Na FAUSTINEKAPAMA-Mahakama, Lushoto
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, leo tarehe 31 Desemba, 2025 amekabidhi
kwa Mkandarasi Namis Cooperate Limited michoro na eneo itakapojengwa Mahakama mpya
ya Wilaya Lushoto kwa gharama ya fedha za ndani Shilingi za Kitanzania Bilioni
4.272.
Makabidhiano hayo yalifuatiwa
na utiaji saini wa mkataba wa ujenzi uliofanywa na Prof. Ole Gabriel, kwa upande
wa Mahakama, na Bw. James Msumali, kwa niaba ya Mkandarasi.
Hafla hiyo imeshuhudiwa
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe,
pamoja na Viongozi wengine.
Viongozi wengine
waliokuwepo ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batlida Buriani, Mkuu wa
Wilaya ya Lushoto, Mhe. Zephania Sumaye, Wabunge na wengine kutoka Taasisi mbalimbali, Mahakama ya Tanzania na Wadau.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mtendaji Mkuu amemtaka Mkandalasi kukamilisha mradi huo wa ujenzi ndani
ya siku 395 kwa mujibu wa mkataba na kuonya kuwa hapatakuwepo na muda wa nyongeza.
‘Nimeshamwelekeza
Mkandarasi kuwa inapofika tarehe 15 Februari, 2027 saa 4 asubuhi, tutakuwa hapa
kwa ajili ya kupokea jengo letu zuri, nikuombe Waziri, Mkuu wa Mkoa na Viongozi
wengine muwepo siku hiyo…
‘Hatutakuwa na muda wa nyongeza,
hatutakuwa na nyogeza ya gharama na hatutakuwa na utani kwenye suala la kazi
hii, ni kazi muhimu, wananchi wanasubiri Mahakama hii kwa shauku kubwa,’
amesema.
Prof. Ole Gabriel ameeleza
kuwa Mahakama hiyo ni ya kisasa na yenye mfano kwani itakuwa kama maabara
inayowawezesha Wanafunzi wanaosoma Sheria katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto kufanya mazoezi kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mhe.
Prof. Shemdoe amemtaka Mkandalasi kununua vifaa vya ujenzi ndani ya Wilaya ya
Lushoto, ikiwemo mbao, misumari na vingine, jambo litakalowezesha fedha kuzunguka
na kuwanufaisha wananchi wa eneo hilo.
Ameelekeza pia vijana waliopo
katika maeneo ya karibu kupatiwa ajira kwenye mradi huo na kusisitiza kazi ya
ujenzi kukamilika kwa wakati. Hivyo akamhimiza Mkandarasi kuweka mpango kazi
ili kuhakikisha anakabidhi jengo hilo mwezi Februari, 2027.
‘Mimi kama Mbunge wa Jimbo
hili, tutakwenda sambamba, nitahakikisha ninafuatilia kwa ukaribu sana. Sina
wasiwasi na usimamizi wa jengo hili,’ amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa
ameeleza kuwa ujenzi wa Mahakama hiyo utasaidia wananchi kupata haki mapema
ipasavyo na bila kutumia gharama.
Ametumia fursa hiyo
kuwakumbusha wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio la makabidhiano hayo kuwa Mahakama
ya kwanza Tanganyika ilijengwa Tanga, hivyo ujenzi wa Mahakama hiyo mpya ya
Wilaya ni kuendeleza historia katika Mkoa huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Lushoto ameihakikishia Mahakama ya Tanzania kuwa uongozi wa Wilaya yake
utakuwa bega kwa bega kuhakikisha usalama kuanzia kwenye vifaa vya ujenzi na
kutoa ushirikiano wowote watakaouhitaji wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Bi. Victoria Chilewa, amemshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuidhinisha fedha za utekelezaji wa mradi huo.
Amesema kuwa ujenzi wa
Mahakama hiyo utasaidia kuimarisha huduma za utawala bora na kusogeza huduma za
utoaji haki karibu na wananchi. Amesema kuwa kama halmashauri wataendelea kutoa
ushirikiano utakakaohitajika katika sekta zote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni