Jumatatu, 29 Septemba 2025

WATUMISHI WA MAHAKAMA DODOMA WAJENGEWA UELEWA KUPITIA CHAKULA CHA UBONGO

Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma.

Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma pamoja na wale wa Mahakama za Wilaya tarehe 26 Septemba 2025 walishiriki katika mafunzo ya Chakula cha Ubongo yaliyolenga kuongeza uelewa na stadi za kiutendaji.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Evaristo Longopa katika ukumbi wa Mahakama Kuu uliopo Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma (IJC). Sehemu ya washiriki walihudhuria moja kwa moja na wengine kwa njia ya mtandao kupitia kiungo maalumu (link).

Katika kikao hicho, mada ya kwanza ilihusu “Jinsi ya Kukabiliana na Vikwazo Mahali pa Kazi” iliyowasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii na Mratibu wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, Bi. Mwanaamini Mtoo.

Mada ya pili ilikuwa “Maadili katika Utumishi wa Umma” iliyotolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Maadili kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, Bi. Janeth Mishinga.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mhe. Dkt. Longopa alisisitiza umuhimu wa mafunzo ya aina hiyo kwa watumishi wa Mahakama akibainisha kuwa:

“Maadili na uwezo wa kukabiliana na changamoto kazini ni nguzo kuu za ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wananchi, ni wajibu wa kila mtumishi kuyazingatia haya kwa vitendo kila siku.”

Kupitia mafunzo hayo, watumishi walipata fursa ya kujifunza mbinu za kukabiliana na changamoto za kikazi pamoja na kuimarisha maadili, jambo linalotarajiwa kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.



Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Evaristo Longopa  akifungua kikao cha Chakula cha Ubongo kilichojumuisha watumishi wa Mahakama Kuu na Mahakama za Wilaya kupitia ushiriki wa moja kwa moja na mtandaoni.”.

 

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Evaristo Longopa (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi wa mafunzo hayo. Kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii na Mratibu wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, Bi. Mwanaamini Mtoo na kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Maadili kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, Bi. Janeth Mishinga.



 Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini.

Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii na Mratibu wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa kutoka Ofisi ya Rais, Utumishi, Bi. Mwanaamini Mtoo akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Maadili kutoka Ofisi ya Rais Utumishi, Bi. Janeth Mishinga akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma. Mhe. Dkt. Evaristo Longopa (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni