Jumatano, 24 Septemba 2025

WATUMISHI MAHAKAMA KUU KANDA YA DODOMA WAPATIWA ELIMU YA MIFUKO YA UWEKEZAJI

Na. ARAPHA RUSHEKE – Mahakama Kuu, Dodoma

Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, pamoja na Mahakama za Mwanzo Dodoma mjini hivi karibuni wameshiriki mafunzo maalum ya elimu ya mifuko ya uwekezaji yaliyoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uelewa katika eneo la uwekezaji.

Mafunzo hayo yalitolewa na mtaalamu wa masuala ya uwekezaji kutoka katika mfuko wa uwekezaji [UTT AMIS], Bw. Ahmed Ismail katika ukumbi wa mikutano wa IJC.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo aliwataka watumishi hao kuyazingatia yote watakayofundishwa kwani yana faida kwa wakati wa baadaye pamoja na wakati wa kustaafu kazi.

“Natamani kila moja asikilize kwa umakini mambo yote yatakayofundishwa ili tujijengee uelewa katika masuala ya uwekezaji, naamini elimu itatupa msukumo mkubwa kwa wote kuweza kujiunga na mifuko hii ya uwekezaji kwa ajili ya faida yako kwa wakati ujao na wakati wa ustaafu,” alisema Mhe. Masabo.

Kwa upande wake, Bw. Ismail alibainisha kuwa kuna faida nyingi kwenye uwekezaji ikiwemo fedha kuwa salama, kutokuwa na tozo zozote kama mabenki na kupata gawio la faida kutokana na faida ya uwekezaji.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa yale yanayoratibiwa na kutolewa kwa watumishi kwa lengo la kuwajengea uwezo, maarifa na ujuzi katika nyanja mbalimbali za kikazi na maisha yao kwa ujumla.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Dkt. Juliana Masabo (aliyesimama) akitoa neno la ufunguzi wa mafunzo hayo.

Mwezeshaji wa mafunzo ya uwekezaji kutoka UTT – AMIS, Bw. Ahmed Ismail alipokuwa akiendesha mafunzo hayo ya uwekezaji katika mifuko mbalimbali ya uwekezaji.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama walioshiriki katika mafunzo hayo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni