Jumatatu, 19 Januari 2026

MAHAKAMA YA TANZANIA KUENDELEA KUIMARISHA MATUMIZI YA USULUHISHI KATIKA UTATUZI WA MIGOGORO

  • Jaji Kiongozi akumbushia njia hiyo muhimu
  • Aonesha kukerwa na mapingamizi yanayolenga kuchelewesha haki

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Uwepo wa vyombo imara na huru vya utoaji haki ni njia mojawapo ya ulinzi wa amani na utulivu katika jamii yoyote inayoheshimu misingi ya utawala wa sheria, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amesema.

Akizungumza kwenye hafla ya utoaji Tuzo za Usuluhishi jijini Dar es Salaam leo tarehe 19 Januari, 2026, Mhe. Dkt. Siyani amebainisha kuwa Mahakama ya Tanzania imeendelea kuimarisha matumizi ya usuluhishi kama njia muhimu ya utatuzi wa migogoro.

‘Kwa upande wangu, naamini ni muhimu sana kuendelea kukumbushana juu ya hatua hizi na umuhimu wa usuluhishi katika utatuzi wa migogoro. Kufanya hivyo kutawezesha watu wengi zaidi katika jamii yetu na wale wanaokuja kuwekeza katika nchi yetu kuona fursa iliyopo kwenye usuluhishi,’ Jaji Kiongozi amesema.

Mhe. Dkt. Siyani amebainisha kuwa Ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba yaJamhuri ya Muungano wa Tanzania inaitaka Mahakama kukuza na kuendeleza usuluhishi wakati wa utekelezaji wa jukumu lake la msingi la utoaji haki.

Amesema kuwa licha ya kuwa ni matakwa ya kikatiba, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inazungumzia usuluhishi kama nyenzo muhimu ya kimkakati katika kujenga Taifa lenye uchumi shindani, jumuishi na imara.

‘Katika uchumi unaotegemea uwekezaji, ubunifu na kasi ya uzalishaji, usuluhishi unapunguza muda na gharama za migogoro ya kibiashara, hivyo kuweka mazingira salama na yenye uhakika kwa wawekezaji na wafanyabiashara,’ amesema.

Akizungumzia upande wa ustawi jamii, Jaji Kiongozi amebainisha kuwa, usuluhishi unachangia kulinda utu, kupunguza madhara ya migogoro ya kifamilia, kijamii, ajira na ardhi, na hivyo kuimarisha mshikamano wa kijamii.

Amesema pia kuwa usuluhishi ni njia inayotoa nafasi kwa wanawake, vijana na makundi maalum kushiriki katika kupata haki bila gharama kubwa au vikwazo vya kimuundo.

Kwa upande wa utawala bora, Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa usuluhishi unajenga imani ya wananchi kwa Taasisi za utoaji haki kwasababu unategemea uwazi, uadilifu na makubaliano.

‘Usuluhishi hupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani, huongeza ufanisi wa mfumo wa haki na huimarisha dhana ya uongozi unaozingatia ushirikishwaji na uwajibikaji.

Akizungumzia eneo la ushirikishwaji wa Wadau wa Usuluhishi, Jaji Kiongozi amesema kuwa  Mahakama imeendelea kushirikiana na Wadau wake katika kukuza na kuimarisha usuluhishi.

Amebainisha kuwa taarifa za mashauri yanayopitia usuluhishi mahakamani na nje ya Mahakama, pamoja na mkusanyiko wenye lengo la kutambua michango na mafanikio katika eneo la utoaji haki kupitia usuluhishi, ni ushuhuda wa kuimarika kwa ushirikishwaji wa Wadau.

‘Kupitia usuluhishi, Wadau wamefanikiwa kutatua migogoro mingi ikiwemo ile ya ardhi, biashara na ajira kwa kutumia njia za mazungumzo na maridhiano. Haya yote yanaashiria mtazamo mpya unaodhihirisha kwamba, migogoro haihitaji kusubiri mabishano mahakamani, hatua ndefu na za kiufundi zinazoweza kuwanyima watu haki, na matumizi ya gharama kubwa ili kupata hukumu,’ amesema.

Mhe. Dkt. Siyani ametoa rai, hasa kwa Aadau, Mawakili wasomi wote, wawe wa Serikali na, au binafsi, na hata wale walioruhusiwa kutoa msaada wa kisheria, kutoona mbinu za kiufundi, hasa kupitia mapingamizi ya awali kama njia rahisi ya kumaliza migogoro.

‘Ukweli ni kuwa mengi ya mapingamizi hayo, hayamalizi migogoro bali yanachelewesha mchakato wa haki. kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.

‘Badala yake, wasomi hawa na jamii kwa ujumla, sasa itambue umuhimu wa usuluhishi na kwamba migogoro yao inaweza kutatuliwa mapema, haraka na kwa njia inayolinda mahusiano ya kijamii na kiuchumi,’ amesema Jaji Kiongozi.

Wakati wa hafla hiyo, jumla ya Tuzo 26, ambazo zimeandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, zimetolewa kwa Wadau mbalimbali wa usuluhishi.

Wadau hao ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili, Taasisi za Umma na Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Halmashauri na Manispaa, Ofisi ya Ustawi wa Jamii, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Taasisi za Fedha na Wasuluhishi Binafsi.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani [juu na chini] akizungumza kwenye hafla ya utoaji tuzo za wadau wa usuluhishi leo tarehe 19 Januari, 2026 jijini Dar es Salaam.



Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania [juu na chini] wakiwa kwenye hafla hiyo.



Sehemu ya Viongozi na Wadau mbalimbali [juu na picha mbili chini] wakiwa kwenye hafla hiyo.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni