Alhamisi, 22 Januari 2026

MSAJILI MKUU AFUNGUA MAFUNZO KWA MAAFISA MIREJESHO KITUO CHA HUDUMA KWA MTEJA

Na. HABIBA MBARUKU & JAMES BUSANYA, Mahakama-Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya leo tarehe 22 Januari, 2026 amefungua mafunzo kwa Maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja katika Ukumbi wa Chumba Maalumu cha Mifumo ya Utoaji Taarifa (Judiciary Situation Room) kilichopo Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mhe. Nkya amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi wote wanaotekeleza majukumu yao katika Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania (Judiciary Customer Service Center zamani Judiciary Call Centre) katika matumizi ya mfumo ulioboreshwa wa mawasiliano na mteja, mfumo ambao ulianza kutumika katika toleo la kwanza ambao sasa umeboreshwa kwa kiwango kikubwa hadi kufikia toleo la nne.

Mhe. Nkya ameongeza kuwa maboresho hayo yametokana na uzoefu wa matumizi ya mfumo wa awali pamoja na tathmini ya mahitaji ya kiutendaji ili kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kwa wakati.

Maboresho haya yametokana na uzoefu wa matumizi ya mfumo wa awali pamoja na tathmini ya kina ya mahitaji ya kiutendaji kwa lengo la kuongeza ufanisi, ubora wa huduma na kurahisisha mawasiliano kati ya Mahakama na wananchi, amesema Mhe. Nkya

Aidha, Msajili Mkuu ameeleza kuwa, mfumo wa toleo la nne umeongezewa huduma mbalimbali ikiwemo kuunganishwa na WhatsApp Chatbot, hatua inayolenga kuisogeza Mahakama karibu zaidi na wananchi kwa kuwafikia kupitia majukwaa wanayotumia kwa wingi katika maisha ya kila siku.

Ameeleza kuwa tofauti na awali, mfumo huo sasa unaweza kutumika popote bila kuathiri utoaji wa huduma, hali itakayosaidia kuongeza ufanisi wa kazi na mwendelezo wa huduma kwa wananchi wakati wote.

Mhe. Nkya ameongeza kuwa, Maboresho mengine ni pamoja na uwezo wa watoa huduma kuwarudia wateja kwa kuwapigia simu moja kwa moja, kufanya ufuatiliaji wa masuala katika Mahakama yoyote nchini, pamoja na kuwa rafiki zaidi kwa mtumiaji kwa kupunguza makosa ya kibinadamu.

Vilevile, Mahakama imeimarisha upatikanaji wa huduma muda wote kwa kuanzisha Kituo cha Akiba cha Mfumo katika Mkoa wa Dar es Salaam, ili kuhakikisha huduma hazikatiki hata kunapojitokeza changamoto za kiufundi.

Sambamba na hayo Mhe. Nkya amesisitiza kuwa, baada ya mafunzo hayo, Mahakama inatarajia kuona ongezeko la ufanisi katika kushughulikia mawasiliano ya wananchi, matumizi sahihi ya takwimu katika kufanya maamuzi ya kiuendeshaji, pamoja na kuimarika kwa uwajibikaji na uwazi kwa watumishi.

Msajili Mkuu, ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa watakayoyapata kuboresha huduma, kuimarisha maadili ya kazi na kuendelea kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama.

Masajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya akizungumza wakati alipokuwa akifungua mafunzo kwa Maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, leo 22 Januari, 2026 katika Ukumbi wa Chumba Maalumu cha Mifumo ya Utoaji Taarifa (Judiciary Situation Room) kilichopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania  jijini Dodoma.

Naibu Msajili na Mkurugenzi wa Divisheni ya Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Mirejesho kwa Umma na Maadili, Mhe. Maira Kasonde akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Msajili Mkuu wa Mahakama ili kufungua mafunzo kwa Maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, leo 22, Januari, 2026 katika Chumba Maalumu cha Mifumo ya Utoaji Taarifa (Judiciary Situation Room) kilichopo Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja baada ya kufungua mafunzo kwa maafisa hao, katika Chumba Maalumu cha Mifumo ya Utoaji Taarifa (Judiciary Situation Room) Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma, wengine ni Naibu Msajili na Mkurugenzi wa Divisheni ya Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Mirejesho kwa umma na Maadili, Mhe. Maira Kasonde wa kwanza kulia.

Sehemu nyingine ya maafisa mirejesho wa kituo cha huduma kwa mteja wakiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe. Eva Nkya (wa kwanza kushoto) baada ya kufungua mafunzo kwa maafisa hayo katika Chumba Maalumu cha Mifumo ya Utoaji Taarifa (Judiciary Situation Room) Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma, (wa pili kushoto) ni Naibu Msajili na Mkurugenzi wa Divisheni ya Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Mirejesho kwa umma na Maadili, Mhe. Maira Kasonde.


Sehemu ya maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja wakifuatilia hotuba ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya.

Sehemu ya maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja wakifuatilia hotuba ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya.

Maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja wakisikiliza hotuba ya Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe. Eva Nkya (aliyesimama mbele) wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, leo 22 Januari, 2026 katika Chumba Maalumu cha Mifumo ya Utoaji Taarifa (Judiciary Situation Room) kilichopo Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Sehemu ya Maafisa Mirejesho wa Kituo cha Huduma kwa Mteja wakifuatilia hotuba ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (aliyesimama mbele)

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni