Jumanne, 23 Septemba 2025

MAJAJI WA ZANZIBAR WATEMBELEA MANYARA KWA AJILI YA ZIARA YA MAFUNZO

Na. Christopher Msagati – Mahakama, Manyara

Mahakama Kuu Kanda ya Manyara imewapokea Majaji wanne kutoka Mahakama Kuu Zanzibar kwa ajili ya ziara ya mafunzo ya wiki moja ili kubadilishana uzoefu katika shughuli za uendeshaji wa mashauri mbalimbali yakiwemo mashauri ya uhujumu uchumi yatayaoanza kusikilizwa Mahakamani hapo hivi karibuni.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya Majaji hao, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora aliwapongeza wageni hao kwa kuichagua Mahakama Kuu Manyara kwa ajili ya kujifunza kwa kuwa Mkoa wa Manyara una mashauri ambayo katika Kanda nyingine huwa hayasikilizwi kwa wingi kama ilivyo katika Kanda ya Manyara.

“Waheshimiwa Majaji karibuni sana Manyara na ninawapongeza kwa kuichagua Kanda yetu kwa ajili ya kujifunza, Kanda yetu ina mashauri mengi sana yanayohusu Uhujumu Uchumi, Madawa ya Kulevya na Nyara za Serikali. Hivyo ninaamini kuwa mmechagua Kanda sahihi kwa ajili ya mafunzo yenu” alisema Mhe. Jaji Kamuzora.

Majaji ni Mhe. Fatma Hamidi Mahmoud, Mhe. Said Hassan Said, Mhe. Salma Ali Hassan pamoja na Mhe. Khadija Shamte Mzee. Katika ziara hiyo wameambatana pia na Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mhe. Hussein Makame Hussein.

Akiongea wakati wa mapokezi hayo, Mhe Fatma Mahmoud Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar aliushukuru uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kwa kuwapokea na kuwawezesha kupata mafunzo hayo.

“Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara tunawashukuru kwa kutupokea na kutuwezesha kuyapata mafunzo haya. Tunaamini katika wiki nzima hii ambayo tutakaa pamoja tutajifunza mengi kutoka kwenu na tukirudi Zanzibar yatakuwa tija katika utendaji kazi wetu” alisema Mhe. Fatma Mahmoud.

Mahakama Kuu Manyara imeanza kikao cha wiki moja cha kusikiliza mashauri ya Uhujumu Uchumi ambacho kinaongozwa na Mhe. Jaji Devotha Kamuzora kuanzia tarehe 22 Septemba 2025 mpaka tarehe 26 Septemba 2025. Kikao hiki ndicho kinachotumiwa na Majaji hao kutoka Zanzibar kwa ajili ya kujifunza mienendo ya mashauri ya Uhujumu Uchumi.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora (wa nne kutoka kushoto) akiwa pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar waliofika Manyara kwa ajili ya Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uhujumu Uchumi. 


Waheshimiwa Majaji wakiwa wanaangalia ukumbi wa Wazi wa Mahakama Kuu Manyara ambao ungetumika kabla ya kuanza mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uhujumu Uchumi.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora akiwatembeza na kuwaonesha miundombinu ya Mahakama Kuu Manyara kabla ya kuanza kwa mafunzo.

Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar Mhe. Khadija Shamte Mzee  akiangalia chumba cha kuhifanyia nyaraka mbalimbali kinachotumiwa na Mahakama Kuu Manyara, akimeambatana na Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar Mhe. Salma Ali Hassan.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora  akiwakaribisha waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar ambao wametembelea Mahakama Kuu Manyara kwa ajili ya Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uhujumu Uchumi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni