Ijumaa, 19 Septemba 2025

MBEYA YAFANYA MAANDALIZI YA VIKAO VYA USIKILIZAJI MASHAURI YA MAUAJI

Na. Daniel Sichula – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga afungua kikao cha awali cha maandalizi ya usikilizwaji wa mashauri ya kesi za mauaji kwa mwaka 2025/2026 ambapo mashauri hayo yataendeshwa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya na Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Akitoa taarifa ya tathimini Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu alisema kuwa mashauri 16 yamepangwa kusikilizwa kuanzia tarehe 22 Septemba 2025 ambapo Mashauri 08 yatasikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga na mashauri 08 yatasikilizwa Mbeya mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa.

Baada ya kupokea taarifa ya tathimini kutoka kwa Mhe. Temu wajumbe walijadili juu ya changamoto zinzoweza kujitokeza na namna ya kuzitatua kabla ya usikilizwaji wa mashauri kuanza ikiwepo ya mahabusu walioko mbali na sehemu ambako mashauri yao yatasikilizwa.

 Akiwasilisha hoja Afisa Magereza alisema Mhe. Jaji watu wote wapo mahabusu ila kuna baadhi ya mahabusu wapo Mbeya na mashauri yao yatasikilizwa Songwe na bado hawajafuatwa.

Akijibu hoja hiyo Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya, Mhe. Temu alisema kuwa “maandalizi yote yameshakamilika na wadaawa wamepelekewa wito wa kuitwa Mahakamani wakiwemo walioko Songwe na muda wowote kuanzia hivi sasa mahabusu hao watakuwa wamesha fuatwa kwa ajili ya kusikiliza mashauri yao huko Songwe”.

Akiwasilisha taarifa kutoka Ofisi ya waendesha mashtaka mkoa wa Mbeya (NPS), kuwa kwa upande wao hakuna changamoto yoyote kwenye mashauri yatakayoingia kwenye vikao hivyo.

“Mhe. Jaji, mashahidi wamepigiwa simu na kupewa wito wa kufika mahakamani na wametoa ushirikiano wa kutosha na kuthibitisha kuwa wapo tayari kuja kutoa ushahidi wao” alisema mwakilishi kutoka ofisi ya mwendesha mashitaka mkoa wa Mbeya (NPS).

Kwa upande wa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkoa wa Songwe waliwasilisha taarifa za mashauri 08 yanayotarajiwa kusilikilizwa mkoani Songwe na walithibitisha kuwa hakuna changamoto yoyote na wapo tayari kwa vikao hivyo.

Aidha, Mawakili wa utetezi nao pia walitoa taarifa zao kuwa nao hawana changamoto yoyote mandalizi yanaendelea vizuri na wako tayari kwa vikao hivyo kuwasimamia wateja wao.

“Niwapongeze washiriki wote, Ofisi ya NPS, Ofisi ya RCO Mbeya na Songwe na Mawakili wa kujitegemea kwa hatua mlizofikia na kuonesha kuwa hadi sasa hakuna changamoto yoyote na mupo tayari kwa ajili ya usikilizaji wa mashauri yaliyopo mbele yetu na kuwasisitiza muda tuliokubalina hapa wa kuanza kusikiliza mashauri yaliyopo mbele yetu tuuzingatie,” alisema Mhe. Tiganga

“Matarajio ni kumaliza kesi zote za vikao hivi vilivyoandaliwa na ninawahakikishia kuwa tumejipanga na kesi zote zitasikilizwa na kumalizika, ninawasisitiza kuwa wepesi kubadilika kuendana na mazingira ya hali yoyote ya mabadiliko itakayojitokeza.” Mhe. Jaji Tiganga alisema.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Mbeya Bi. Mavis Miti, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Gereza Mbeya, Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Mbeya na Songwe na Ofisi ya Waendesha Mashtaka (NPS) Mkoa wa Mbeya na Songwe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga (kushoto) akiwa na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu wakiongoza kikao cha awali cha tathimini usikilizaji wa mashauri ya mauaji kwa Mahakama Kuu Mbeya na Mahakama Mkoa wa Songwe.

Sehemu ya washiriki katika kikao cha awali cha tathimini usikilizaji wa mashauri ya mauji.

Sehemu ya washiriki katika kikao cha awali cha tathimini usikilizaji wa mashauri ya mauji.

Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti akiwa mmoja ya washiriki wa kikao hicho

Afisa Magereza akichangia maoni yake katika kikao hicho

Sehemu ya washiriki katika kikao cha awali cha tathimini usikilizaji wa mashauri ya mauji

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni