Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, leo tarehe 19 Januari,
2026, amekabidhi Tuzo 26 kwa Wadau wa Usuluhishi baada ya kutambua mchango wao katika kuimarisha matumzi ya
usuluhishi kama njia mbadala ya utatuzi wa migogoro.
Hafla hiyo ya utoaji Tuzo
imefanyika kwenye Ukumbi wa Kilimanjaro wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania,
Naibu Wasajili na Mahakimu wa ngazi mbalimbali na Wadau kutoka Taasisi kadhaa
nchini.
Tuzo hizo zimeandaliwa na
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, kwa kutambua Wadau na Taasisi
mbalimbali nchini zinazochangia kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Waliokabidhiwa Tuzo hizo
ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili, Taasisi za Umma na
Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Halmashauri na Manispaa, Ofisi ya Ustawi wa
Jamii, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Taasisi za Fedha na Wasuluhishi Binafsi.
Utoaji wa Tuzo hizo
ulitanguliwa na makala maalum iliyoelezea safari na faida za usuluhishi na
kisha kufuatiwa na mada inayosema, ‘Haki kwa Haraka Mapema Ipasavyo; Hatua za
Suluhu kabla ya Kesi.’
Mada hiyo iliwasilishwa
na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Dkt. Abdallah
Gonzi na kujadiliwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara,
Mhe. Dkt. Cleophace Morris na Wadau mbalimbali kwa usimamizi wa Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliamani Laitaika.
Wadau mbalimbali walitoa
uzoefu wao kuhusu masuala ya usuluhishi, akiwemo Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha
Sheria Tanzania, Bw. George Mandepo, Wakili wa Kujitegemea, Msomi Mpaya Kamara
na Msuluhishi Binafsi, Bi. Medeline Kimei.
Wengine ni Msimamizi wa
Usuluhishi Malalamiko ya Bima, Bw. Zakaria Muyengi, Msajili wa Malalamiko ya
Bima, Bw. Jamal Mwasha na Msuluhishi Malalamiko ya Kibenki, Bw. Ramadhani
Mnyonga.
Hii ni mara ya tatu kwa Mahakama Kituo cha Usuluhishi kutoa Tuzo kama hizo kwa Wadau mbalimbali. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2024, ikafuatiwa na mwaka 2025.
Picha chini zinaonesha matukio kadhaa wakati wa utoaji wa Tuzo hizo.










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni