Jumanne, 25 Novemba 2025

MTENDAJI MKUU AIOMBA WIZARA KUSAIDIA UPATIKANAJI VIWANJA VYA KUJENGA MAHAKAMA ZA MWANZO

Na INNOCENT KANSHA - Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria kusaidia upatikanaji wa viwanja vya kujenga Mahakama za Mwanzo nchini, hasa kwa maeneo yenye uhitaji kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyagiza wakati akizindua Jengo la Makao Makuu ya Mahakama.

Prof. Ole Gabriel ameyasema hayo leo tarehe 25 Novemba, 2025 alipokuwa akifanya wasilisho fupi la taarifa ya utendaji kazi mbele ya ujumbe uliongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homela ambaye alifanya ziara ya kutembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, kujitambulisha na kukutana na watumishi wa Mahakama.

Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa, mafanikiwa na maboresho ya Mahakama yanatokana na juhudi za wadau wote hiyo ndiyo siri ya mafanikio na Mahakama itaendelea kushirikiana na wadau wote hususani mihimili mingine yote ya dola bila kuathili majukumu mengine ya kikatiba na kuhakikisha uhuru wa Mahakama unakuwepo na unalindwa kwa wivu mkubwa.

Mtendaji Mkuu akaongelea pia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wa kuwekeza kwenye ujenzi wa jengo la kisasa lenye thamani ya shilingi bilioni 127.9 za kitanzania, lenye ukubwa wa mita za mraba elfu 63 na la sita kwa ukubwa duniani na la kwanza Afrika kwa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama.

Vilevile, Prof. Ole Gabriel amemweleza Waziri kuwa Serikali, kupita fedha za ndani imejenga makazi ya Majaji kwa gharama ya bilioni 42.3 katika eneo la Iyumbu, karibu na Chuo Kikuu Dodoma. Jumla ya nyumba 48 za makazi ya kisasa zimejengwa na kila block ina nyumba 24.

Kadhalika, Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa kuna ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tisa ambao unaendelea na gharama yake ni bilioni 76 ambazo ni fedha za awamu ya pili ya mkopo wa Banki ya Dunia. Awamu ya kwanza Mahakama ilipata dola za kimarekani milioni 65 na awamu ya pili milioni 90 na kazi inaendelea katika maeneo mbalimbali nchini katika hatua tofauti tofauti kwenye Mikoa ya Lindi, Songea kwa asilimia 77, Njombe, Songwe, Katavi kwa asilimia 85, Singida, Geita kwa asilimia 94, Simiyu kwa asilimia 95 na Pemba ikiwa ni sehemu ya kudumisha Muungano.

Aidha, kuna Mahakama za Mwanzo zinaendelea kujengwa maeneo mbalimbali nchini kama vile Nanjilinji kule Lindi na ni kati ya maeneo magumu kijiografia lakini Mahakama imepeleka huduma kwa sababu kuna wananchi wapaswa kupata huduma za haki kama sehemu zingine nchini.

Mtendaji Mkuu akaelezea jambo lingine lililoipa Mahakama heshima kubwa ni matumizi ya TEHAMA kwani Mahakama ndiyo Taasisi ya kwanza ya Serikali inayofanya vizuri sana katika matumizi hayo mifumo mingi imejengwa na wataalam wa ndani kupitia kurugenzi yake yenyewa ambayo ni mahili sana ina wataalamu wabobezi.

“Kwani wataalum hao hufungiwa eneo maalumu lenye utulivu mkubwa kupewa maslahi bora ili kujenga mifumo mbalimbali inayotumika mahakamani kusaidia uendeshaji wa shughuli za mahakamani za utoaji haki kwa wananchi,” amesema Ole Gabriel.

Mtendaji Mkuu ametumia nafasi hiyo kuiomba Wizara pia kusaidia kutangaza Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, ambacho kilichoazishwa mwaka 2022 na kinatoa huduma ndani ya masaa 24 kila siku. Amesema kuwa Kituo hicho kina watumishi 10 wanaotoa huduma muda wote na kwa humahiri mkubwa, hivyo kuna kila sababu ya kukitangaza.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alipokuwa akifanya wasilisho fupi la taarifa ya utendaji kazi mbele ya ujumbe uliongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homela alipofanya ziara ya Kujitabulisha Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

Sehemu ya watumishi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania walidhuria kwenye kikao cha kujitambulisha Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homela

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homela (wa pili kulia) alipofanya ziara ya kukagua kituo cha huduma kwa mteja cha Mahakama ya Tanzania

Mtaalum kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania Mhe. Denice Mlashani (wa kwanza kulia)  akitoa maelezo ya namna kituo hicho kinavyofanya kazi

Mkurugenzi wa TEHAMA Mahakama ya Tanzania Bw. Kalege Enock akitoa maelezo ya namna kituo hicho cha situation Room kinavyofanya kazi katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelezo ya uanzishwaji wa situation Room katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homela akifafanua jambo wakati wa ziara hiyo.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homela akifafanua jambo wakati wa ziara hiyo.




 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni