Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapema leo amewaapisha
Wasajili wa Mahakama ya Tanzania, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais amemuapisha Mhe.
Katarina Revocatti, kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. John
Kahyoza naye ameapishwa kuwa, Msajili wa Mahakama ya Rufani (T).
Kabla ya uteuzi wake, Mhe.
Revocatti alikuwa, Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), naye Mhe. Kahyoza alikuwa
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa upande, Msajili Mteule
wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Revocatti ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na
kuendeleza mapambano ya maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama ya
Tanzania.
“Mahakama ya Tanzania ipo
katika mipango mingi ya maboresho ambayo yote inalenga kuboresha huduma ya
utoaji haki nchini, hivyo ni jukumu langu kuhakikisha naendeleza mikakati yote
ya maboresho iliyopo ndani ya Mahakama,” alisema Mhe. Revocatti.
Aliongeza kuwa changamoto
iliyopo kwa upande wa jamii ni uelewa mdogo wa taratibu mbalimbali za
Kimahakama hivyo, amewataka wadau mbalimbali wa Mahakama na Sheria kwa ujumla
kusaidia katika kuelimisha wananchi juu ya taratibu mbalimbali za Kimahakama.
Aidha, Jaji Kiongozi wa
Mahakama ya Tanzania, naye amemuapisha, Mhe. Ilvin Mugeta kuwa Msajili,
Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye anashika nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. John
Kahyoza ambaye ameteuliwa kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani (T).
Kabla ya uteuzi wake, Mhe.
Mugeta alikuwa Mkurugenzi wa Maadili na Ukaguzi-Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni