Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Mkutano Mkuu wa Mwaka
unaowaleta pamoja Mahakama na Majaji wote nchini umeanza leo tarehe 13 Januari,
2026 katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mkutano huo wa Chama cha
Mahakimu na Majaji Tanzania [TMJA] umefunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na Viongozi
mbalimbali wa Serikali na Mahakama.
Jumla ya wanachama wa TMJA zaidi ya 1,200 wamehudhuria Mkutano huo, ambao ni wa pili kufunguliwa na Mkuu wa Nchi tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1984. Mkutano mwingine ulifanyika mwaka 1984 na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere jijini Arusha.
Rais Samia aliwasili
kwenye ukumbi wa Mkutano majira ya saa 4.30 asubuhi na kupokelewa na Jaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, Rais wa TMJA, Mhe. Elimo Masawe, Waziri
wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary
Senyamule.
Wengine ni Amidi wa
Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof.
Elisante Ole Gabriel na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya.
Baada ya kuwasili, wimbo
wa Taifa ulipigwa ukafuatiwa na ule wa Afrika Mashariki, huku Bendi ya Jeshi la
Polisi ikiongoza wanachama wa TMJA na watumishi wengine kushiriki kuimba nyimbo
hizo.
Baada ya utambulisho
uliofanywa na Rais wa TMJA, ilifuata burudani kabambe kutoka Kikundi cha Ngoma
za Asili Maheza iliyokonga nyoyo za wanachama kufuatia midundo na uchezaji
mahiri uliooneshwa na wanamichezo hao.
Mhe. Masawe pia alitumia
fursa hiyo, kabla ya kikundi cha ngoma kutumbuiza, kutoa salamu. Katika salamu
zake, Rais wa TMJA alimshukuru Rais Samia kwa kukubali mwaliko wao na kuwa
mgeni rasmi kwenye Mkutano huo, ukiwa ni mwaka wa 41 tangu kuundwa kwa chama
hicho.
‘Uwepo wako umeonesha
uwazi na dhamira ya Serikali unayoiongoza katika kuimarisha uhuru wa Mahakama
kama ilivyo kauli mbiu ya Mkutano huu, yaani Jukumu la Mahakama Huru katika
Utoaji wa Haki,’ alimweleza Mhe. Dkt. Samia.
Mhe. Masawe alimweleza
Rais Samia kuwa chama cha JMTA ni cha kitaaluma chenye malengo mbalimbali, ikiwemo
kukuza na kulinda uhuru wa Mahakama kama sharti la msingi na la lazima la
utekelezaji wa majukumu ya kimahakama.
Malengo mengine ni kukuza
maslahi na ustawi wa wanachama, kudumisha hadhi, heshima na tamaduni za Majaji
na Mahakimu, kuongeza na kuendeleza ujuzi, maarifa na uelewa wa Majaji na
Mahakimu kuhusu majukumu yao ya kimahakama kupitia tafiti endelevu na elimu ya
kitaaluma.
Mengine ni kutoa taarifa
na machapisho mbalimbali kuhusu masuala yenye maslahi au yanayowahusu wanachama,
kuandaa makongamano na mikutano ya wanachama na kudumisha mahusiano ya karibu
kadri inavyowezekana miongoni mwa wananchama na kushirikiana, na inapobidi,
kujiunga na vyama au Taasisi nyingine zenye malengo yanayofanana.
Jumla ya mada 12, ikiwemo
‘Jukumu la Mahakama la Mahakama Huru katika Utoaji Haki’ zinatarajiwa
kuwasilishwa wakati wa Mkutano huo wa siku tatu na kufuatiwa na Bonanza
litakaloshirikisha michezo mbalimbali, ikiwemo Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete,
Kamba na mingine mingi.
Kama sehemu ya Mkutano
huu, wamachama wa TMJA wanatarajia kufanya matendo ya huruma kwenye vituo
viwili ambavyo vinahudumia watoto wenye changamoto mbalimbali wanaoanzia umri
wa miezi sita hadi miaka 17.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni