- Awaasa kuviishi viapo vyao
·
Awasisitiza kutekeleza majukumu kwa
kuzingatia Katiba na Sheria za Nchi
·
Awataka kuzingatia Kanuni za Kimahakama
ikiwemo kutochelewesha haki bila sababu za kimsingi
·
Awasihi kutoendekeza masharti ya
kiufundi katika kazi ya utoaji haki
·
Ahimiza utatuzi wa migogoro kwa njia
ya usuluhishi
·
Awataka pia Mahakimu hao waliokuwa na
chembechembe za uanaharakati na siasa kuacha mara moja
Na
MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 07 Oktoba, 2025 amewaapisha jumla
Mahakimu Wakazi wapya 89 na kuwataka kuviishi viapo vyao wanapokeleza majukumu
yao.
Hii ni mara ya kwanza kwa
Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kufanya uapisho wa Mahakimu hao wapya tangu kuapishwa
kwake kushika nafasi hiyo miezi mitatu iliyopita.
Akizungumza na Mahakimu
hao mara baada ya kuwaapisha kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju amewapongeza Mahakimu hao na
kuwataka kuviishi viapo vyao sawasawa na walivyoapa.
“Nina machache sana ya
kuwashauri leo, moja karibu kila mmoja aliyekula kiapo hapa alikuwa ameshika
Biblia au Quran, hivyo nikaamini kwamba tunatambua uwepo wa Mwenyezi Mungu,
ushauri wangu kwenu ni kwamba nendeni mkiishi hicho kiapo sawasawa na jinsi
mlivyoapa, ninapenda kuamini kwamba mlipokuwa mnaapa hiki kiapo mlikichukulia
kwa dhati basi enendeni mkakiishi hiki kiapo,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesisitiza
kuwa, “Mungu hadhihakiwi, unachokipanda ndicho utakachokivuna, kama ulishika
Biblia au Quran ukayatamka yale maneno kuanzia kuwa muaminifu kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kufanya maamuzi yako kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Sheria za Nchi na mila na desturi za Tanzania na bila
upendeleo, chuki, uwoga na huba nendeni mkaishi hicho kiapo hicho ndicho
mlichopanda na ndicho mtakachovuna.”
Aidha, Jaji Mkuu
amewahakikishia Mahakimu hao kwamba, wao kama Viongozi, Walezi lakini pia kama
wazazi wao wanawapa baraka zote kama wataenda kukiishi kiapo hicho kwa kuwa
wamepewa heshima kubwa.
“Baada ya uapisho huu,
mtaenda kwenye mafunzo elekezi na pale tutawakuta Viongozi wetu wa dini
watawashauri na kuwaasa kila mmoja hapa ili mnavyotenda shughuli zenu hizi mjue
kwamba mnapaswa kuzitenda, mnasimama badala ya Mwenyezi Mungu hapa duniani na
wengi wenu mtaenda kufanya kazi vijijini, mtakuwa watu wa kipekee sana huko
vijijini, wataendelea kuwaheshimu na ninyi waheshimuni wale watu wanaokuja
mbele yenu muwatendee kwa haki sawasawa na viapo vyenu,” amesema Mhe. Masaju.
Amewasisitiza kutenda
haki sawa kwa wote bila kuwasahau wajane, maskini, yatima hivyo wasichukulie
kigezo cha unyonge wa makundi hayo kupora haki zao kwa kutumia kalamu zao.
“Anayewaonea watu hao,
Mungu atamuadhibu lakini na sisi tuna utaratibu wa kuwajibishana, niwaombeni
sana tumekuwa na utaratibu hapa kwamba wanaokiuka maadili ya utumishi wetu,
tunawachukulia hatua za kinidhamu kwa utaratibu tunaouweka, kama ukiukwaji wa
maadili yetu pia ni kosa la jinai mimi ningependa huyu mtu tumpeleke Mahakamani
kwanza na yeye ajifunze badala ya kumsimamisha tu halafu kufanya mchakato wa
ushughulikiaji wa nidhamu ambao nao unachukua muda mrefu, kwa hiyo kukiwa na
ushahidi wa kutosha, Vyombo vya Dola vinavyohusika na kutekeleza iwe ni Jeshi
la Polisi, iwe ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
watachukua hatua ipasavyo hakutakuwa na cha kusema kwamba huyu ni Hakimu au ni
nani,” ameeleza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju ameongeza kwa
kurejea kauli iliyotolewa na Hayati Mwalimu Nyerere alipokuwa anahutubia
mkutano wa Majaji mwaka 1981 jijini Arusha alisema, “Zipo kazi zinazoweza
kufanywa na watu tunaowatilia mashaka lakini Uhakimu na Ujaji sio mojawapo ya
kazi hizo, Jaji au Hakimu akitiliwa mashaka hata kama ushahidi hautoshi ni
lazima aanze kuchunguzwa mara moja.”
Aidha, Jaji Mkuu
amewaeleza Mahakimu hao kuhusu Kanuni zitakazowaongoza katika utumishi wao
ambazo zinapatikana kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 107A,
107B na Ibara ya 26. Ibara ya 107A inasema,
‘Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano
itakuwa ni Mahakama.’
“Masuala ya haki mamlaka
yenye kauli ya mwisho ni Mahakama, ni kana kwamba tunachukua nafasi ya Mungu
hapa duniani hapa Tanzania, ndio maana nawasisitiza kwamba haya mlioapa muende
muyaishi, mtakuwa na kauli ya mwisho haijalishi wewe ni Hakimu wa Mahakama ya
Mwanzo ambayo ni Mahakama ya ngazi ya chini kabisa katika mfumo wa Mahakama za
Tanzania bado utakuwa na hiyo kauli ya mwisho na kama mtu hajaridhika na uamuzi
wako atakata rufaa Mahakama ya Wilaya na pengine hadi Mahakama ya Rufaa,”
amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu ameongeza
akirejea Ibara 107A(2) isemayo, “katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na
jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo: - a) Kutenda
haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi b) Kutochelewesha
haki bila sababu ya kimsingi c) Kutoa fidia ipasavyo kwa watu wanaoathirika
kutokana na makosa ya watu wengine na kwa mujibu wa Sheria mahsusi iliyotungwa
na Bunge d) Kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika
migogoro na e) Kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kifundi
yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.
Aidha, amewasihi Mahakimu
hayo kutoa ushauri wa kufanya usuluhishi kati ya wadaawa ikiwa ni pamoja na
kuwaelimisha wadaawa faida na hasara za kuendelea au kutoendelea na shauri
Mahakamani.
“Sio wajibu wenu
kuwasuluhisha lakini ni wajibu wenu kuwashauri kwamba jamani ninyi ni
wanandugu, halafu tena pengine ninyi ni majirani mgogoro wenu huu ninavyoona
mnaweza kuumaliza tu kindugu au kifamilia maisha yakaendelea,’ amesema Mhe.
Masaju.
Kadhalika, Jaji Mkuu
amewaeleza Mahakimu hao kwamba Mahakama za Mwanzo kimsingi zilikusudiwa ziwe
Mahakama za upatanishi na ndio maana makosa yote ya jinai yanayosikilizwa na
Mahakama za Mwanzo yote yanadhaminika lakini pia hata mtu asiye na mdhamini
anaweza akajidhamini.
“Na kwa sababu hiyo
tumeelekeza kwamba Mahakama za Mwanzo zisipeleke watu Mahabusu na mpaka sasa
hakuna hata Mahabusu mmoja wa Mahakama za Mwanzo katika Magereza yetu ya
Tanzania, matumaini yetu ni kwamba nanyi mtaenda kuanzia hapo muendelee, msije
mkasema mnakuja na ufundi fulani, makosa yote ya jinai yanayosikilizwa Mahakama
za Mwanzo yanadhaminika, kama mtu ana wadhamini watamdhamini na kama amekosa
wadhamini kwa namna yoyote ile aruhusiwe kujidhamini,” amesisitiza Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amesema kwamba,
kuna kanuni za msingi ambazo hawawezi kuzipuuza, hivyo ni muhimu Maafisa hao
kuzingatia vitendea kazi vya utendaji kazi ikiwa ni pamoja kutenda haki na
kujiridhisha kama haki imetendeka ‘sensitive to justice’, waweze pia
kujiongeza, kuwa waadilifu, kujituma kufanya kazi, kuwa wabunifu ili kuimarisha
ufanisi, kuwa na uzalendo wa Taifa.
Mhe. Masaju ameongeza
kuwa, “Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nayo ni moja
ya Kanuni zinazoongoza utendaji kazi wa Mahakama, nayo inasema, ‘Katika
kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia
tu masharti ya Katiba na yale ya Sheria za Nchi.’
Ameeleza kwamba, uhuru
huo unapatikana kwa kuzingatia mambo matatu ambayo ni pamoja na kuzingatia Katiba
na Sheria za Nchi, kuzingatia maadili ya utumishi wa Maafisa wa Mahakama
(Mahakimu na Majaji) na kuzingatia kiapo. Hivyo, amesema kwamba Maafisa hao
wakishindwa kusimamia hayo watashindwa kuwa huru kutekeleza majukumu yao ya
utoaji wa maamuzi.
“Kwa mfano kwa wale
wanaokula rushwa, ukishakula rushwa una uhuru gani? Mtapendelea, ukisema huyu
ni ndugu yangu ni kabila langu, sijui tunasali wote pamoja hapo tena huwezi
kuwa huru, kwahiyo niwaombeni tunapata nguvu hii sisi ya kuwa kauli ya mwisho
ya kutoa haki kwa sababu tunakuwa huru tunapokuwa tunafanya maamuzi,”
amesisitiza Jaji Mkuu.
Amesema Serikali
inachukua hatua za kuboresha maslahi ya Watumishi wa Mahakama, hivyo amewataka
Mahakimu hao kwenda kufanya kazi kwa amani na kutoweka sababu mbalimbali
ikiwemo mshahara mdogo kutokuwa kigezo cha kuchukua rushwa.
Aidha, Mhe. Masaju
amewataka Mahakimu hao kutenga muda wao kusikiliza hotuba na maelekezo ya
Viongozi wa Kitaifa wakiwemo Viongozi wa Kitaifa wa Mahakama ya Tanzania kwa
sababu maelekezo yanapatikana kwenye Katiba, Sheria lakini pia yanapatikana kwa
Viongozi wa Serikali ambayo inajumuisha Mahakama. Amewasisitiza pia Mahakimu
kuisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na kudumisha utawala
wa sheria.
Katika hatua nyingine,
Jaji Mkuu amewasihi Mahakimu hao kuendelea kuwajali wazazi wao, wenza wao licha
ya kuwa wamepata nafasi hiyo ambapo amesema, “Wakati mnaapa wengine nimewaona
wana pete kuashiria kwamba ni wanandoa, sasa mafanikio haya mliyoyafikia leo
yasije yakawatenganisha kwenye ndoa zenu, msifanye hivyo endeleeni kuheshimiana
na wale ambao hamjapata ndoa endeleeni kujiheshimu mpaka hapo mtakapofikia
hatua ya kuwa na ndoa lakini pia mtaendelea kujiheshimu maisha yenu yote.”
Baada ya hafla ya
uapisho, Mahakimu hao wapya watapatiwa mafunzo elekezi ya siku 10 ili kupatiwa
‘abc’ za utendaji wa kazi ya uhakimu kabla ya kwenda kuanza kufanya kazi hiyo
rasmi katika Vituo walivyopangiwa.
Sehemu ya ndugu, jamaa na marafiki wa Mahakimu Wakazi waliofika kushuhudia uapisho wa Maafisa hao wa Mahakama.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni