Jumatatu, 19 Januari 2026

UTOAJI TUZO JUKWA MUHIMU LA KUUNGANISHA MAHAKAMA, WADAU WA USULUHISHI; JAJI MARUMA

Na HALIMA MNETE-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama ya Tanzania itaendeelea kutambua mchango wa wadau mbalimbali wanaoshiriki katika kuimarisha matumzi ya usuluhishi kama nyenzo muhimu ya katika utoaji wa haki, ujenzi wa amani na utulivu wa kudumu katika jamii.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 19 Januari 2025 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, kwenye hafla ya utoaji Tuzo za Wadau wa Usuluhishi kwa mwaka 2025, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Maruma amesema tukio hilo ni jukwaa muhimu linalounganisha Mahakama na Wadau wake kwa lengo la kutafakari safari ya usuluhishi nchini, mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na mwelekeo wa kuimarisha zaidi utamaduni wa usuluhishi kama njia mbadala na endelevu ya utatuzi wa migogoro.

Ameeleza kuwa usuluhishi si dhana mpya, bali ni sehemu ya urithi wa kitamaduni wa Watanzania uliotumika tangu enzi za mababu, na kwamba utamaduni huo umepewa msisitizo wa kikatiba chini ya Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kutambuliwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama nguzo ya kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Mhe. Maruma amesema utoaji wa tuzo hizo ni njia ya Mahakama kuenzi na kutambua mchango wa dhati wa Wadau wa Usuluhishi, kuhamasisha maadili, weledi na mshikamano, pamoja na kuonyesha dhamira ya Mahakama ya Tanzania katika kujenga amani ya kudumu kupitia majadiliano, mazungumzo na vikao vya suluhu vinavyoongozwa kwa hekima na busara.

Ameongeza kuwa falsafa ya usuluhishi inalenga kubadili mtazamo wa jamii kwamba haki hupatikana mahakamani pekee, akisisitiza kuwa jamvi la usuluhishi huwezesha kupata haki ya kweli kwa kurejesha mahusiano, kuondoa uhasama na kujenga maridhiano ya kudumu.

Kauli mbiu ya Tuzo za Wadau wa Usuluhishi kwa mwaka huu, Kujenga Msingi na Kuimarisha Ushiriki wa Wadau kwa Matokeo Endelevu,” ambayo ina akisi kwa kina falsafa ya usuluhishi kama mwanzo wa kurejesha amani na mahusiano, badala ya kuwa mwisho wa migogoro.

Akizungumzia ushiriki wa Wadau, Mhe. Maruma amesema mafanikio yanayoonekana yametokana na mshikamano wa Wadau mbalimbali wakiwemo Majaji, Mahakimu, Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea, Viongozi wa Dini na Kimila, Wasuluhishi Binafsi pamoja na Taasisi zinazotekeleza usuluhishi kwa mujibu wa sheria.

Mgeni Rasmi wa hafla hiy alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapha Mohamed Siyani, ambaye alimwakilisha Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Siyani ameendelea kusisitiza kuwa usuluhishi si suala la hiari bali ni dhamira ya kikatiba, ambapo Mahakama kama chombo cha mwisho cha utoaji haki ina wajibu wa kukuza na kuendeleza mbinu za usuluhishi katika utatuzi wa migogoro.

Katika kuimarisha usuluhishi, hafla hiyo pia imeambatana na mdahalo wa kitaaluma wenye mada isemayo “Haki kwa Haraka, Mapema na Ipasavyo: Hatua za Suluhu Kabla ya Kesi,” iliyowasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Abdallah Gonzi, na kujadiliwa na wabobezi wa masuala ya usuluhishi kutoka ndani na nje ya Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, akizungumza kwenye hafla ya utoaji Tuzo za Wadau wa Usuluhishi. Picha chini ni Naibu Msajili wa Mahakama Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando.



Picha ya pamoja ya Watoa mada wakati wa hafla hiyo.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani [katikati waliokaa] ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji Wafawidhi wa Divisheni za Mahakama Kuu.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani [katikati waliokaa] ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu waliohudhuria hafla hiyo.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani [katikati waliokaa] ikiwa katika picha ya pamoja na Wachokoza mada kwenye hafla hiyo.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani [katikati waliokaa] ikiwa katika picha ya pamoja na Wadau mbalimbali.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani [katikati waliokaa] ikiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni