Na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amewataka Majaji, Mahakimu,
Wasuluhishi, Wadau na Wananchi kwa ujumla kuzingatia na kutekeleza mambo manne
muhimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kuendeleza na kutambua umuhimu
wa matumizi ya usuluhishi.
Akizungumza leo tarehe 19
Januari, 2026 katika Hafla ya Utoaji Tuzo kwa Wadau wa Usuluhishi kwa mwaka
2025 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam,
Mhe. Dkt. Siyani amesema, Mahakama imeendelea
kuchukua hatua mbalimbali na kuweka vipaumbele mahususi vyenye lengo la
kuhakikisha mashauri yanayosajiliwa mahakamani, yanakamilika mapema
ipasavyo na usuluhishi kama sehemu ya utekelezaji wa takwa la katiba ya nchi
yetu katika ibara ya 107A (2), umepewa kipaumbele
kikubwa.
“Nimesikia
takwimu zilizowasilishwa na Jaji Mfawidhi kuhusu mafanikio ya usuluhishi kwa
mwaka 2025, ni dhahiri
kwamba Mahakama na wadau wa usuluhishi wamendelea kutumia usuluhishi kama nyenzo madhubuti yenye kuaminika katika utatuzi wa migogoro. Hata hivyo, kwakuzingatia wingi wa mashauri katika nchi yetu, bado kuna nafasi zaidi kwa wananchi kutumia njia hii kutatua migogoro yao,” amesema Jaji Kiongozi.
Mhe. Dkt. Siyani ameyataja mambo manne
ya kuzingatia katika kuendeleza matumizi ya Usuluhishi kuwa ni pamoja na kuongeza elimu kwa umma kuhusu usuluhishi, kuwekeza katika
mafunzo endelevu, ni muhimu kuwekeza
katika mafunzo ya mara kwa mara kwa
wapatanishi, Matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuendeleza na kukuza ushirikiano wa wadau,
ni kwa kupitia ushirikiano huu wa karibu kati ya Mahakama na Wadau wote.
Akizungumzia kuhusu kuongeza elimu kwa umma kuhusu usuluhishi, Jaji Kiongozi amesema, ni jukumu la Wadau wote
wa Mahakama kuwaelimisha wananchi kwamba haki inaweza pia
kupatikana kupitia mazungumzo, maridhiano na makubaliano yanayoheshimu maslahi ya pande zote.
Kuhusu suala la kuwekeza katika
mafunzo endelevu, Mhe. Siyani ameeleza kwamba, ni muhimu
kuwekeza katika mafunzo ya mara kwa mara kwa wapatanishi ili
kuimarisha uelewa, mbinu za njia za usuluhishi, kutambua na kushirikiana katika kujenga mifumo
yenye ufanisi na mazingira bora ya uendeshaji wa njia za usuluhishi
zinazoendana na vigezo vinavyotumika katika
upimaji wa mfumo wa utoaji haki wa migogoro ya madai.
Katika jambo hilo, Jaji Kiongozi amekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Kituo cha Usuluhishi kwa juhudi za kuwezesha mafunzo ya njia ya upatanishi kwa Wahe Majaji na Mahakimu katika kuwajengea uwezo wa kufanya usuluhishi.
Katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mhe. Siyani amewataka Wadau wa Haki kuyazingatia kwa kuwa hayakwepeki katika zama hizi ambapo amesema, “Sote ni mashuhuda wa namna matumizi ya mifumo ya kidijitali yalivyokuwa injini ya mageuzi katika mifumo ya utoaji haki duniani. Uwekezaji katika TEHAMA si hiari, ni muhimu ili kuongeza ufanisi na upatikanaji wa huduma kwa wakati.”
Ameongeza
kuwa, Mahakama kupitia mageuzi ya teknolojia, mifumo kama Mfumo wa Kielektroniki
wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) na Usuluhishi Mtandao(Virtual/Online Mediation) yameleta mapinduzi makubwa katika upatikanaji wa huduma za usuluhishi
na kwamba matumizi ya teknolojia yamepunguza
kwa kiasi kikubwa gharama, muda unaotumika kufika mahakamani, pamoja
na nguvu kazi inayohitajika na hivyo kuongeza upatikanaji wa haki bila vikwazo.
Aidha,
kuhusu jambo la kuendeleza na kukuza ushirikiano wa wadau, Jaji Kiongozi
amesema kuwa, ushirikiano wa karibu kati ya Mahakama na Wadau wote ndio utakaohakikisha kuwa usuluhishi unakuwa njia yenye matokeo
endelevu, inayotekelezeka na inayokubalika katika jamii.
“Kupitia ushirikiano huu tutaweza kujenga msingi wa kujenga taifa linalothamini mazungumzo, linaloweka
mbele maridhiano na linajenga mfumo wa utoaji haki unaotazama utu na maendeleo ya watu wake,” amesisitiza.
Katika
hafla hiyo, Mhe. Dkt. Siyani amewajuza Wadau wote wa Mahakama kuwa kutakuwa na
Wiki ya Usuluhishi na kuwaomba wadau wote wa usuluhishi na wanufaika wa huduma hizi, kuweka juhudi za pamoja katika kufanikisha wiki hiyo ambayo ni ya kihistoria na inayotarajiwa kutoa fursa nyingi
za kutoa elimu ya usuluhishi.
“Niwaombe pia wananchi kutumia fursa hii katika
kupata elimu na kutatua migogoro kwa
njia rahisi na kukuza utamaduni na desturi za kiafrika katika kutatua
migogoro nje ya Mahakama kwa njia za maridhiano, hasa kwa kuzingatia uwepo wa Wapatanishi na Wasuluhishi
binafsi ambao hivi sasa wanatambulika kisheria,”
amesema Jaji Kiongozi.
Kadhalika,
Mhe. Dkt. Siyani ametoa wito kwa wadau wote
wa mfumo wa utoaji haki, kuchagua njia za usuluhishi kwa mujibu wa sheria, badala
ya kupitia mchakato mrefu, wa gharama wa kimahakama unaohitaji
kusubiri hukumu ambayo wakati mwingine huongeza maumivu ya mgogoro badala ya
kutibu majeraha ya mgogoro kama ilivyo katika njia za usuluhushi ambazo msingi wake mkuu ni maridhiano.
Sambamba
na hilo, Mhe. Dkt. Siyani pia wananchi
kutumia fursa ya wiki hiyo katika kupata elimu na kutatua migogoro kwa njia rahisi na kukuza utamaduni na desturi za
kiafrika katika kutatua migogoro nje ya Mahakama kwa njia za maridhiano, hasa kwa kuzingatia uwepo wa Wapatanishi na Wasuluhishi binafsi
ambao hivi sasa wanatambulika kisheria.
Hafla hiyo imebeba
kauli mbiu isemayo; 'Kujenga maelewano na
kuimarisha ushiriki wa wadau katika upatanishi kwa matokeo endelevu.'
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji walioshiriki kwenye Hafla ya Utoaji Tuzo kwa Wadau wa Usuluhishi kwa mwaka 2025 iliyofanyika leo tarehe 19 Januari, 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.




















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni