- Waziri ayakubali, atoa maelekezo
Na
FAUSTINEKAPAMA-Mahakama, Lushoto
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof.
Riziki Shemdoe, ameyakubali maombi yaliyowasilishwa na Mahakama ya Tanzania, ikiwemo
kusamehe tozo zinazotakiwa kulipwa wakati wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi nchini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, aliwasilisha maombi hayo jana tarehe
31 Desemba, 2025 kwenye hafla ya kukabidhi eneo itakapojengwa Mahakama mpya ya Wilaya
Lushoto kwa gharama ya fedha za ndani Shilingi za Kitanzania Bilioni 4.272.
Mhe. Prof. Shemdoe alikuwa Mgeni Rasmi kwenye hafla ya makabidhiano hayo
iliyofanyika wilayani Lushoto.
Katika maombi hayo, Prof.
Ole Gabriel, kwa niaba ya Jaji Mkuu, aliomba Mahakama isitozwe gharama sizizo
za kisheria, ikiwemo zinazohusu utawala wa kihalmashauri, pale panapohitajika viwanja
vya ujenzi wa majengo ya Mahakama, ama kwa ajili ya huduma za Mahakama au
makazi.
Mtendaji Mkuu alimweleza
Waziri kuwa huduma zitakazotolewa na Mahakama baada ya kutekeleza miradi ya
ujenzi huo itawanufaisha wananchi wa halmashauri husika. ‘Tunakuomba Waziri,
kama ikikupendeza, kusamehewa hizi gharama za kiutawala ili kazi nyingine
ziweze kuendelea,’ alisema.
Prof. Ole Gabriel alitoa
mfano katika Mkoa wa Tanga ambapo gharama za kiutawala kwenye halmashauri ni
Shilingi za Kitanzania 250,970,000 kwa mchanganuo kwenye mabano kwa kila Wilaya
za Korogwe [12m/=], Lushoto [10m/=] na Muheza kuna viwanja tisa [31,500,000/=].
Kwa upande wa Pangani
kuna viwanja nane [14m/=], Tanga [3.9m/=], Handeni kuna viwanja 12 [22.99m/=], Mkinga
[13m/=], Kilindi [24m/=] na pia kuna viwanja kwa ajili ya nyumba za Majaji
ambavyo vinafanyiwa upembuzi [118m/=].
Ombi lingine linahusu
utoaji wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama na nyumba za makazi kwa
Majaji na Mahakimu. Prof. Ole Gabriel ameomba Wakuu wa Mikoa kuendelea kuratibu
maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu TAMISEMI kushirikiana
na Mahakama ya Tanzania na Wizara ya Fedha kuhakikisha Kata na Wilaya zote
nchini zinapata majengo yake.
‘Haya maelekezo aliyatoa
tarehe 5 Aprili, 2025 akiwa anazindua jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
jijini Dodoma. Naomba nikupe taarifa kwamba kuna pa kuanzia. Wapo Wakuu wa Mikoa
watatu, Rukwa, Katavi na Tanga, ambao tayari wameshalibeba kidedea suala hili,’
amesema.
Ombi lingine linahusu
Wakuu wa Mikoa kutenga fedha kwa ajili ya kuwezesha kufanyika kwa Kamati za
Maadili za Mahakimu. Mtendaji Mkuu alimweleza Waziri kuwa Wakuu wa Mikoa na
Wilaya ni Wenyeviti wa Kamati hizo katika ngazi husika.
Amemuomba Waziri kushajirisha
suala hilo ili Wakurugenzi ili watenge bajeti kwa ajili ya kuimarisha Kamati
hizo na watambue kuwa zipo kwa mujibu wa Sheria, kwani pale haki inapotendeka,
haki pia inatamalaki na ndiyo hasa Dira ya 2050 inavyoelekeza.
Ombi la nne linahusu
ujenzi wa barabara itakayowezesha wananchi kufika kwa urahisi kwenye Mahakama
hiyo mpya. Mtendaji Mkuu alimuomba Waziri kuwaelekeza TARURA kutengeneza barabara
angalau kwa changalawe kwa kuanzia kabla ya kiwango cha lami ili kumwezesha Mkandarasi
kuendelea na ujenzi.
Akijibu maombi hayo kwa
kuanzia na suala la gharama za utawala, Prof. Shemdoe amemwelekeza Katibu Mkuu
wa TAMISEMI kuona namna kama kufutwa kwa tozo hizo hakutavunja sheria. ‘Nadhani
milioni 250 siyo fedha nyingi kihivyo, zinaweza kuondolewa na mambo mengine haya
ya Mahakama yakaendelea,’ amesema.
Akizungumzia suala la Kamati
za Maadili, Mhe. Prof. Shemdoe pia amemwelekeza Katibu Mkuu kutoa mwongozo kwa mamlaka
za Serikali za Mitaa ili kutenga bajeti kuwawezesha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia
Kamati hizo kwa ajili ya watendaji wa Mahakama.
“Hili ni jambo la msingi
ambalo lipo kisheria na lipo kwenye utaratibu wa kazi za Viongozi hawa. Naomba utoke
waraka wa kuweza kuwaelekeza Wakurugenzi kutenga bajeti kwenye eneo hili,”
amesema.
Kuhusu kuwepo kwa majengo
ya Mahakama kwenye kila Kata na Wilaya, Waziri Shemdoe alisema kuwa tarehe 16
Desemba, 2025 alisaini barua kwenda kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanalichukulia
zoezi hilo kwa uzito mkubwa.
Alifurahi kusikia kuwa
Wakuu wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Tanga wamekuwa mstari wa mbele, hivyo kwa
mara nyingine aliwaelekeza Wakuu wa Mikoa 23 iliyobaki kulifanyia kazi jambo
hilo na kulichukulia uzito unaostahili.
Kuhusu TARURA, Waziri
Shemdoe ameielekeza Taasisi hiyo kuanzia Wilaya ya Lushoto, Mkoa wa Tanga na Makao
Makuu kuhakikisha kwenye bajeti inayofuata wanatenga fedha kwa ajili ya barabara
ya kwenda kwenye jengo hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni