Jumatano, 1 Oktoba 2025

UTOAJI HAKI MADAI UENDANE NA MKAKATI WA MAHAKAMA NA DIRA YA NCHI; JAJI RWIZILE

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile ametoa rai kwa Wadau wa Haki Madai kuboresha huduma za haki madai kwa kuzingatia Dira ya Nchi pamoja na Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2024/2025 na 2025/2026.

Akiongoza kikao cha Wadau wa Kusukuma Mashauri ya Haki Madai kilichofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Rwizile alisema utamaduni wa kufanya vikao hivyo husaidia pia kuharakisha kutoa haki, kudumisha amani na kuchochea maendeleo yanayoinua uchumi wa wananchi katika kutunza muda wao Mahakamani.

Jaji Rwizile alisema, "vikao hivi vitumike kusaidia kufanya kazi kwa weledi, ushirikiano na kubadilishana uzoefu wa kazi."

Jaji Mfawidhi huyo aliwataka wadau hao kushirikiana na kuongeza weledi katika matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), akiwataka nao kuanzisha mifumo yao itakayosomana na ya Mahakama ili kuendelea  kurahisisha muda wa utendaji kazi za utoaji haki mahakamani.

Aidha, aliwasisitiza juu ya matumizi ya tehama yaendelee kuimailishwa katika ofisi zao kwani kila mdau ataendesha Mahakama akiwa katika ofisi yake bila kuja Mahakamani, hii yote nikuhakikisha tunaokoa muda wa wadau wetu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea, Bw. Eliutha Kivyiro aliihakikishia Mahakama kuwa jukwaa hilo limejipanga kuhakikisha linakwenda kwa kasi ya Mahakama katika maswala yote ya utoaji haki.

Bw. Kivyiro aliwajulisha wadau wa haki madai kuwa, Mawakili wameendelea kujiimarisha katika matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), hii ikiwa ni moja ya kupanga mashauri kwa muda mfupi na kuhakikisha wananchi wanaohitaji uwakilishi wa Wakili mahakamani wanapata huduma hiyo kwa haraka na kuzingatia muda.

Vilevile, Dalali wa Mahakama Bw. Robert Lusenga, aliwajulisha wadau hao kuwa amekuwa akifanya kazi za Mahakama bila ya changamoto kubwa ambazo kutokana na uboreshaji wa huduma za Mahakama umepunguza changamoto, hivyo kazi ya udalali wa Mahakama inatendeka bila vikwazo kama ilivyokuwa awali.

Wajumbe walioshiriki kikao hicho ni kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa Kigoma, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Jukwaa la Mawakili wa kujitegemea Tanganyika (TLS), Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kigoma na Madalali wa Mahakama.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akisisitiza jambo hivi karibuni wakati wa kikao cha Wadau wa Kusukuma Mashauri ya Haki Madai kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.


Sehemu ya wajumbe wa Kikao cha Wadau wa Haki Madai wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (aliyeketi mbele).

Kaimu Mfawidhi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Frank Makigijo, akitoa ufafanuzi juu wa mashauri yaliyopo katika ofisi hiyo na nini mkakati wa kuisaidia Mahakama kumaliza mashauri hayo.


Dalali wa Mahakama, Bw. Robert Lusenga, akitoa mwelekeo wa shughuli za dalali katika kuisaidia Mahakama kuharakisha huduma za haki kwa wananchi.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni