Mhe.
Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (wa tatu kulia),
akimshukuru Rais Mhe. John Pombe Magufuli mbele ya Waziri wa fedha na Mipango Dkt.Philip
Mpango(wa pili kushoto) na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Harrison Mwakyembe(wa pili kulia), Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Catarina Revocatti (wa kwanza kushoto), na Msajili Mahakama ya Rufani, Mhe. John Kahyoza (wa kwanza kulia), kwa kuipatia Mahakama fedha Bilion Kumi na mbili na Milioni mia tatu ikiwa
ni kutimiza ahadi ya Rais aliyoahidi siku alipokuwa mgeni rasmi Siku ya Sheria
hapa nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango akizungumza juu ya matarajio ya Mhe. Rais baada ya kukabidhi fedha kwa
ajili ya maendeleo ya Mahakama ya Tanzania.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari
wakati wa kumshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kuwakabidhi fedha
alizoahidi, lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya Mahakama ili kuweza kutoa
na kutenda haki kwa wakati.
Waandishi
wa Habari waliohudhuria mkutano baina ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Waziri wa
Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa
kutimiza ahadi yake ya kuipatia Mahakama kiasi cha shilingi Bilioni 12.3 alizoahidi
wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4, 2016 jijini Dar es salaam.
Amesema Fedha hizo zitatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama na ujenzi wa Mahakama
mpya katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa shukrani hizo jijini Dar es salaam
Mhe.Othman amesema kuwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 Mahakama imepata
asilimia 100 ya fedha zote za Maendeleo zilizokasimiwa na Bunge kwenye Bajeti
yake ya mwaka 2015/2016.
Amesema
kupatikana kwa fedha hizo ambazo ni za Maendeleo kutasaidia kufufua
miradi ya ujenzi iliyosimama, kufufua Mahakama ambazo zilikua hazifanyi kazi
kwa sababu ya uchakavu na kuipatia Mahakama fursa zaidi ya kutoa huduma bora
kwa wananchi kwa kuwasogezea huduma za Haki karibu katika maeneo wanayoishi.
Mhe.Othman ameeleza kuwa kwa kipindi cha bajeti za
miaka 3 mfululizo kuanzia mwaka 2012 /2013 hadi 2014/2015 Mahakama ilikua ikipokea fedha pungufu ya
kiasi kilichopangwa katika Bajeti hali iliyochangia kuzorota kwa shughuli za
Mahakama.
" Kwa mara ya kwanza Mahakama tumepata asilimia
100 ya Bajeti yetu ya mwaka 2015/2016 kutoaka Serikalini, mwaka 2012/2013
tulipata shilingi bilioni 26.9 ikiwa ni pungufu ya bajeti yetu kwa asilimia 78,
mwaka 2013/2014 tukapata Bilioni 42.7 pungufu kwa asilimia 82 na mwaka
2014/2015 tulipewa shilingi bilioni 41.5
ambayo ni pungufu kwa asilimia 92 "
Akizungumzia miradi ya ujenzi wa majengo mapya ya
Mahakama amesema kuwa tayari Mahakama ina michoro ya ramani za majengo
yatakayojengwa katika maeneo mbalimbali ambayo hayakuwa na huduma hiyo ikiwemo
mikoa 12 kati ya 25 ambayo haina Mahakama Kuu, wilaya 22 kati ya 133 ambazo
hazina Mahakama za Wilaya pamoja na kuongeza Mahakama za Mwanzo ambazo ziko 976
kufikia kata zote 3,957.
Kuhusu Mradi wa
ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya
Mahakama utakaofanyika katika uwanja wa Chimala jijini Dar es salaam
amesema utahusisha maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za
Kimahakama na kuongeza kuwa Mahakama
itajenga jengo lenye viwango kwa
kuwatumia Wakandarasi na wataalam wa kitanzania watakaojenga Mahakama nzuri na yenye viwango kwa
gharama nafuu.
" Mahakama
tutatoa kipaumbele kwa wataalam wetu wa ndani ili waweze kutujengea Mahakama
zetu, tunalenga kuwafikishia huduma zetu katika maeneo wanayoishi tunao mfano mzuri wa Mahakama ya mwanzo ya
Dumila iliyoko Morogoro, Mahakama hii imejengwa kijijini ni ya kisasa" Amesisitiza Mhe.Othman.
Kwa upande wake
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Serikali
itaendelea kushirikiana na Mahakama ya
Tanzania ili kuwezesha ufanisi wa shughuli zake kwa kuhakikisha kuwa kiwango
cha fedha za Bajeti kinachopitishwa kwa ajili ya kuhudumia shughuli za Mahakama kinafika kwa wakati.
Akizungumzia kuhusu
uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi, amesema uanzishwaji wake uko katika hatua
nzuri na wakati ukifika wananchi watataarifiwa kama ilivyoahidiwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuungwa mkono na Mahakama ya Tanzania.
Naye Waziri wa Fedha
na Mipango Dkt. Philip Mpango,
akizungumzia fedha za Maendeleo zilizotolewa
na Mhe.Rais amesema kuwa lengo la ahadi ya Rais kwa Mahakama ilikua ni
kuhakikisha Haki inapatikana kwa wananchi kwa Wakati na kwamba miongoni mwa
vitu vilivyokua vikichelewesha haki kwa watanzania walio na mashauri Mahakamani
ni ukosefu wa fedha na uchakavu wa miundombinu.
Amesema Serikali
inaendelea kujenga uwezo ili kuimarisha utoaji wa huduma za katika mihimili
yote ikiwemo Bunge na Mahakama, msisitizo ukiwekwa katika kukusanya mapato
"Kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tuna dhamira ya dhati ya
kukusanya mapato ya ndani ili kujenga uwezo wa Serikali tutawabana wote
waliokuwa wanakwepa kulipa kodi na hili tutalisimamia kikamilifu"
Amesema utoaji wa
Haki ni moja ya ukuzaji wa maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa Mahakama ya
Tanzania inafanya kazi nzuri pamoja na ufinyu wa bajeti yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni