Ijumaa, 9 Januari 2026

JAJI MFAWIDHI MAHAKAMA KUU KANDA MPYA YA SIMIYU ARIPOTI RASMI

Na NAUMI SHEKILINDI, Mahakama-Simiyu

Hivi karibuni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu, Mhe. Wilbert Chuma amekaribishwa na watumishi wa Mahakama mkoani humo akitokea Mwanza ikiwa ni mara ya kwanza kufika katika Kituo hicho tangu alipoteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa  Kanda hiyo mpya.

Itakumbukwa kuwa, Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu ilitangazwa kuwa Mahakama Kuu kwa tangazo la Serikali na.690 la 2025 kuanza kutoa huduma kuanzia tarehe 02 Januari, 2026.

Watumishi Mkoani Simiyu wakiongozwa na Kaimu Naibu Msajili, Mhe. Martha Mahumbuga pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita walimkaribisha Jaji Mfawidhi huyo kwa furaha kubwa ikiwa ni pamoja na kumuahidi kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji.

Aidha, Mhe. Chuma alitembelea jengo jipya la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu na kujionea muonekano wa jengo hilo pamoja na samani za kisasa zilizomo ndani ya jengo hilo.

Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo alipata nafasi ya kuongea na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu (IJC) na kuwasisitiza kuwa na ushirikiano katika kazi, kutoa huduma bora kwa wateja wa nje na ndani, vilevile kila mtumishi anatakiwa kuyatambua majukumu yake ili kuweza kufikia malengo na Dira ya Mahakama.

 


  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu, Mhe. Wilbert Chuma akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu alipowasili katika Mahakama hiyo hivi karibuni.

     Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu, Mhe. Wilbert Chuma (wa kwanza kulia) na viongozi wengine wakikagua ubora wa samani katika chumba cha mafunzo ndani ya IJC Simiyu.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu, Mhe. Wilbert Chuma (aliyesimama) akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu alipowasili katika Mahakama hiyo hivi karibuni. Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita na kulia ni Kaimu Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga.




Watumishi wa Mahakama Kanda ya Simiyu wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo alipokuwa akizungumza nao hivi karibuni.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni