Na. Hilary Lorry –
Mahakama, Lindi
Watumishi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Mahakama ya Wilaya ya Lindi pamoja na Mahakama
ya Mwanzo Lindi mjini wameshiriki mafunzo maalum ya afya ya akili
yaliyoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto ya
afya ya akili.
Mafunzo hayo
yametolewa na mtaalamu wa afya ya akili, Dkt. Monica Gloria katika ukumbi wa
wazi wa Mahakama ya Hakimu MKazi Lindi tarehe 19 Septemba, 2025.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi
Bi. Quip Godfrey Mbeyela amewataka watumishi hao kuyazingatia watakayo
fundishwa na daktari huyo bingwa wa Afya ya akili kwani suala la changamoto ya
afya ya akili limekuwa likiwasumbua watu wengi.
“Natamani
kila moja asikilize kwa umakini mambo yote yatakayofundishwa hapa ili
tujijengee uwezo wa kukabili changamoto za afya ya akili, naamini elimu hii
itatusaidia kukabili changamoto za afya ya akili mahala pa kazi, katika familia
zetu na hata kwa jamii inayotuzunguka” alisema Mtendaji huyo”.
Kwa upande
wake, Dkt. Monica amebainisha kuwa changamoto ya afya ya akili ni ya kweli na imekuwa
ikiathiri utendaji kazi wa watumishi wengi katika maeneo mbalimbali hasa katika
kutekeleza majukumu yao.
Vilevile Dkt. Monica alifundisha mambo yanayoweza kupelekea mtu kuwa na changamoto ya afya ya akili, dalili/ishara za changamoto ya afya ya akili na jinsi ya kukabili changamoto ya afya ya akili pamoja na njia tano zinazoweza kusaidia kukabiliana na msongo ambao unapelekea changamoto ya afya ya akili, njia hizo ni kuishi (Five A’S ambazo ni Avoid, Act, Alter, Accept And Adopt) akifafanua vipengele hivyo alisema tunatakiwa kujiepusha na mambo yanayosababisha Msongo, kufanya mambo yatakayo kuepusha na msongo wa mawazo, kuzungumza mambo yanayokusababishia msongo kwa mtu unayemwamini,kukubaliana na hali na mazingiza na mwisho kuishi katika hali yako kwakuzingatia mazingira yako.
“Tukifanikiwa
kuishi mambo hayo matano basi tutakuwa tumefanikiwa kupambana na tatizo la afya
ya akili,” ameeleza Dkt. Monica, huku akihamasisha watumishi hao kujijengea
tabia ya kujitambua na kutafuta msaada mapema pindi wanapohisi mabadiliko
katika afya ya akili.
Uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi umeweka bayana kuwa Mafunzo haya yatakuwa endelevu na sehemu ya mikakati ya kuboresha ustawi wa watumishi na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.
Daktari kutoka hospitali ya Rufaa ya
Sokoine Lindi Bi. Monica Gloria (aliyesimama mbele) akitoa elimu ya afya ya
akili kwa watumishi wa Mahakama ya Lindi (hawapo kwenye picha).
Msaidizi wa
Kumbukumbu Mwandamizi Bw. Selemani Chikumba (aliyesimama) akitoa neno la shukrani
kwa niaba ya watumishi baada ya Mafunzo.
Watumishi wa Mahakama ya Lindi
wakifuatilia kwa makini Mafunzo ya Afya ya akili yaliyowasilishwa Dkt. Monica.
Mtendaji wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip godfrey Mbeyela (kushoto) akiwa na Hakimu
Mkazi Mahakama ya Wilaya ya Lindi Mhe.Khalfan O. Khalfan (kulia) wakifuatilia
mafunzo hayo.
Hakimu Mkazi
Mahakama ya Wilaya ya Lindi Mhe. Khalfan O.Khalfan Akichangia mada wakati wa
Mafunzo.
Mkaguzi wa
ndani Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bw. Faustine Peter Alo (benchi la pili kutoka
mbele kushoto) akiuliza jambo wakati wa Mafunzo.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni