- Apongeza maboresho yanayofanywa na Serikali kwa Mhimili wa Mahakama
- Ashauri Serikali kuharakisha mchakato kuwezesha migogoro ya ardhi kusikilizwa na Mahakama
- Asema muundo wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama kubadilishwa
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju amesema kuwa, Mahakama nchini imepiga hatua kubwa za
kuboresha mfumo wa utoaji haki kikatiba, kisheria, kisera na kiutendaji ili
kuhakikisha inaendelea kuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mhe. Masaju ameyasema
hayo leo tarehe 13 Januari, 2026 wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa
Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) unaofanyika Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
“Serikali imeendelea na
jitihada nyingi za kuiwezesha Mahakama kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na
ufanisi, hatua hizo zimeleta mafanikio makubwa yanayoonekana katika nyanja mbalimbali
za utoaji haki,” amesema Jaji Mkuu.
Akinukuu Ibara ya 107 (A) (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kwamba mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki, katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama. Hivyo, Mhe. Masaju amesema, kwa kuwa Mahakama ni sehemu ya Serikali na Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ipasavyo Mahakama hiyo inapaswa kuwa huru, isiingiliwe na Mihimili mingine inayounda Serikali na Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaani Mihimili ya utendaji na Bunge licha ya ushirikiano uliopo miongoni mwao. Ni kwa sababu hiyo Ibara ya 107B ya Katiba inaelekeza kwamba katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki; Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi huku ikiwajibika kuzingatia, kutia maanani na kutekeleza masharti yote yaliyotajwa katika Ibara ya 6-11 ya Katiba kama Ibara ya 7 ya Katiba inavyoelekeza.
Aidha, Mhe. Masaju amepongeza maboresho yote yanayofanywa na Serikali kwa Mhimili wa Mahakama na kukiri kuwa, yanaakisi dhamira ya dhati ya kuimarisha uhuru wa Mahakama kwa vitendo.
“Ni ukweli usiopingika
kwamba, Mahakama haiwezi kuwa huru iwapo haina miundombinu ya msingi,
rasilimali fedha na mazingira salama ya kutekeleza majukumu yake. Ujenzi wa
majengo ya Mahakama, uwezeshaji wa rasilimali watu na fedha pamoja na kuboresha
mazingira ya kazi kwa Majaji, Mahakimu na watumishi wa Mahakama ni nguzo muhimu
zinazowezesha uhuru wa Mahakama kuwa halisi, unaoonekana na unaotekelezeka kwa
ustawi wa wananchi na utawala wa sheria kwa ujumla,” ameeleza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesema katika
kuonesha dhamira ya kulinda na kuimarisha uhuru wa Mahakama, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Serikali ya Awamu
ya Sita wakati wa hafla ya uapisho wa Jaji Mkuu tarehe 15 Juni, 2025, Rais
Samia alitoa maelekezo kwa Jaji Mkuu kuhakikisha kuwa, Mahakama ya Tanzania
inakuwa yenye hadhi duniani.
“Hakuna shaka kwamba
ulipotoa maelekezo hayo, ulikuwa na ufahamu mpana na vigezo maalum vinavyopima
Mahakama yenye hadhi duniani ambavyo kwa kiasi kikubwa vinajengwa juu ya uhuru
wa Mahakama katika kufanya maamuzi yake bila woga, upendeleo au shinikizo
kutoka pande zozote,” amesema Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju
ametaja vigezo vya kimataifa vinavyotumiwa na Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia,
‘International Commission of Jurists, ‘World Justice Project’ (WJP) na taasisi
nyingine za Kikanda na Kimataifa za utawala wa sheria, hutumia viashiria maalum
kupima utendaji na ubora wa mfumo wa Mahakama ikiwa ni pamoja na Uhuru wa Mahakama
na kutopendelea upande wowote, Usalama wa ajira ya Majaji na Mahakimu, Urahisi
wa kufikia huduma za haki, Ufanisi na kuzingatia wakati.
Ametaja vigezo vingine kuwa ni pamoja na uadilifu na uthabiti, upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha, maslahi na stahiki za kutosha zinazolindwa Kisheria na Miundombinu na Teknolojia.
Jaji Mkuu amesema kwamba, licha ya Mahakama kupiga hatua kubwa katika baadhi ya sifa au vigezo vilivyoanishwa na taasisi za Kimataifa na za Kikanda kuhusu viashiria vya kiutendaji na ubora wa mfumo wa Mahakama huru kikatiba, kisheria na kisera na kiutendaji, bado Mhimili huo ukabiliwa na changamoto katika baadhi ya vigezo hasa katika kigezo cha saba na cha nane, vinavyohusu Upatikanaji wa Rasilimali Fedha za Kutosha (Adequate Availability of Financial Resources) na Maslahi na Stahiki za Kutosha Zinazolindwa Kisheria (Adequate and Secure Emoluments).
Ameongeza kwa, kuahidi kwamba, vigezo ambavyo viko ndani ya uwezo wa Mahakama, kama vile matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), matumizi ya Lugha ya Kiswahili, usikilizaji wa mashauri na ukamilishaji wake mapema ipasavyo, kusogeza huduma karibu na wananchi, kuchapishwa kwa maamuzi ya Mahakama, uadilifu, weledi, uwajibikaji na mengine yataendelea kusimamiwa na kutekelezwa ipasavyo ili kuendelea kuwa Mahakama huru na kufikia kuwa Mahakama yenye hadhi duniani.
Hata hivyo, Mhe. Masaju ameiomba Serikali kuongeza bajeti ya Mahakama pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama kwa ujumla, ikiwemo kuimarisha huduma za bima ya afya ili ziendane na mahitaji maalum yanayotokana na asili na mazingira ya kazi wanayoifanya.
“Kuongezeka kwa bajeti ya Mahakama kutaiwezesha kuendelea kufanya maboresho ya kiutendaji, kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi, na kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa utoaji haki nchini,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Kadhalika Mhe. Masaju ameeleza kwamba, kuongezeka kwa maslahi ya watumishi kutaimarisha uhuru wa Mahakama ambao unaweza kuingiliwa (compromised) pale mtumishi wa Mahakama anapokuwa na hali duni sana ya kimaslahi.
“Kazi ya Jaji au Hakimu ni kazi inayohitaji kujitenga kwa namna fulani ili kuepusha muingiliano wa kimaslahi katika mambo mbalimbali zikiwemo shughuli za kiuchumi za kujipatia kipato,” ameeleza Jaji Mkuu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju ametaja masuala mengine yanayoweza kuathiri ubora na uhuru wa Mahakama kufikia Mahakama yenye hadhi duniani kuwa ni pamoja na mashauri yanayohusu migogoro ya Ardhi Kuendelea Kusikilizwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.
Amebainisha kuwa, hali ilivyo sasa ni kwamba mashauri ya migogoro ya ardhi yanashughulikiwa katika Mhimili wa mahakama (Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani), Wizara ya Ardhi (Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya) na TAMISEMI (Mabaraza ya Kata, Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji) na kwamba hali hiyo inasababisha mkanganyiko katika mfumo wa utoaji haki nchini kwani jukumu la utoaji haki nchini ni la Mahakama hata kama Mabaraza mbalimbali (Tribunals) nayo yanatambuliwa na Katiba katika Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba.
“Kwa kuzingatia changamoto zilizopo katika mfumo wa utatuzi wa mashauri ya migogoro ya ardhi; na kwa kuwa Serikali iko katika mchakato wa kufanya maamuzi kwamba mashauri yote ya migogoro ya ardhi ngazi ya Kata na Wilaya yasikilizwe na Mahakama ya Tanzania; na Mahakama ya Tanzania tunao uwezo wa kusikiliza mashauri ya migogoro ya ardhi ipasavyo, tunaishauri Serikali iharakishe mchakato wa kuwezesha mashauri yote ya migogoro ya ardhi kusikilizwa na Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na kuendelea hata Mahakama za juu kabisa nchini,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju ameongeza kwamba, Mabaraza ya Ardhi hayapo katika wilaya zote nchini, jambo linalowanyima wananchi wengi kupata haki zao sawa kwa wote mapema ipasavyo. Ameongeza kwa kusema kuwa, “Hii ni tofauti na mfumo wa Mahakama ambao tayari una Mahakama za Wilaya katika wilaya zote isipokuwa Wilaya tatu za Chamwino na Mkalama ambako ujenzi wa Mahakama unaendelea na Wilaya ya Ikungi ambapo ujenzi wa majengo ya Mahakama utaanza mwaka wa fedha ujao.”
Akizungumzia kuhusu Usimamizi wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama, Jaji Mkuu amesema kuwa baada ya Mahakama kutafakari kwa kina kuhusu muundo wa sasa wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama zinazoundwa chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mahakama (Judiciary Administration Act, Cap. 237), amesema wanakusudia kufanya maboresho ya muundo huo ili kuimarisha uhuru wa Mahakama kwa kuhakikisha kuwa usimamizi na nidhamu ya watumishi wake unafanyika ndani ya mfumo wa Mahakama yenyewe, bila kuingiliwa na vyombo vya utendaji vya Serikali.
“Katika muktadha huo, inakusudiwa kubadili muundo wa sasa ambapo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na Maafisa Tawala wa Mikoa na Wilaya wataondolewa kwenye Kamati hizo. Kwa muda mrefu, mfumo huu umeleta mgongano wa kimaslahi kwa kuwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ni viongozi wa utendaji na wanasiasa, hali inayoweza kuathiri uhuru wa Hakimu katika utoaji wa maamuzi,” amesisitiza Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amebainisha kuwa, mapendekezo ya Muundo mpya ni kwamba, Kamati hizo sasa zitaongozwa na Viongozi wa Mahakama yenyewe katika ngazi hizo.
Amesema kuwa, muundo huo wa Kamati za Maadili ya watumishi wa Mahakama (self-regulation) utajenga ujasiri, uhuru na uwajibikaji kwa Mahakimu na Majaji kutoa maamuzi kwa mujibu wa sheria na ushahidi bila hofu ya kuingiliwa na mhimili wa utendaji.
“Mahakama ya Tanzania tupo tayari tumeshirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa rasimu ya Muswada kwa ajili hiyo kwa ajili ya hatua zake zaidi ipasavyo ili muswada ufikishwe Bungeni mapema,” amesema Mhe. Masaju.
Kadhalika, Jaji Mkuu amezungumzia kuhusu suala la Makazi bora na salama kwa ajili ya Mahakimu na Majaji ambapo amesema, “tunashauri kwamba Mahakimu na Majaji wawezeshwe kuishi katika maeneo salama yenye hadhi kama ilivyokuwa zamani. Aidha, zinapokuwepo nyumba za Serikali zilizowazi basi, Majaji na Mahakimu wapewe kipaumbele kupewa nyumba hizo katika maeneo ya Low Density na secure kama ilivyokuwa zamani. Vinginevyo, Mahakama itengewe bajeti inayotosheleza kulipia pango Majaji na Mahakimu katika maeneo salama ili kulinda usalama, hadhi na heshima yao katika jamii.”
Amesema, kwa sasa ambapo Majaji na Mahakimu wengi wanapanga nyumba binafsi hali inayoweza kuathiri kiwango chao cha kuwa huru katika maamuzi kwa waliowapangisha.
“Tayari tumeomba TAMISEMI, waitengee Mahakama viwanja kwa ajili ya makazi ya Mahakimu na Majaji katika maeneo yanayofaa kukaliwa na Viongozi lakini pia viwanja kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hapo baadaye mahitaji ya matumizi ya Mahakama yatakapokuwa yameongezeka mijini,” ameeleza Mhe. Masaju.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amezungumzia pia kuhusu usafiri kwa ajili ya Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama ili kuimarisha, uhuru wa Mahakimu, usalama na heshima yao, hivyo ameshauri kwamba Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama nao wafikiriwe kupatiwa usafiri wa pamoja wa ofisi wa kuwapeleka kazini na kuwarejesha nyumbani, ama Serikali iweke utaratibu utakaowawezesha Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama kupata mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kujinunulia vyombo vya usafiri hususani magari kwa ajili hiyo.
Jumla ya
wanachama wa TMJA zaidi ya 1,200 wamehudhuria Mkutano huo wenye Kaulimbiu
isemayo, ‘Jukumu La Mahakama Huru Katika Utoaji
Haki.’
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) leo tarehe 13 Januari, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni