JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAHAKAMA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mahakama
ya Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) imeandaa
mafunzo ya siku mbili kwa Waandishi wa Habari wanaoandika Habari za Mahakama
itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 25. Jaji Mkuu Mheshimiwa Mohamed Chande Othman anatarajiwa
kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mafunzo
haya kwa waandishi wa habari ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya Mahakama
Tanzania na tasnia ya habari chini ya uratibu wa MCT ulianza Desemba 03, 2014
ambapo ulifanyika mkutano mkubwa wa kwanza ambao kwa upande wa Mahakama ujumbe
wake uliongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman na
majaji wa mahakama kuu zaidi ya 30 huku ule wa tasinia ya habari ukiongozwa na
Rais wa MCT Mh. Jaji Thomas Mihayo (r) na watendaji wakuu wa vyombo vya habari
nchini.
Katika
mkutano huo ilikubaliwa kuimarishwa uhusiano baina ya taasisi hizi mbili ili
kuwahudumia vyema zaidi wananchi ikiwa ni pamoja na kuendesha mafunzo ya
kuwajengea uwezo waandishi wa habari vivyo, hivyo kuwajengea uelewa wafanyakazi
wa Mahakam kujua mazingira ya utendaji kazi wa tasinia ya habari kwa lengo la
kupunguza kutoelewana baina yao.
Mafunzo
haya ya siku mbili yana lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari za
mahakama kuzingatia maadili na weledi wa taaluma yao na utamadani wa mahakama
ili kuwafanya wananchi kujenga imani kwa taasisi hiyo yenye wajibu wa kutoa
haki kwa wananchi.
Kauli
mbiu ya Semina ni‘Uandishi wa Habari za Mahakama unaozingatia maadili, weledi na
utamaduni wa Mahakama’. Waandishi wapatao 60 kutoka vyombo vya habari
nchini yakiwemo magazeti, runinga na redio wanataraji kushiriki mafunzo hayo.
Mada
kadhaa zitatolewa ikiwa ni pamoja na misingi ya uandishi wa habari na
mawasiliano, muundo wa mahakama Tanzania, matumizi sahihi ya lugha za habari za
mahakama na uzoefu wa MCT katika kufuatilia habari za mahakamani. Aidha,
kutatolewa ushuhuda na waandishi nguli wa habari za makamani kuhusu tamu na
chungu.
Mafunzo
hayo ya siku mbili yataendeshwa na wabobezi wa sheria kutoka ofisi ya Jaji Mkuu
wa Tanzania, mawakili waliopata kuwa waandishi wa habari na wasomi wa
mawasiliano ya umma. Washiriki watatunukiwa vyeti vya kushiriki.
Walengwa
wa mafunzo hayo ni waandishi wa habari wanaoandika habari za Mahakama, wahariri,
waheshimiwa majaji, manaibu wasajili, na mahakimu wakazi wafawidhi wa mkoa wa
Dar Es Salaam.
Ni
matumaini ya Mahakama nchini na MCT kuwa baada ya mafunzo hayo uandishi wa
habari za mahakama utapata msukumo mpya na kwamba utakuwa bora zaidi kuliko
ilivyo sasa.
Imetolewa
na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni