Ijumaa, 10 Oktoba 2025

KIKAO CHA MENEJIMENTI MKOA WA MBEYA CHAKETI

Na. Muksini Nakuvamba – Mhakama, Mbeya

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Said Kalunde amengoza kikao cha menejimenti mkoa wa Mbeya kilichofanyika jana tarehe 09 Oktoba 2025 katika ukumbi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya.

 Akiwasilishwa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2025/2026 Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambaye pia alikuwa Katibu katika kikao hicho Bi. Mervis Miti alitoa taarifa ya rasilimali watu ambapo ilieleza kuhusu hali ya watumishi wa Mahakama Mkoa wa Mbeya, upimaji wa watumishi na motisha za watumishi.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuhusu taarifa ya usimamizi wa rasilimali fedha, vyombo vya usafiri, taarifa ya mashauri, taarifa ya matumizi ya TEHAMA na ushughulikiaji wa malalamiko na mapendekezo, utoaji wa elimu kwa umma na hali ya majengo mbalimbali ya Mahakama mkoa wa Mbeya.

Vilevile, taarifa hiyo ilifafanua juu ya mafanikio kadhaa ikiwemo kupokea watumishi 18 wa ajira mpya, ukarabati na uboreshaji wa baadhi ya majengo ya Mahakama, kusimamia nidhamu ya watumishi, matengenezo ya magari ya ofisi na kupokea na kuanza kutumika kwa Majengo mapya matatu yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Kwa upande mwingine, taarifa hiyo ilieleza changamoto kadhaa ikiwemo uchakavu wa magari na majengo ya ofisi kama majengo ya Mahakama za mwanzo na nyumba ya kuishi Jaji Mfawidhi hali inayopelekea kupanga nyumba mtaani kwa gharama kubwa.

Changamoto zingine ni usajili wa mashauri kwa jina moja la wadaawa au washitakiwa kwa mashauri ambayo yana washitakiwa zaidi ya mmoja, sambamba na hilo pia kumekuwa na changamoto ya uwepo wa vielelezo vya muda mrefu katika mahakani, alisema Mtendaji huyo.

Taarifa hiyo pia ilifafanua juu ya mikakati kadhaa ya kuimarisha mifumo ya TEHAMA kwa kuhakikisha upatikanaji wa nishati na mtandao, kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo na kuendelea kulipa mirathi kwa wakati.

Aidha, iliwasilishwa taarifa ya mashauri kwa Mahakama zote za mkoa wa Mbeya na Mahakama Kuu, Kanda ya mbeya, taarifa hiyo iliwasilishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba.

“Baki ya mashauri hadi mwezi juni ni 639 na yaliyofunguliwa kuanzia julai hadi septemba ni 2481, yaliyomalizika kati ya julai hadi septemba ni 2501 na mashauri yaliyobaki hadi kufikia Septemba ni mashauri 619,” alisema Mhe. Mlimba.

Aidha, kikao kilijadili taarifa za Mirathi kwa Mahakama zote za Wilaya Mkoa wa Mbeya ambapo Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama zote waliwasilisha taarifa zao.

Mtendaji hiyo wa Mahakama aliwasilisha taarifa ya mirathi inayowataka kushirikiana katika kufanya tathimini ya fedha zote zilizopo kwenye akaunti ya mirathi kwa Mahakama zote na kuzilipa kwa haraka na kutuma taarifa ya utekelezaji wa jambo hilo kabla ya tarehe 05 novemba, 2025.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya ambaye ni mwenyekiti katika kikao hicho akifuatilia mawasilisho.


Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambaye pia alikuwa Katibu katika kikao hicho Bi. Mervis Miti akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kanda hiyo.

Sehemu ya wajumbe wa kikao

Hakimu mkazi mfawidhi mahakama ya wilaya Rungwe Mhe. Jackson Banobi (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya mirathi mahakama ya wilaya Rungwe

Afisa Hesabu Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Bi. Nancy Rwebembela (aliyesimama) Akichangia Hoja katika kikao hicho

Sehemu ya wajumbe wa kikao

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba (kulia) akiwasilisha taarifa ya mashauri na mirathi kwa Mahakama za Mkoa wa Mbeya.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni