Na YUSUFU AHMADI-IJA, Dar es Salaam
Zaidi ya washiriki 25
kutoka Mikoa mbalimbali nchini wameanza kupatiwa mafunzo ya 15 ya udalali na usambazaji
wa nyaraka za Mahakama huku wakisisitizwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
watakazofundishwa katika utendaji wao wa kazi, kwa kuwa kosa dogo wakifanya linaweza
kuleta madhara kwao binafsi, kwa Mahakama na Taifa kwa ujumla.
Mafunzo hayo ya siku 15 yanayofanyika
katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania)
jijini Dar es Salaam yalifunguliwa hivi karibuni na Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo. Aidha mafunzo hayo
yameandaliwa na yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Opiyo alisema, “Majukumu haya msipoyatekeleza
vyema mtalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi na kwa hiyo ni dhahiri
kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa.”
Pia aliwahimiza washiriki
hao kutumia mafunzo hayo kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuongezeana maarifa na kuboresha
utendaji kazi ili kupunguza malalamiko yanayotokana na wananchi kutokupata
huduma bora.
Kwa upande wake, Mratibu
wa mafunzo ambaye pia ni Mhadhiri wa IJA, Bi. Fatuma Mgomba alisema kuwa ndani
ya siku hizo za mafunzo washiriki watapatiwa maarifa ya vitendo na nadharia
kutoka kwa wawezeshaji mahiri na hivyo kuzalisha Madalali na Wasambaza Nyaraka
wenye weledi wa kutekeleza amri za Mahakama.
Mafunzo hayo yatafanyika
kwa muda wa wiki mbili hadi tarehe 13 Octoba, 2025, yanalenga kutoa ujuzi wa
vitendo na nadharia kwa washiriki ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia kanuni, taratibu, sheria, maadili, weledi na ufanisi.
Baada ya mafunzo haya,
Washiriki watapimwa kwa kufanya mitihani ya umahiri wao na watakaofaulu
watapatiwa vyeti vinavyowapa sifa ya kuomba na kufanya kazi hiyo.
Mara baada ya kuhitimu
mafunzo, wahitimu watakuwa na sifa ya kufanya kazi za Mahakama na pia kufanya
kazi ya minada (auctions) na katika Taasisi nyingine za Serikali au Sekta
binafsi, kama vile ya Benki, Taasisi za fedha na kadhalika.
Chuo cha IJA kimekuwa kikiendesha mafunzo kama hayo tangu mwaka 2018 kwa mujibu wa Kanuni ya 4 na ya 6 za Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na.363 za mwaka 2017 ili kuwajengea uwezo watu wenye nia ya kufanya kazi hiyo na hivyo kuboresha mnyonyoro wa utoaji haki.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya 15 ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama yanayofanyika katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania) jijini Dar es Salaam.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo. Kushoto ni Mratibu wa Mafunzo ambaye pia ni Mhadhiri wa IJA, Bi. Fatuma Mgomba na kulia kwake ni Mhadhiri Msaidizi wa IJA, Bw. Roggers Cletus.
Washiriki wa mafunzo ya udalali na usambazaji wa nyaraka za Mahakama wakiwa katika mafunzo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Mwajuma Lukindo akiwasilisha mada katika mafunzo hayo.
Mhadhiri wa IJA, Bi. Fatuma Mgomba akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni