Jumanne, 13 Januari 2026

SERIKALI KUENDELEA KULINDA, KUHESHIMU UHURU WA MAHAKAMA; RAIS SAMIA

Na FUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza Mahakimu na Majaji kwa kazi nzuri wanazozifanya za kuwahudumia wananchi katika muktadha mzima wa utoaji haki nchini.

Mhe. Dkt. Samia ametoa pongezi hizo leo tarehe 13 Januari, 2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa siku tatu unaofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

"Nawapongeza Majaji na Mahakimu kwa kazi mnayofanya kwa ajili ya raia wa Tanzania. Majukumu yenu yanadai zaidi ya maarifa ya kisheria; yanahitaji hekima na ujasiri kulinda wasio na hatia na kuzingatia sheria bila kuwapendelea wenye nguvu au kuwakandamiza wanyonge," Rais Samia amesema.

Amesema Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu uhuru wa Mahakama, huku akisisitiza uwajibikaji, uadilifu, nidhamu, utii wa sheria na uzalendo kwa Taifa.

Rais Samia amesema Watanzania wana matarajio makubwa na Mahakama kwa kutoa haki kwa uwazi, kwa kuzingatia Katiba, Sheria na maadili yanayojali utu wa binadamu.

Amesema kwamba, tafiti za mara kwa mara zinaonesha kuwa imani ya wananchi kwa Mahakama imeongezeka, jambo ambalo linatia moyo Mahakama zinafanya kazi ya kuridhisha.

Rais Samia ameeleza pia kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha utendaji wa Mahakama, ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo. Amebainisha kuwa jengo la Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma ni la sita la aina yake duniani na la kwanza barani Afrika, akieleza kuwa hayo ni mafanikio makubwa.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia amesema kwambrasilimali watu imeongezeka, huku Majaji wengi wakiteuliwa na Mahakimu kuajiriwa katika ngazi zote na kuboresha maslahi kwa ustawi wa wafanyakazi.

"Pia tumeimarisha matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA], ambayo yanaunga mkono kikamilifu utoaji wa haki," amesema.

Dk Samia amemeeleza kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025–2050 ambayo inazingatia utawala bora, amani, usalama na utulivu, huku Mahakama ikiwa na jukumu kubwa katika kujenga Taifa linalozingatia haki na utulivu.

"Serikali imepitisha mpango wa muda mrefu wa utekelezaji wa Dira ya 2050. Asilimia 22 ya shughuli zitatekelezwa na Serikali, asilimia 70 kwa ubia na sekta binafsi, na asilimia nane na Taasisi za umma. Mahakama ina jukumu kubwa la kusimamia mchakato huu na kutetea haki za wananchi na maslahi ya Taifa," amesema Rais Samia.

Kuhusu migogoro ya ardhi, Mhe. Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali inapanga kutenga bajeti ya kutosha kujenga Mahakama za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini, sawa na uwekezaji unaofanywa katika vituo vya afya, hatua itakayosaidia mashauri ya ardhi kushughulikiwa kwa ufanisi.

Aidha, Rais Samia aliwakumbusha Majaji na Mahakimu kusimamia haki kwa mujibu wa Katiba, Sheria na viwango vya maadili kwa mujibu wa viapo vyao.

"Ni muhimu kwa wale wanaotoa haki kusimama kidete upande wa haki wakati wa kufanya uamuzi, bila woga au upendeleo," amesema.

Rais Samia amemnukuu Hayati Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa anafungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho mwaka 1984 na kusisitiza kuwa, kazi ya kusimamia haki ni ngumu na inahitaji uadilifu mkubwa na kwamba sio kila mtu anaweza kuitekeleza kwa ufanisi.

"Hakuna Taifa linaloweza kupata maendeleo endelevu au ustawi wa watu wake bila usimamizi mzuri wa haki," amesema na kuongezea, "Mahakama huru, yenye uwezo na maadili ni nguzo muhimu ya utawala bora na msingi wa upatikanaji wa haki."

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizungumza leo tarehe 13 Januari, 2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa siku tatu unaofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania, Mhe. Elimo Masawe, akiwatambulisha Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo.

Sehemu ya wanachama wa TMJA [juu na chini] wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla hiyo.


Sehemu nyingine ya wanachama wa TMJA [juu na chini] wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla hiyo.


Sehemu nyingine ya tatu ya wanachama wa TMJA [juu na chini] wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla hiyo.


Sehemu nyingine ya nne wanachama wa TMJA [juu na chini] wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla hiyo.


Sehemu nyingine ya tano wanachama wa TMJA [juu na mbili chini] wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla hiyo.






 

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni