Jumanne, 7 Oktoba 2025

MAHAKAMA KUU MBEYA WATEMBELEA GEREZA KUU RUANDA

Na. Muksini Nakuvamba - Mahakama, Mbeya

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Saidi Kalunde amefanya ziara ya kutembelea Gereza Kuu Ruanda Mbeya jana tarehe 06 Oktoba, 2025 kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea gerezani hapo pamoja na kusikiliza changamoto za wafungwa na mahabusu gerezani hapo.

Ziara hiyo ilianza kwa kupokea taarifa ya Gereza Kuu Ruanda kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Gereza SSP Grace Mbedule ili kufahamu taarifa kamili ya changamoto za wafungwa na mahabusu gerezani hapo.

Katika taarifa hiyo alieleza hali za wafungwa na mahabusu waliopo Gerezani hapo, ambapo kwa sasa kuna jumla ya Wafungwa 681 na Mahabusu 196. Kaimu hiyo Mkuu wa Gereza SSP Mbedule alieleza changamoto zinazolikabili Gereza Ruanda kwa kusema.

“Mhe. Jaji mfawidhi, Gereza letu linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ucheleweshwaji wa upelelezi wa kesi suala linalopelekea kuwa na mrundikano mkubwa wa mahabusu, sambamba na hilo pia kuna Kasha kwa ajili ya Mahakama mtandao ambalo limekamilika isipokuwa samani zake hazijaletwa ili lianze kutumika, kwa sasa Mahakama mtandao inaendeshwa ndani ya gereza,” SSP Mbedule alisema

Taarifa hiyo ilihitimishwa kwa kumuomba Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Kalunde kuongeza ushirikiano na vyombo vingine vya haki jinai ili kukamilisha upelelezi wa kesi kwa wakati ili kukabiliana na changamoto ya msongamano wa mahabusu gerezani hapo.

Aidha, Mhe. Kalunde alifanya ukaguzi gerezani hapo kwa kutembelea sehemu za kulala wafungwa na mahabusu, Zahanati, jikoni na sehemu ya kugawia chakula wafungwa na mahabusu.

“Niwapongeza kwa kuwa na sehemu nzuri ya kuandalia chakula na pia alipongeza matumizi ya nishati ya Gesi na makaa ya mawe kwa kupikia chakula cha wafungwa na mahabusu,” alisema Mhe. Jaji.

Katika ziara hiyo Mhe. Kalunde alikutana na Wafungwa na Mahabusu ambao waliwasilisha changamoto zao kwa Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Temu.

Katika risala iliyosomwa na wafungwa na mahabusu walieleza changamoto zao zinazowakabili na mapendekezo yao kwa Mhe. Jaji Mfawidhi na naibu msajili mfawidhi “Tunaomba idadi ya mashauri yanayosikilizwa kuongezwa ili kuturahisishia kupata haki zetu. Pia tunamuomba Naibu Msajili awe anatutembelea gerezani mara kwa mara ili kutusikiliza shida zetu,” alisema mfungwa mmoja msomaji wa risala hiyo.

Mhe. Kalunde vilevile, alitoa fursa kwa Wafungwa na Mahabusu wenye shida binafsi kwake na kwa Naibu Msajili mfawidhi na wadau wengine wa haki jinai alioambatana  kuonana nao kwa utaratibu uliowekwa na waliweza kusikilizwa shida zao.

Vilevile, Mhe. Kalunde alitembelea Gereza Kuu Ruanda upande wa Wanawake ambapo kwa upande huo pia alipokea risala ya Wafungwa na Mahabusu Wanawake ambapo nao waliwasilisha changamoto zao.

Mhe. Kalunde pia alitembelea Kasha lilioandaliwa kwa ajili ya kutumika na Mahakama Mtandao na kujionea miundombinu yake na hatua iliyofikia.

Aidha, Mhe. Kalunde alihitimisha kwa kutoa shukurani kwa Uongozi wa Gereza, Wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Ruanda. “Nawashukuru kuwa pamoja nasi kuwasikiliza hoja zenu, tumezichukua na tutazifanyia kazi,” alisema Mhe. Kalunde

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Gereza akitoa shukurani zake kwa ujio wa ugeni huo, kwa kuwa umekuwa na tija kubwa kwao kwa kutoa fursa kadhaa ikiwemo kulipia ving’amuzi ya televisheni zinazotumiwa na Wafungwa na Mahabusu, kushughulikia suala la kupunguza mrundikano wa mahabusu na kutoa fursa ya michezo kwa Wafungwa na Mahabusu wa Gereza kuu Ruanda.

Katika ziara hiyo Mhe. Kalunde aliambatana na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu, Kaimu Mtendaji Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Bw. Ibrahim Mgallah, Msimamizi wa Kitengo cha Jinai Mahakama Kuu Mbeya, Mahakimu wakiongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Mwenyekiti TLS Chapta ya Mbeya, na wadau wengine wa Haki jinai.

Kaimu Mkuu wa Gereza Kuu la Ruanda SSP Grace Mbedule (katikati) akiwa na Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Said Kalunde (kulia) na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Temu (kushoto).


Kaimu Jaji mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Said Kalunde Akipokelewa na mwenyeji wake Kaimu mkuu wa gereza, Gereza kuu Ruanda SSP Grace Mbedule alipotembelea gerezani hapo.

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Said Kalunde na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Aziza Temu wakikagua miundombinu ya Kasha la mahakama mtandao.

Kaimu Jaji mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Said Kalunde na Kaimu mkuu wa gereza, Gereza kuu Ruanda SSP Grace Mbedule wakiwa kwenye matembezi ya ukaguzi Gereza Ruanda.

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Said Kalunde (wa saba kulia) akiwa na mwenyeji wake Kaimu mkuu wa gereza, Gereza kuu Ruanda SSP Grace Mbedule (kushoto), Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Aziza Temu (wa tano kushoto) wakiwa mbele ya lango la Gereza kuu Ruanda Mbeya.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni