Jumanne, 10 Novemba 2015

JAJI MKUU AKUTANA NA BALOZI MPYA WA SINGAPORE NCHINI.



    Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Mohamed Chande Othman alikutana leo ofisini kwake na Balozi mpya wa Singapore Nchini Mhe. Tan Puay Hiang. Katika mazungumzo yao Mhe. Balozi alimfahamisha Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania kuwa lengo la kumtembelea ni kujitambulisha kwake na kuona njia bora ya kujenga mahusiano kati ya Mihimili ya Mahakama ya Nchi hizo mbili. 

 
Mhe Tan Puy Hiang alimfahamisha Mhe. Jaji Mkuu kuwa, kati ya Singapore na Tanzania tangu enzi za ukoloni sheria zilizo nyingi zilitokana na Sheria za ukoloni wa Kiingereza.  ‘’Kama unavyojua Mhe.Jaji Mkuu Singapore ilikuwa chini ya himaya ya Kiingereza hivyo Sheria zetu nyingi zimetokana na Sheria za Kikoloni za Kiingereza na kuwa zinafafana na za kwenu’’ alisema Balozi Tan Puay Hiang.  Balozi Tan Puay Hiang alimueleza Mhe Jaji Mkuu maendeleo yaliyopatikana Nchini Singapore tangu uhuru katika sekta zote ikiwamo Mahakama.

 Mhe.Jaji Mkuu wa Tanzania alianza kwa kumshukuru Mhe.Balozi kwa kupata muda wa kumtembelea na kumuahidi kuendeleza uhusiano bora uliopo.Alimueleza kuwa, ujumbe wa Mahakama ya Tanzania ulitembelea Singapore mwaka huu ili kupata uzoefu katika masuala ya ufanisi wa Kazi za Mahakama, Mifumo ya uendeshaji wa Mashauri,matumizi ya teknolojia katika uendeshaji wa Mashauri ya Kimahakama.

 Kuhusu mfumo wa Mahakama Mhe.Mohamed Chande Othman alimueleza Mhe. Balozi huyo kuwa, mfumo wa Mahakama ya Tanzania unaanzia ngazi ya Mahakama ya Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani. Na katika Mahakama Kuu tuna vitengo vya Mahakama Kuu inayoshughulikia masuala ya Ardhi, Biashara, Kazi na kuwa kuna takribani Mawakili 4600 Nchi nzima.  ‘’Mhe.Balozi 70% ya mashauri hapa Tanzania yapo kwenye Mahakama za mwanzo na tuna karibu Mahakama 100 Nchi nzima’’ alifafanua Mhe.Jaji Mkuu.  

Alimueleza Mhe.Balozi kuwa, Mahakama iko katika maboresho yatakayosaidia kurahisisha uendeshaji wa mifumo ya Mashauri, na kuendesha mashauri kwa njia ya Tehama. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw.Hussein Kattanga, Mtendaji Mahakama Kuu Bw. Solanus Nyimbi, Msajili wa Mahakama Rufani Mhe.John Kahyoza na afisa toka Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa.
      

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni