· Watuma salamu za shukrani kwa Jaji Mkuu kufuatia hatua ya kuhakikisha watuhumiwa wote Mahakama za Mwanzo kudhaminiwa au kujidhamini
· Wasifu hatua ya kupatiwa nakala za hukumu na mienendo kwa wakati
· Wakoshwa na uendeshaji wa mashauri kwa Mahakama Mtandao
Na PAUL PASCAL, Mahakama-Moshi
Mahakama
Kuu Kanda ya Moshi imefanikiwa kutatua changamoto ya utoaji wa mienendo ya mashauri na
nakala za hukumu kwa wafungwa na wadaawa wote katika mashauri yaliomalizika na
yanayoendelea kumalizika kwa asilimia 100 na kusaidia kupunguza malalamiko kwa kiasi kikubwa.
Hayo
yalibainishwa hivi karibuni wakati wa ziara ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya na
Magereza ya Wilaya za Same na Rombo kwa Robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/2026
iliyofanywa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella.
Akitoa
salamu za ukaribisho wakati wa ukaguzi huo pamoja na kusoma taarifa fupi ya Gereza
la Wilaya Same, Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Same, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Ipyana
Thomson Mwakyusa alisema kuwa, mpaka kufikia tarehe 29 Septemba, 2025 Gereza
hilo lilikuwa na jumla ya wafungwa na mahabusu 90 ambapo wafungwa ni 74 wanaume
wakiwa 72 na wanawake wawili na mahabusu ni 16 pekee.
“Gereza
hili lina uwezo wa kubeba wafungwa na mahabusu 160, kwa takwimu hizo za
wafungwa na mahabusu nilizotoa, nikiri mbele kuwa Gereza letu linamudu
kuwahudumia wananchi hawa kipekee niwapongeze kwa kasi ya umalizaji mashauri
pamoja na kuwa na utaratibu mzuri wa dhamana uliowekwa kupitia maelekezo ya Mhe
Jaji Mkuu mambo haya ndio yametusaidia kupunguza mlundikano wa mahabusu katika
gereza letu hakika mnastahili pongezi,” alisema Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mwakyusa.
Aidha,
Mkuu huyo wa Gereza alimuomba Jaji Mfawidhi kufikisha salamu za pongezi kwa
Jaji Mkuu kwani kwa kipindi kifupi tangu ameteuliwa wameanza kuona kasi yake na
ya wasaidizi wake katika kumaliza changamoto zilizokuwa zinawakabili kubwa likiwa
ni mlundikano wa mahabusu.
Kadhalika,
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mwakyusa alimshukuru Jaji Mfawidhi wa Kanda ya
Moshi pamoja na Viongozi alioambatana nao kwa kufanya ukaguzi katika Gereza
hilo na kusema kuwa, hiyo ni ishara ya wazi ya kwamba wako pamoja katika
kuwahudumia wananchi.
Mara
baada ya ukaribisho huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Moshi, Mhe. Dkt Lillian Mongella alipata fursa ya kuzungumza na Wafungwa na Mahabusu
wa Wilaya ya Same na kuwaeleza lengo la ugeni wao pamoja na msafara wote wa
alioambatana nao.
“Ndugu
zangu kwanza niwape pole kwa haya yote mnayoyapitia pia niwatie moyo kwa kuwa
yote haya ni sehemu ya mapito ya maisha yetu sisi wanadamu niwajuze tu tuko
pamoja nanyi kwa wakati wote ndio maana leo tumeona ni vema kufika mbele yenu
tukiambatana safu nzima ya wahusika katika mnyororo wa utoaji haki jinai ili
tuweze kuwajulia hali, kuona mazingira yenu huku pamoja na kujadiliana endapo
kuna kikwazo chochote katika majukumu yetu niwaombe tuambizane mambo yote
tunayoyaona kama kikwazo kwenu katika zoezi zima la upatikanaji haki niwaahidi
yote yatakayosemwa hapa tunakwenda kuyatatua mimi pamoja na timu yangu,”
alisema Mhe. Dkt. Mongella.
Akizungumza
kwa niaba ya Wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Wilaya Same mmoja wa Wafungwa
alisema, “binafsi niwapongeze Mahakama kwani kwa sasa hakuna ucheleweshaji wa
nakala za hukumu, hakuna kupelekwa mahabusu kwa makosa madogo madogo na
kujazana magerezani pasipo sababu hatua hii mliochukua kiukweli ni utunzaji wa
haki za kibinadamu, sisi wafungwa wa Same hatuna lalamiko la kucheleweshewa
nakala zetu hivyo tumeweza kukata rufaa zetu tunasubiria haki itendeke asanteni
kwa kututembelea.”
Katika
ziara ya ukaguzi Gereza la Wilaya ya Same Jaji Mfawidhi aliambatana na Naibu
Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje, Mtendaji
wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bi Maria Itala, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe
Chrisanta Chitanda, Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo zilizoko Wilaya ya Same, Mkuu
wa Upelelezi Wilaya ya Same pamoja na Waendesha Mashtaka wa Wilaya hiyo.
Katika
hatua nyingine, naye Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi
aliongoza ukaguzi katika Gereza la Wilaya Rombo tarehe 01 Oktoba, 2025 ambapo
walitembelea na kukagua Gereza hilo pamoja na kusomewa na kupokea risala ya Wafungwa
na Mahabusu iliyobainisha kuridhishwa kwao kwa utendaji wa Mahakama Kuu Kanda
ya Moshi.
Akisoma
Risala ya Wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Wilaya Rombo, Mwakili wa Wafungwa alibainisha
juu ya uwepo wa Wafungwa na Mahabusu 116 kwenye Gereza hilo na kwamba lina
uwezo wa kubeba Wafungwa na Mahabusu 270.
Aidha,
Mfungwa huyo alilalamikia juu ya tabia ya kubambikiwa kesi iliyoshamiri katika Wilaya
ya Rombo ambapo alisema, “Mhe Jaji
tunashukuru kwa ujio wako, kiukweli kwa upande wa Mahakama hatuna lalamiko
lolote dhidi yenu kilio chetu ni kwa Polisi wanatubambikia kesi ambazo
hatujatenda na kuweka mashahidi wa uwongo nitawasilisha orodha ya
wanaolalamikia kitendo hicho, tunawashukuru Mahakama kwa kuboresha huduma zenu
hatudai nakala ya hukumu wala hatubabaishwi kwa namna yoyote tunapofika mahakamani,”
alisema Mfungwa huyo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Gereza la Wilaya Rombo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Omary
Gunda alibainisha changamoto zinazokabili Gereza hilo kwa sasa ni changamoto ya
mtandao kwa eneo hilo.
“Tunashukuru
Mahakama imetupatia TV ya kisasa kwa ajili ya kesi za mtandaoni ila tunashindwa
kuitumia ipasavyo kwa kuwa tu hatuna mkongo wa taifa katika eneo letu, vilevile
naleta kwako ombi la kupatiwa kontena maalum kwa ajili ya matumizi ya chumba
cha kusikilizia kesi kwa njia ya mtandao kama ambavyo mmefanya kwa Gereza Kuu
la Karanga naamini na sisi Rombo mtatuboreshea kwa namna hiyo,” alisema SSP
Gunda.
Akihitimisha
kwa kujibu hoja mbalimbali pamoja na kuazimia mambo yaliojadiliwa katika
ukaguzi huo, Mhe. Kilimi alisema, “ndugu zangu kwanza nishukuru kwa mapokezi na
ushirikiano mliouonyesha, pili niahidi yote tuliojadili tunayakwenda kuyafanyia
kazi lakini pia yote tulioazimia hapa kwa pamoja naamini tumeridhika.”
Aidha
Jaji Kilimi aliwapongeza kwa mazingira safi ya Gereza hilo na kusema kuwa, hiyo
ni ishara ya wazi kuwa wanarekebika na kuwaahidi kuwa Mahakama itafanyia kazi maombi
yote yaliyowasilishwa na Wafungwa na Mahakama hao na kupata majibu haraka
iwezekenavyo.
Katika ziara hiyo Jaji Kilimi aliambatana na Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt Casian Mshomba, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Rombo, Mhe. Innocent Nyella, Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo zilizoko Wilaya ya Rombo, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Rombo pamoja na Waendesha Mashtaka Wilaya ya Rombo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe Dkt. Lillian Mongella (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu na wadau wa Mahakama walioshiriki katika zoezi la ukaguzi wa Gereza la Wilaya Same uliofanyika hivi karibuni.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu na wadau wa Mahakama walioshiriki katika zoezi la ukaguzi wa Gereza la Wilaya Rombo uliofanyika hivi karibuni.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni