Jumatatu, 22 Desemba 2025

TIMIZENI WAJIBU WENU IPASAVYO, NINYI NDIO INJINI YA MAHAKAMA-JAJI MKUU

  • Awataka Wasajili & Naibu Wasajili wa Mahakama kufanya kazi kwa kujituma bila maelekezo ya Viongozi
  • Atoa rai kwa Majaji/Mahakimu kuyapa kipaumbele mashauri ya mirathi, ardhi……
  • Awakumbusha Wasajili hao kuwa waadilifu hata baada ya kuteuliwa kuwa Majaji 
  • Asema ili kuendelea kuhudumia wananchi, Mahakama imeamua kufanya ugatuzi wa madaraka ya Mahakama ya Rufani kwenye Kanda

Na MARY GWERA & HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Wasajili na Naibu Wasajili wa Mahakama nchini kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwa wao ndio injini ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama.

Akizungumza wakati wa kikao kati yake na Wasajili na Naibu Wasajili wa Mahakama kilichofanyika leo tarehe 22 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu jijini Dodoma na kwa njia ya Mkutano Mtandao (Video Conference), Mhe. Masaju amesema kuwa, ni muhimu kwa Wasajili hao kujituma na kuwa wabunifu badala ya kutekeleza majukumu kwa kutegemea maelekezo ya Viongozi pekee.

“Ninyi ndio injini ya shughuli za Mahakama, ndio mashine za utendaji wa shughuli za Mahakama, tunataka hata tunapofanya ugatuzi wa madaraka ya Mahakama ya Rufani kwenye Kanda tuendeleze jitihada za kuhakikisha haki inatolewa mapema ipasavyo,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Masaju  amewataka Wasajili wa Mahakama nchini kuimarisha utendaji kazi, kuzingatia maadili ya kazi na kusimamia kikamilifu mashauri ili kuhakikisha haki inatolewa mapema ipasavyo na kwa mujibu wa sheria, licha ya kuwepo kwa changamoto katika uendeshaji wa mashauri, hususani ucheleweshaji wa mashauri unaosababisha wananchi kunyimwa haki zao za msingi.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, rufaa zisizo na msingi ni miongoni mwa sababu zinazochangia msongamano wa mashauri mahakamani, huku akiwataka Wasajili kutumia mamlaka yao kikamilifu katika kusimamia hatua za awali za mashauri.

Sambamba na hayo, amewaelekeza kuyapa kipaumbele mashauri ya mirathi pamoja na mashauri ya ardhi na mashauri yote kwa ujumla ili yakamilike mapema na shughuli nyingine za maisha ziweze kuendelea.

“Tuyape kipaumbele mashauri ya mirathi, hayana sababu ya kukaa kwa muda mrefu, tusishabikie vitu vinavyoweza kuweka majonzi kwenye familia, hivyo tuyamalize mashauri hayo mapema ipasavyo,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amesema kuwa, yeye hatampima Jaji au Hakimu kulingana na idadi/viwango vya uondoshaji wa mashauri vilivyowekwa, bali anavutiwa zaidi na ufanisi katika kazi.

"Ninatambua tulikuwa na sababu za msingi kwa nini tuliweka kanuni ya 'backlog', kwamba kesi itachukuliwa kwamba hii imechelewa kusikilizwa kama kwa mfano Mahakama ya Rufaa itakuwa tangu miaka miwili haijaikilizwa, Mahakama Kuu miaka miwili, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya mwaka mmoja, Mahakama ya Mwanzo miezi sita, huo ulikuwa utaratibu mzuri uliokusudia kushughulika na hii changamoto tuliyokuwa nayo ya wingi wa mashauri wakati ambapo tulikuwa na miundombinu ya Mahakama, unakuta Mahakama moja ya Wilaya inahudumia na Wilaya nyingine mbili, Mahakimu hawapo, rasilimali fedha hakuna lakini sasa tumetoka huko Mahakimuw apo hizo rtasilimali za kusikiliza mashauri zipo," ameeleza.

Ameongeza kwamba,  Mahakama zipo kwa hiyo haiwezi kuendeleza utaratibu huo, huku akihoji kwanini mashauri ya Mahakama za Mwanzo yachelewe? Na kwamba kwa upande wa Mahakama za Wilaya kuna mwongozo wa mashauri ya jinai tangu mwaka 2020 kwamba, shauri linapopokelewa mahakamani linaanza kusikilizwa siku hiyohiyo, watu wakikamatwa na Polisi mwongozo uliopo ni kwamba wanatakiwa kwenda na mashahidi, kila mmoja anaenda na mashahidi wake, hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha shauri kwa kigezo cha kusubiri miezi sita na muda uliowekwa na ngazi nyingine za Mahakama.

"Sasa kama ni hivi, hizi Mahakama za Mwanzo kwa nini tuchelewe, kwa nini kesi za jinai zichelewe mpaka miezi sita, hiyo miezi sita kesi haijaisha tu kuna baadhi ambao hata hawana mashahidi wengi, kwa hiyo ni uzembe, tunatakiwa kuwahudumia wananchi wa Tanzania katika ukweli na haki," amesisitiza Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Masaju amewakumbusha Wasajili kusimamia nidhamu ya kazi kwa watumishi wa Mahakama, akisisitiza kuwa vitendo vya uzembe, kutowajibika na ukiukwaji wa maadili haviwezi kuvumiliwa kwa kuwa vinadhoofisha taswira ya Mahakama kwa jamii.

“Sisi kama Viongozi tuna wajibu wa kushirikiana pamoja na watumishi wote wa Mahakama kubuni mikakati na kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuzitatua na kusonga mbele,” amesema Jaji Mkuu.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amewataka Wasajili kujishughulisha na shughuli halali katika kujipatia kipato, huku akisisitiza kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi halali afanye kazi huku akitimiza wajibu wake, akirejea Ibara ya 9 (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) ambayo inasema ‘kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu riziki yake.’

Akizungumzia kuhusu changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiikabili Mahakama, ambazo ni pamoja na changamoto ya miundombinu ya majengo, changamoto ya rasilimali watu na rasilimali fedha na changamoto za kimaadili, Jaji Mkuu amesema kwamba, Serikali imechukua hatua madhubuti katika kutatua changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa Mahakama katika Mikoa na Wilaya ambazo hazikuwa na Mahakama.

Ameongeza kuwa, kuna ya ujenzi wa Majengo mapya ya Mahakama Kuu- Masjala mpya za Simiyu, Katavi, Lindi, Njombe, Singida, Songwe na kwamba Masjala hizo zinatarajia kuanza kazi tarehe 02 Februari, 2026 huku ujenzi wa ukiendelea katika Mikoa ya Songea na Geita na inatarajiwa kukamilika tarehe 01 Februari 2026.

“Serikali imechukua hatua madhubuti kutatutua tatizo la miundombinu ya Mahakama, wakati huu katika Mahakama ya Tanzania hasa Tanzania bara Mahakama za wilaya ziko katika kila wilaya isipokuwa wilaya tatu ya Chamwino mkoani Dodoma, Ikungi na Mkalama za Mkoani Singida na Serikali iko katika mpango wa kujenga Mahakama katika kila Kata,” Amesema Mhe. Masaju.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewaeleza Wasajili hao kuhusu Sera ya Mahakama ya kuwa na Mahakama ya Mwanzo kila Kata maana yake zitajenga Mahakama za Mwanzo, ambapo ametoa rai kwao kuwa sehemu ya utafutaji wa maeneo/viwanja vizuri kwa ajili ya matumizi ya Mahakama sambamba na makazi ya Majaji/Mahakimu. 

Mhe. Masaju amesema katika hilo, TAMISEMI imetakiwa kutenga ekari 2 kwa kila Kata kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama mpya za Mwanzo ambazo zitasaidia upatikanaji wa haki karibu kwa wananchi, kuongeza ajira kwa wananchi katika kada mbalimbali na kuleta ustawi wa jamii ambao unasisitizwa pia katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 146(2)(b) isemayo Utawala bora, Usalama na Ustawi wa jamii.

Aidha, katika kuhakikisha kuwa Haki inatolewa kwa wote mapema ipasavyo, Jaji Mkuu amewataka Wasajili/Naibu Wasajili wanapoandaa ratiba za mashauri (causelists) kuhakikisha kuwa, mashauri yote yaliyoiva kwa usikilizwaji yanasikilizwa.

"Sambamba na hili  nitawataka ninyi Wasajili mnaopopanga 'cause lists' zile kwa ajili ya Majaji iwe katika ngazi zote za Mahakama na hasa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani muhakikishe kwamba mashauri yote ambayo yameshaiva kusikilizwa kadri yalivyosajiliwa mahakamani yanapaswa kusikilizwa msiyaruke mkiyaruka ndio mnaleta hii dhana ya Mahakama kufanywa kuwa Sehemu ya kuegesha majalada," amesisitiza Mhe. Masaju. 

Kadhalika, amewataka Wasajili hao kuwa na Ushirikiano na Uwajibikaji kwa kuwa ushirikiano ni nguzo ya mafanikio. Na vilevile kuondoa matabaka ya vyeo kwa kujenga usawa, heshima na mshikamano kazini. Mhe. Masaju ameongeza kwa kutoa rai kwa Wasajili hao kuwa na Ubunifu na kubadili mitazamo na fikra kwakuwa ndio msingi wa ufanisi.

Mhe. Masaju ameongeza kwa kuwakumbusha Wasajili hao kuwa waadilifu hata baada ya kuteuliwa kuwa Majaji na kuacha dhana ya kutaka kuwa Waheshimiwa huku wakiwa wazembe na wavivu kutimiza majukumu yako, badala yake wawe wachapa kazi huku wakiendana na mabadiliko ya vyeo vyao kwa kuzidisha uadilifu na na unyeyekevu.

“Halafu sehemu fulani nimeona Mahakimu wanafanya vizuri wanateuliwa wanakuwa Majaji, baada ya kuwa Jaji akili inaharibika kabisa, unajiuliza hivi huyu mtu tulifanya makosa, mimi nitaendelea kuwafanyia 'monitoring' ili tunaowapendekeza kwenda kuteuliwa wawe ni wale ambao kwa kweli hawana tabia za uvivu, hatutaki cheo cha Ujaji kiwe cheo cha uheshimiwa, kile ni cheo cha utumishi tena cheo kikubwa sana, nilishawaambia kadri unavyokuwa na madaraka makubwa ni kwa kiwango hicho hicho ndivyo unavyopaswa kuwa mnyenyekevu, na kwa kiwango hicho hicho unakuwa mtumishi wa wote  kwa kiwango hicho hicho unakuwa tegemezi kwa wote, sasa wanaopata vyeo vya Ujaji halafu baadae wakaishi maisha ya kujitutumua hatutaki, tunataka mthibitishe kwamba mnaweza kufanya kazi kwa uadilifu,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amesisitiza juu ya vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambavyo ni Utawala wa Bora na Haki, Serikali za Mitaa Imara na zenye Ufanisi, Utumishi wa Umma Ulioimarika, pamoja na Amani, Usalama na Utulivu.

Amewataka pia kuwasimamia vizuri Mawakili wa Serikali na Mawakili wa kujitegemea, huku akisisitiza uwajibikaji bila kusubiri maelekezo na kama wakiona kuwa kuna kitu hakiendi sawa watoe ushauri, huku akiwakumbusha Mawakili wote kuwa wao ni Maofisa wa Mahakama hivyo, mashauri yanaposikilizwa wanatakiwa wawepo ili kusikiliza mashauri ya wateja wao.



Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Wasajili na Naibu Wasajili wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 22 Desemba, 2025 wakati wa kikao kati yake na Wasajili hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu jijini Dodoma. Kikao hicho kimefanyika kwa njia ya Mtandao (Video Conference) ambapo kilifuatiliwa na Wasajili wengine waliopo katika Kanda mbalimbali nchini.

Picha za makundi mbalimbali ya Wasajili na Naibu Wasajili wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipokuwa akizungumza nao leo tarehe 22 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu uliopo Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni