Jumatano, 26 Novemba 2025

WAZIRI KATIBA NA SHERIA ATEMBELEA MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA YA TANZANIA

·       Afanya mazungumzo na Jaji Mkuu, Menejimenti, Watumishi wa Makao Makuu ya Mahakama na Tume ya Utumishi wa Mahakama

·       Jaji Mkuu awapongeza Waziri na Naibu wake, ashukuru kwa ushirikiano unaotolewa na Wizara

·       Waziri Homera naye apongeza maboresho ya Mahakama ikiwemo matumizi ya TEHAMA, huduma za Mahakama Zinazotembea

·       Aahidi kuwa Balozi wa Mahakama kwa kuhubiri yote mazuri yanayofanywa na Mhimili huo

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera jana tarehe 25 Novemba, 2025 alikutana na kufanya mazungumzo na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Menejimenti na Watumishi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na kuahidi kushirikiana na Mahakama katika utekelezaji wa utoaji huduma kwa wananchi, sambamba na kuwa balozi wa kuhubiri mazuri yanayofanywa na Mhimili huo.

Mhe. Dkt. Homera aliwasili katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainabu Athuman Katimba, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Franklin Jasson Rwezimula na baadhi ya Watumishi wengine wa Wizara hiyo ambao walipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama.

Akizungumza wakati wa kikao kifupi kilichowahusisha Jaji Mkuu, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu na Viongozi wengine wa Mahakama, Mhe. Masaju alimpongeza Mhe. Dkt. Homera na Naibu wake kwa uteuzi waliopata kushika Wizara hiyo muhimu kwa Taifa na kuwahakikishia ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa majukumu kati ya Wizara na Mahakama ya Tanzania.

“Sisi tunawashukuru Wizara ikiwa tu ndio mmeteuliwa kuwa Viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria, moja ya Wizara nyeti sana katika Taifa hili, mkaona mje mtutembelee, mjue nasi tulipo na majukumu yetu na namna tunavyoyatekeleza, mipango yetu tuliyonayo ya kutekeleza hili jukumu kuu la kutoa haki kwa wananchi wa Tanzania linavyoendelea, mafanikio ni wapi tumefanya vizuri, changamoto ni zipi, mikakati ipi tunayo kwenda mbele, mmechagua Taasisi muhimu sana kwa kuanzia utekelezaji wa majukumu ya Wizara,” alisema Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu alieleza kuwa, Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inaanzisha Mhimili wa Mahakama na Mihimili yote ya Serikali lakini ikiwa na jukumu la kutoa haki, “Lakini Ibara ya 107A inasema Mahakama ya Tanzania ndio itakuwa mamlaka yenye kauli ya mwisho kwenye masuala ya utoaji haki. Na ‘vision’ yetu ni Haki sawa kwa wote, mapema ipasavyo, na kwa sababu hiyo na sisi sasa hata mikakati yetu tuliyo nayo ni ya kuhakikisha kwamba hii Dira yetu inatekelezeka,” alisisitiza.

Jaji Mkuu alitumia fursa hiyo kumshukuru Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu ushirikiano wa dhati ambao Mahakama inapata kutoka Wizara hiyo.

“Mpaka sasa tunawashukuru sana Wizara kwa ushirikiano mkubwa mnaotupatia kwakweli mmekuwa wa msaada mkubwa kwetu, itoshe tu kusema kwamba tuna ushirikiano mzuri na Watangulizi wenu tulikuwa na ushirikiano mzuri na tunafanya kazi kwa karibu, kwa hiyo mkiwa na jambo lolote ambalo mnaona mnahitaji msaada wetu msisite kuwasiliana nasi,"alisema Mhe. Masaju.

Vilevile alieleza kuhusu Dira ya Mahakama ya Tanzania ya ‘Haki sawa kwa wote, mapema ipasavyo’ ambapo amesema kuwa jitihada/maboresho yote yanayofanywa na Mahakama ni kuhakikisha kuwa Dira inafikiwa.

Mhe. Masaju alisema kwamba, katika jitihada za kuhakikisha kuwa Mahakama inaendelea kutoa haki kwa wananchi mapema ipasavyo, tayari wameshaandaa Muswada wa mabadiliko ya mifumo ya Mahakama ambapo pamoja na mambo mengine Mahakama inakusudia kubadilisha Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufani (The Appellate Jurisdiction Act) ili kuondoa urasimu lakini pia kuimarisha ufanisi wa utekelezaji wa majukumu.

“Sambamba na sheria hiyo tunafanya pia, tunapendekeza kufanya mabadiliko kwenye Sheria ya Mahakama za Mahakimu (The Magistrates Court Act) ili inayoitwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, tunataka kuibadilisha sasa iitwe Mahakama ya Mkoa ifanye mashauri yake yenyewe kwa kuanzia (Original jurisdiction), Mahakama hiyo pia itakuwa inasikiliza rufaa kutoka Mahakama za Wilaya, lakini lengo letu ni kuimarisha upatikanaji wa haki na kusogeza huduma hizi kwa wananchi,” alieleza Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Masaju alisema kwamba, Mahakama ya Tanzania ina miradi mingi na inaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya majengo ya Mahakama ili kusogeza huduma ya utoaji haki karibu zaidi ya wananchi na kuongeza ufanisi, ametaja miradi inayoendelea kujengwa ni pamoja na ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) katika Mikoa ya Singida, Simiyu, Songwe, Njombe, Lindi, Geita, Pemba, Katavi na nyingine.

“Lakini pia kuna majengo ya Mahakama za Wilaya yanaendelea kujengwa, lakini tunayo Sera hapa kwamba kila Kata inapaswa kuwa na Mahakama za Mwanzo, tulichokifanya sisi tumewaandikia TAMISEMI kuomba ardhi kila Kata tupewe ardhi isiyopungua hekari mbili kwa ajili ya kujenga Mahakama na hiyo ardhi sio lazima iwe Makao Makuu ya Serikali ya Kata, kwahiyo tuwaombe Waheshimiwa mtakapokuwa karibu na watu wa TAMISEMI muwahimize hilo sisi tunamaanisha hilo kwa Mahakama hizo pia zitasaidia katika eneo la kuimarisha utawala bora,” alisisitiza Jaji Mkuu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju alimuomba Mhe. Dkt. Homera kuendelea kuisemea Mahakama ili kuendelea kuboresha maslahi ya Majaji na watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla.

Kadhalika, Jaji Mkuu alimueleza Waziri huyo na ujumbe alioambatana nao kuwa, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika jukumu la utoaji haki kwa wananchi, ambapo alibainisha kuwa, Mahakama ina uwezo wa kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao na inaendelea kujiboresha zaidi katika eneo hilo kwa kujifunza kutoka katika Nchi nyingine ikiwemo Korea Kusini, Singapore, China na kadhalika.

Kadhalika, Jaji Mkuu alimueleza Waziri Homera kuwa, kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mengi ya ardhi ambayo mengine yanatoka kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na mamlaka nyingine ambapo amesema kwamba Mahakama ipo tayari kuchukua jukumu la kusikiliza mashauri ya ardhi ya nchi nzima ili kuondokana na changamoto zinazojitokeza kuhusu masuala ya ardhi ambayo ni mali muhimu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Masaju alisema kwamba katika kuendelea kuboresha huduma za utoaji haki, kwa sasa hakuna Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo kwa kuwa wanapatiwa dhamana hatua ambayo imewezesha kupunguza idadi ya mahabusu gerezani, kupungua kwa mashauri ya jinai hata katika katika Mahakama hizo hata katika Mahakama za Wilaya.

Jaji Mkuu aliongeza kuwa, kufuatia maelekezo aliyotoa wakati alipofanya ziara katika Gereza la Isanga jijini Dodoma tarehe 10 Julai, 2025 kuhusu Mahakama za Mwanzo kutopeleka Mahabusu Gerezani amesema limesaidia kwa kiasi kikubwa na sasa hakuna Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo kutokana na maelekezo hayo.

Kadhalika, Mhe. Masaju alisema kwa sasa kuna maandalizi ya kuandika hukumu kwa Lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Homera amekiri kufurahishwa kwa mapokezi mazuri waliyopata yeye pamoja na ujumbe alioambatana nao na kusema kuwa, Wizara ipo tayari kushirikiana na Mahakama katika utekelezaji wa majukumu.

“Sisi kama Wizara, tupo tayari kufanya kazi, ni muhimu mambo yanayofanywa na Mahakama yatangazwe ni muhimu Watanzania wakajua kinachofanyika kwa kila Taasisi,” amesema Mhe. Waziri huyo.

Aidha, Mhe. Dkt. Homera amesema kuwa, Wizara iko tayari kufanyia kazi maombi ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ambayo Mahakama inapendekeza na kuiomba Mahakama kuwasilisha nyaraka zote muhimu zinazohitajika ili taratibu stahiki zifanyike pamoja na kuahidi kufanyia kazi suala ya kuwasiliana na TAMISEMI kuhusu suala ya kutenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.

“Mimi siamini kwenye kuchelewa, naamini kwenye kuwahi na matokeo,” amesema Waziri huyo ambaye ameomba pia kufanyika kwa vikao hivyo mara kwa mara ili kuweza kupata taarifa mbalimbali za maendeleo/uboreshaji huduma za Mahakama.

Kwa upande mwingine, Mhe. Dkt. Homera akizungumza na watumishi wa Makao Makuu ya Mahakama mara baada ya kupokea Mawasilisho kutoka kwa Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama, amewapongeza watumishi wa Mahakama kwa kazi nzuri akiahidi kutoa ushirikiano ili Mahakama iendelee kufanya kazi kwa ufanisi.

Amepongeza pia Mahakama kwa usimamizi thabiti wa Miradi ya Ujenzi wa Mahakama ambapo amesema si jambo jepesi kusimamia mradi na kukamilika.

Aidha, Waziri huyo ameshauri kuwa Vitabu vya Mashauri ya mauaji viandaliwe mapema na kwa uharaka kama ambavyo nakala za hukumu zinavyopatikana kwa haraka.

Waziri huyo pamoja na alioambatana nao wamepata fursa ya kutembelea Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Virtual Situation Room), Ofisi ya Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama (Call Centre) pamoja na Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama.

 Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (kulia) alipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma jana tarehe 25 Novemba, 2025 kwa lengo la kusalimia na kupata uelewa juu ya utendaji kazi wa Mahakama nchini. Wanaoshuhudia katikati ni Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

 Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera alipowasili ofisini kwa Jaji Mkuu jana tarehe 25 Novemba, 2025. Kulia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba.


 Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (katikati) akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika kikao na ujumbe kutoka Waziri wa Katiba na Sheria, Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Watumishi wengine wa Mahakama. Kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Kiongozi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija na kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Washiriki wengine waliohudhuria kikao kati ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera alipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma jana tarehe 25 Novemba, 2025.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera alipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (kushoto) na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba (kulia).
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (kushoto) pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (kulia).
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel (wa kwanza kulia), Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (wa pili kushoto), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba (wa pili kulia) na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Franklin Jasson Rwezimula.


Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (wa pili kushoto),  Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba (wa pili kulia), Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (wa kwanza kushoto).

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akimkabidhi nyaraka muhimu za Mahakama ikiwemo Jarida la Mahakama (HAKI Bulletin) kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera.


Picha mbalimbali za sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama, Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiwa katika kikao na Ujumbe kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ulioongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Katimba (hayupo katika picha) walipotembelea Makao Makuu ya Tanzania jijini Dodoma jana tarehe 25 Novemba, 2025.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa wasilisho kuhusu Mahakama kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (hayupo katika picha) alipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania tarehe 25 Novemba, 2025.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akitoa wasilisho kuhusu Mahakama kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (hayupo katika picha) alipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania tarehe 25 Novemba, 2025.


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera na ujumbe alioongozana nao akipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyenyoosha mkono) akiwaongoza Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera na wengine kuelekea ofisini kwa Jaji Mkuu walipowasili Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma tarehe 25 Novemba, 2025.


Ujumbe kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ukiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera wakipata maelezo kuhusu utendaji kazi wa Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Virtual Situation Room) walipotembelea katika chumba hicho.
 

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock akielezea kuhusu utendaji kazi wa Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Virtual Situation Room).

Ujumbe kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ukiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera wakipata maelezo kuhusu utendaji kazi wa Ofisi za Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama (Call Centre) kutoka kwa Hakimu Mkazi Mkuu ambaye ni Mtaalam Mchakata Taarifa wa Kituo hicho, Mhe. Domician Denice Mlashani (wa kwanza kulia).


Ujumbe kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ukiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera wakielekea kutembelea Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama zilizopo mkabala na Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni