Jumatano, 26 Novemba 2025

MAHAKAMA YAPUNGUZA MASHAURI YA MLUNDIKANO HADI ASILIMIA 4.5; MSAJILI MKUU

 ·       Asema hakuna Hukumu inayozidi Siku 90

Na HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mheshimiwa Eva Kiaki Nkya, leo amesema Mahakama imefanikiwa kupunguza mashauri sugu hadi kufikia asilimia 4.5 yakilinganishwa na asilimia 21 miaka mitano iliyopita.

Mhe. Nkya aliyasema hayo jana tarehe 25 Novemba, 2025 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya huduma za kimahakama wakati wa ziara ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera aliyetembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma akiwa pamoja na Naibu Waziri, Mhe. Zainab Katimba.

Akitoa taarifa hiyo, Msajili Mkuu alisema kuwa Mahakama imeendelea kutekeleza mageuzi makubwa yenye lengo la kuharakisha upatikanaji wa haki na kupunguza mlundikano wa mashauri nchini.

Kwa mujibu wa takwimu alizotoa, hadi kufikia mwisho wa mwezi Oktoba mwaka huu, jumla ya mashauri 298,400 yalifunguliwa katika ngazi mbalimbali za Mahakama na kati ya hayo 212,000 yamesikilizwa na kukamilika, sawa na asilimia 71.1. Mashauri yanayoendelea ni 41,000, huku mashauri sugu (backlog) yakiwa 1,951 pekee, sawa na asilimia 4.5, yakilinganishwa na asilimia 21 miaka mitano iliyopita.

Msajili Mkuu alisema kuwa tangu kuanza kwa mwaka huu 2025 hakuna hukumu yoyote katika Mahakama zote nchini iliyozidi siku 90, kama inavyoelekezwa na sheria, jambo linaloonesha ufanisi katika utoaji wa haki.

Akifafanua zaidi, alisema Mahakama imepunguza muda wa wastani wa usikilizaji wa mashauri kutoka siku 554 kwa mwaka 2015 hadi siku 67 kwa sasa.

Aidha, alieleza kuwa, mashauri ya jinai ni asilimia 57 na mashauri ya madai ni asilimia 43, huku Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani zikiendelea na vikao maalum vya kumaliza mashauri ya kiuchumi, kodi na biashara.

Kwa upande wa mashauri katika Mahakama za Chini, Msajili Mkuu alisema kuwa, mashauri yote yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba mwaka huu, isipokuwa yale ambayo siyo chini ya mamlaka ya Mahakama hizo na kwamba lengo la kumaliza mashauri yote sugu nchini ni Juni 2026.

Katika eneo la huduma kwa wateja, alieleza kuwa Mahakama imeimarisha mifumo ya upatikanaji wa taarifa na malalamiko kwa kutumia ‘Chatbot ya WhatsApp 0754 500 400’, uwepo wa madawati ya huduma kwa mteja katika kila Mahakama, tovuti ya Mahakama na Kituo cha huduma kwa wateja. Kwa mwaka huu maoni 2,445 yamepokelewa, ambapo 1,977 yameshughulikiwa.

Msajili Mkuu alihitimisha kwa kusema kuwa Mahakama itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mikakati ya maboresho iliyojiwekea ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora, za viwango na mapema ipasavyo.

“Lengo letu ni kuwa Mahakama yenye ufanisi, uwazi na inayomlinda mwananchi. Tutaendelea kusimamia kila hatua hadi pale mashauri yote sugu yatakapomalizika ifikapo Juni 2026,” alisisitiza Mhe. Nkya.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mheshimiwa Eva Kiaki Nkya akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya huduma za kimahakama wakati wa ziara ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera alipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma jana tarehe 25 Novemba, 2025 akiwa pamoja na Naibu Waziri, Mhe. Zainab Katimba (hawapo katika picha).

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (katikati) akifurahia jambo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) wakati wa mazungumzo na watumishi wa Mahakama ya Tanzania yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma jana tarehe 25 Novemba, 2025.



Sehemu ya Watumishi wa Mahakama na Tume ya Utumishi wa Mahakama wakifuatilia kinachojiri katika Mkutano baina yao na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera alipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma jana tarehe 25 Novemba, 2025.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)









 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni