Jumanne, 25 Novemba 2025

MHE. TARIMO AWAKUMBUSHA MAHAKIMU KIGOMA KUVUKA MWAKA BILA MASHAURI YA MLUNDIKANO

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Varelian Tarimo amewataka Mahakimu Wakazi kusikiliza mashauri mengi ili kuvuka mwaka bila  mashauri ya mlundikano.

Mhe. Tarimo alieleza hayo hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kikazi aliyofanya kwa siku tano ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya ili kuangalia maeneo mbalimbali, ikiwemo usikilizaji wa mashauri na utunzaji wa miundombinu pamoja na  mazingira.

Hongereni kwa kazi nzuri ya kusikiliza mashauri, ni rai yangu kuhakikisha mikakati yetu ijikite katika kuhakikisha mashauri yenye umri mkubwa yanamalizika ndani ya muda tuliojipangia ili kuepuka mashauri ya mlundikano,” alisema Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo katika moja ya Mahakama sita alizokagua.

Mhe. Tarimo aliendelea kusisitiza kuwa, Mahakama za Mwanzo takwimu zao zinakwenda vizuri, hivyo nao wanatarajia kuona wanavuka mwaka wakiwa na twakwimu nzuri za kumaliza mashauri wakizingatia Mpango Mkakati wa Mahakama wa Kutoa Haki kwa Wote, mapema ipasavyo.

Hata hivyo, aliwakumbusha Viongozi na Watumishi wa Mahakama zote sita kushirikiana na Wadau wa Mahakama katika shughuli za utoaji haki ili kurahisisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama.

Aidha, Mhe. Tarimo aliwataka watumishi kuendelea kutunza mazingira ya Mahakama zao kwa kupanda miti ya matunda na kuboresha miundombinu ya majengo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)  ili  kuimarisha mazingira ya kazi kuendelea kuwa  na hatimaye kupunguza muda wa kusikiliza mashauri na utoaji haki mapema ipasavyo.

Kadhalika, Mfawidhi huyo alizipongeza Magereza kwa uboreshaji wa mazingira ya vyoo vya kisasa kwa Wafungwa na Mahabusu wanaopelekwa katika Magereza za Wilaya Kibondo na Kasulu huku akiwataka kuendelea kuboresha zaidi eneo la chakula kwa wafungwa hao. 

Mahakama zilizokaguliwa ni Mahakama za Wilaya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Uvinza, Buhigwe na Kakonko pamoja na Magereza za Wilaya Kasulu na Kibondo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Varelian Tarimo akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu alipofanya ziara hivi karibuni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Varelian Tarimo (aliyeketi) akipokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Mhe. Maira Makonya.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Varelian Tarimo (kushoto) akiwa pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Mhe. Imani Batenzi (kulia) alipokuwa akikagua mazingira ya Mahakama hiyo wakati wa ziara yake aliyofanya hivi karibuni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma Mhe. Aristida Varelian Tarimo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mrakibu Mwandamizi wa Magereza. SSP- Peter Shabani (kushoto). Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Mhe. Maira Makonya mara baada ya ukaguzi wa Magereza ya Wilaya Kibondo, Nyamisivyi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Varelian Tarimo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kakonko, Mhe. Ambikile Kyamba (kushoto) na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kakonko, Mhe. Magreth Rweyemamu. Waliosimama ni sehemu ya watumishi wa Mahakama hiyo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma Mhe. Aristida Varelian Tarimo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Mahakimu na Watumishi. Wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Venance Mwakitalu, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Manyovu Mhe. Straton Mosha (wakwanza kulia) ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Buhigwe Mhe. Erick Sabaya Mollel na wa kwanza kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Bi. Mariamu Lukindo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni