto
zilizoonekana katika Kanuni hizo ni pamoja na kukosekana kwa uwazi na uhakika
pamoja na mapungufu mengine yatakayobainika baada ya kuzipitia kanuni hizo.
Kufuatia maelekezo ya
Jaji Mkuu kuhusu mabadiliko ya kanuni za uchaguzi, Majaji wa Mahakama ya Rufani
kwa pamoja wamepanga kukutana Jumatatu tarehe 22 Septemba, 2025 ili kupitia
kanuni hizo za uchaguzi na kutoa mapendekezo ya maboresho yake.
Aidha, Mhe. Masaju
ameeleza kwamba, mashauri yanayotokana na migogoro ya uchaguzi yatasikilizwa
katika Mahakama zilizopo nchini na kuwataka watu wanaohitaji kufuatilia
mashauri hayo kufika katika Mahakama husika wasikilize kwa amani na kwa kufuata
na kuheshimu taratibu za Mahakama. Ametoa rai kwa mtu ambaye hataridhika na
uamuzi wa Mahakama ya ngazi fulani ana haki ya kukata rufaa kwa kuwa ni haki ya
kikatiba.
Mhe. Masaju amesisitiza
kuwa, Mahakama inalo jukumu la kudumisha utawala wa sheria katika nchi kwa
mujibu wa Ibara ya 26 ya Katiba ambapo amethibitisha kwamba Mahakama
itahakikisha inaendelea kufanya hivyo.
“Pamoja na mamlaka tuliyo
nayo ya kikatiba na kisheria, mamlaka yetu pia yapo katika uwezo wetu wa
kufanya maamuzi ya Mahakama kwa maslahi ya sheria, amesema Jaji.
Kadhalika, Jaji Mkuu ameeleza
kwamba hakutakuwa na urushaji mubashara (live streaming) ya mashauri hayo na
kusisitiza kuwa, “hakutakuwa na ‘live streaming’ ya mashauri hayo huku akirejea
kinachozungumziwa kwenye Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwa; ni haki ya kupata taarifa sio haki ya kutangazwa wakati wote.
Katika hatua nyingine amewashukuru
waandaaji wa mafunzo hayo Mahakama na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA)
Lushoto, wawezeshaji pamoja na washiriki wote wa mafunzo hayo kushiriki
kikamilifu.
“Nawashukuru washiriki
wote, waandaaji na Wawezeshaji wa Mafunzo haya ambayo niliyafungua tarehe 28
Agosti, 2025 lakini katika ngazi mbalimbali, tulianza na Mahakama Kuu kwa
pamoja, Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi
na za Wilaya, zoezi ambalo limefanyika kwa ustadi mkubwa sana,” amesema Mhe.
Masaju.
Kwa upande wake Jaji Mkuu
Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman ametoa uzoefu wake
kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani juu ya mashauri yatokanayo na migogoro ya
uchaguzi ambapo ameshauri juu ya menejimenti fasaha ya mashauri ya uchaguzi kwa
kuwa yanagusa Taifa, kuwa na matumizi fasaha ya lugha na mengine.
“Tuwajibike ipasavyo na
tutumie uchaguzi huu kujiimarisha kama Mahakama kupitia maamuzi yetu kujenga
‘integrity’ ya Mahakama,” amesema Mhe. Chande.
Jaji Mkuu huyo Mstaafu
amesisitiza mambo ya kuzingatia kuwa ni pamoja na Mahakama kuangalia Sheria na
wajibu wake kwenye masuala ya uchaguzi, usikilizwaji wa mashauri ya uchaguzi
mapema ipasavyo na Mahakama iwe na uwazi na yenye kufikika kwa kuwa mashauri hayo
yana maslahi ya umma.
Mhe. Chande amesema, mafunzo
hayo yamekuja wakati muafaka kwa kuwa uchaguzi na migogoro ya uchaguzi kwa
kiasi kikubwa ni muingiliano kati ya siasa na sheria.
Majaji wengine
walioshiriki kutoa uzoefu wao kuhusu mashauri ya migogoro ya uchaguzi ni Majaji
wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Ferdinand Wambali na Mhe. Issa Maige.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa
na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA)
Lushoto yalifunguliwa na Jaji Mkuu tarehe 28 Agosti, 2025 lengo likiwa ni
kuimarisha uwezo wa Maofisa Mahakama, yaani Majaji na Mahakimu katika namna
bora ya kuendesha mashauri ya uchaguzi ili kuwaweka tayari kushughulikia mashauri
hayo kwa weledi na mapema ipasavyo pale ambapo wadaawa watakuwa wamegonga
milango ya Mahakama kutafuta haki.
Kwa mujibu wa Jaji wa
Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe.
Dkt. Paul Kihwelo mafunzo hayo yametolewa kwa jumla ya washiriki 381
wakiwemo Majaji wa Mahakama Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili,
Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba ya kufunga Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi leo tarehe 18 Septemba, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Aliyeketi kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Ferdinand Wambali.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya kufunga Mafunzo ya namna Bora ya Uendeshaji Mashauri ya Uchaguzi yaliyokuwa yakitolewa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 18 Septemba, 2025 jijini Dodoma. Kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Ferdinand Wambali.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni