Na YUSUFU AHMADI-IJA, Dar es Salaam
Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Italia (Sant’Anna School of Advanced Studies -Scuola)
kimeanza kutoa mafunzo ya siku tatu kwa Majaji, Mahakimu wa ngazi
mbalimbali na Waendesha Mashtaka wa Tanzania kuhusu ushirikiano wa kimataifa
katika kukabiliana na makosa ya jinai yanayovuka mipaka.
Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia yalifunguliwa tarehe 29 Septemba,
2025 na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Giuseppe Sean Coppola na
yanafanyika Mahakama Kuu – Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke mkoani Dar es Salaam. Wawezeshaji wa mafunzo
hayo ni Majaji kutoka Tanzania pamoja na Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha
Italia.
Lengo la mafunzo hayo ni
kuimarisha uelewa na uwezo wa Maofisa hao katika kushughulikia makosa hayo ya
jinai hususani maeneo ya ushirikiano wa kimahakama juu ya urejeshaji wa watuhumiwa na kusaidiana kisheria kati ya nchi
mbalimbali.
Katika neno lake la utangulizi, Jaji
Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa amebainisha kuwa
umuhimu wa mafunzo hayo ni kuimarisha mifumo ya ushirikiano wa kimataifa katika
kushughulikia upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya uharifu yanayovuka mipaka.
“Mafunzo haya yatawapatia washiriki kuhusu
namna nchi na vyombo vyao, zinaweza kushirikiana katika kushughulikia uhalifu
wa kuvuka mipaka unaoharibu amani ya dunia, usalama, uchumi na maendeleo ya
jamii,” amesema.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi
Coppola alisema kuwa kupitia mafunzo hayo washiriki wa Tanzania na Italia
watatoka na uelewa wa pamoja katika kushughulia uhalifu huo, akibainisha kuwa
nchi yake ni miongoni wa waathirika wakubwa.
“Mtandao wa uhalifu unaouvuka mipaka ni
tatizo kubwa duniani na umekuwa na athari kubwa kwa jamii, hivyo tunahitaji
kuimarisha ushirikiano kati ya Majaji, Mahakimu na Waendesha Mashtaka wa
Tanzania na Italia, ili tuwe na uelewa mmoja wa jinsi ya kukabiliana na mtandao
huo,” amesema Balozi Coppola.
Pia ameishukuru Serikali ya Tanzania na
Uongozi wa IJA kwa kushirikiana pamoja katika kufanikisha mafunzo hayo.
Ufunguzi huo umehudhuriwa pia na Mkurugenzi
wa Mradi wa Utawala wa Sheria na Ushirikiano wa Mahakama ambaye pia ni Profesa Msaizidi wa Scuola Lorenzo Gasbarri
pamoja na viongozi wengine.
Changamoto
za uhalifu wa kuvuka mipaka
Kwa
mujibu wa takwimu, makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu, dawa za kulevya,
utakatishaji wa fedha, ugaidi, biashara haramu ya silaha na ujangili, na
uhalifu mitandaoni yameongeza kutokana na maendeleo ya teknolojia na uhuru wa
watu kuvuka mipaka..
Hivyo kupitia mafunzo
hayo na ukubwa wa changamoto hiyo, IJA pamoja na Scuola ambacho ni miongoni mwa
Vyuo Vikuu vya Umma vyenye kuheshimika nchini Italia, vinakuwa sehemu ya kuunga
mkono sera na mikakati ya Serikali na Jumuiya za Kimataifa katika mapambaop
dhidi ya uhalifu wa kimataifa kwa kuimarisha mifumo ya haki jinai.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni