MAJAJI, MAHAKIMU WAPATIWA MAARIFA KUHUSU UHIFADHI WANYAMAPORI, MIAMALA YA KIFEDHA
Na FUSTINE KAPAMA na
HALIMA MNETE-Mahakama, Dodoma
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa
Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania [TJMA] umeingia siku ya pili leo tarehe
14 Januari, 2026 kwa wanachama kupitishwa kwenye mada kadhaa na wawezeshaji wabobezi
ili kuwajengea uelewa kwenye maeneo mbalimbali, ikwemo uhifashi wa wanyamapori, utalii na miamala ya kifedha.
Mada ya kwanza
kuwasilishwa kwenye Mkutano huo wa siku tatu, unaofanyika Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania [Judiciary Square] jijini Dodoma, ilihusu mafanikio, changamoto
na mustakabali wa ulinzi wa wanyamapori Tanzania.
Ofisa Mwandamizi kutoka
Shirika la Hifadhi Tanzania [TANAPA] Joachim Tesha, ndiye aliyewasilisha mada
hiyo, huku Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Winfrida Korosso, akiwa
msimamizi mkuu wa majadiliano.
Kadhalika, wanachama wa TMJA
walipitishwa kwenye mada linganifu inayohusu dhana ya uhifadhi-Mamlaka Ngorongoro;
mafanikio, fursa na changamoto. Mada hiyo iliwasilisha na Ofisa kutoka kwenye
Mamlaka hiyo Usaje Mwambene.
Baada ya mapumziko
mafupi, wajumbe wa Mkutano waligawanyika kwenye makundi matatu. Kundi la kwanza
linajumuisha Majaji wa Mahakama ya Rufani ambalo lilipitishwa kwenye mada
inayohusu mchango wa utalii kwenye uchumi na maendeleo ya nchi.
Mada hiyo iliwasilishwa
na Ofisa Mwandamizi kutoka TANAPA July Lyimo, huku Jaji wa Mahakama ya Rufani
Tanzania, Mhe. Rehema Mkuye, akiwa msimamizi mkuu wa majadiliano.
Kundi jingine limejumuisha
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili na Wasaidizi wa Sheria wa
Majaji. Mada kwenye Kundi hili ilihusu uhifadhi endelevu wa rasilimali ya
wanyamapori na mchango wa Mahakama katika uhifadhi.
Mada hii iliwasishwa na maofisa
kutoka Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania [TAWA] P. Marina na R. Komba,
huku Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ilvin Mugeta akiwa msimamizi wa
majadiliano.
Kundi la tatu limehusisha
Mahakimu wa ngazi mbalimbali wanaohudumu kuanzia Mahakama za Hakimu Mkazi,
Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo. Wajumbe hawa wamepitishwa kwenye mada
kuhusu umuhimu wa misitu na changamoto za uhifadhi.
Mada hiyo iliwasilishwa na David Mungo’ong’o na Dkt. Zainabu Bungwa kutoka Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania [TFS], huku Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto [IJA], Mhe. Dkt. Particia Kisinda, akiwa msimamizi
mkuu wa majadiliano.
Baadaye mchana, wajumbe wa Mkutano huo walikusanyika pamoja na kupitishwa kwenye mada nyingine inayohusu uendeshaji wa mifuko ya kijamii, fursa, changamoto na mustakabali wake.
Watoa mada walikuwa Bw. Cosmas Sasi, Bw. James Oigo na Bw. Geofrey
Sirika, huku Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Berke Sehel akiwa
msimamizi mkuu wakati wa majadiliano.
Jana tarehe 13 Januari, 2026, wanachama wa TJMA walipitishwa kwenye mada tatu, ikiwemo inayohusu jukumu la Mahakama huru katika utoaji haki. Mada hii iliwasilishwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Deo Nangela, huku Amidi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija akiwa msimamizi mkuu wa majadiliano.
Mada hiyo ilichangiwa na
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali, Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Rose Ebrahim na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi.
Nyingine ilihusu uelewa
wa miamala na bidhaa mbalimbali; changamoto zinazotolewa na sekta ya benki na
fedha nchini [nafasi ya Majaji, Wasajili na Mahakimu]. Mtoa mada hii alikuwa Bw.
Godwin Ngilimi, huku Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Shaban Lila
akiwa msimamizi wa majadiliano.
Mada nyingine ilihusu
bidhaa ya miamala, changamoto na namna ya kuzishughulikia; mikopo kwa ujumla
wake, miamala ya biashara za kimataifa, dhamana mbalimbali za kibenki,
uwekezaji katika dhamana na hati fungani na changamoto katika utekelezaji wa
amri za Mahakama.
Watoa mada kwenye maeneo
hayo walikuwa Bw. Frank Mukoyogo, Bw. Prosper Mwangamila, Bw. Xavery Makwi, Bi.
Juliana Kombe na Bw. Paschal Mihayo. Msimamizi wa majadiliano alikuwa Amidi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju, alihudhuria uwasilishaji wa mada hizo katika siku
ya kwanza baada ya ufunguzi wa Mkutano huo.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alifungua Mkutano huo na
kuwapongeza Mahakimu na Majaji kwa kazi nzuri wanazozifanya za kuwahudumia
wananchi kwenye muktadha mzima wa utoaji haki nchini.
Awali, akizungumza wakati
akiwakarisha wanachama kwenye Mkutano huo, Rais wa TMJA, Mhe. Elimo Masawe, alisema
kuwa mustakabali wa haki nchini unategemea umoja, maadili na weledi, hivyo Chama
cha Mahakimu na Majaji Tanzania kina nafasi muhimu katika kulinda na kuendeleza
mhimili wa mahakama.
Mhe. Masawe alieleza kuwa
chama hicho ni jukwaa muhimu la kitaaluma linalowaunganisha Majaji na Mahakimu,
hivyo kinapaswa kuendelea kuwa sauti ya kulinda uhuru wa Mahakama, hadhi ya
Majaji na Mahakimu pamoja na maslahi yao ya kitaaluma na kiustawi.
Alihimiza wanachama wapatao
1,200 waliohudhuria Mkutano huo, na wale ambao hawakupata nafasi kwa sababu
mbalimbali, kuzingatia misingi ya haki, uadilifu na uwajibikaji katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mkutano Mkuu wa Chama cha
Mahakimu na Majaji Tanzania unaendelea kuwa jukwaa muhimu la kutathmini
mwenendo wa haki nchini na kuweka mikakati ya kuimarisha taaluma na maadili kwa
maslahi mapana ya Taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni