Mtendaji Mkuu wa
Mahakama Bw. Hussein Katanga (katikati) akisisitiza jambo wakati wa kikao cha
Mrejesho wa Wadau walioshiriki katika utoaji wa Elimu ya Sheria kwa wananchi
Februari 1 hadi 3, 2016 katika viwanja vya Mnazi mmoja, jijini Dar
es salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu Solanus Nyimbi na
Kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. John Lugalema
Kahyoza.
Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. John
Lugalema Kahyoza akizungumza na Wadau walioshiriki katika utoaji wa Elimu ya
Sheria kwa wananchi Februari 1 hadi 3, 2016 katika viwanja vya Mnazi
mmoja, jijini Dar es salaam.
Mahakama
ya Tanzania imesema kuwa inaendelea na mkakati wa kufanya maboresho ya
miundombinu yake ili kurahisisha utoaji wa huduma ya mahakama kwa
wadau na wananchi kwa wakati.
Kauli
hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Bw.
Hussein Katanga wakati wa kikao cha Mrejesho wa Wadau walioshiriki katika
utoaji wa Elimu ya Sheria kwa wananchi Februari 1 hadi 3 mwaka huu katika
viwanja vya Mnazi mmoja, jijini Dar es salaam.
Bw.
Katanga amewaambia wadau hao kuwa Mahakama ya Tanzania inaendelea kufanya
mabadiliko ya huduma zake kutokana na ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka
Serikalini pia kutoka kwa wadau wa Haki wanaoiwezesha Mahakama kufanya
maboresho hayo kwa lengo la kukuza Utoaji wa Haki nchini.
Amesema
kuwa ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi Mahakama
itatekeleza Mpango mkakati wa miaka 5 wa kuiwezesha kushirikiana kwa karibu
zaidi na wadau na Taasisi za utoaji Haki katika masuala yanayohusu shughuli za
kila siku za utendaji wa Mahakama.
“
Mahakama tutaanzisha mpango wa miaka 5 ambao utaanzisha mfumo wa wa
kushirikiana na wadau wetu kwa karibu katika mambo yanayohusu shughuli zetu ili
kuwaondolea wananchi usumbufu na upotevu wa muda pindi wanapofuatilia huduma”
Amesema.
Amefafanua
kuwa Mahakama imeshaanza kujenga majengo mapya ya Mahakama za Mwanzo katika
maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Kigamboni jijini Dar es salaam,
Kawe , Wilaya ya Mkuranga na Kibaha mkoani Pwani ili kurahisisha utoaji
wa Haki.
“
Mahakama sasa tuko katika mwelekeo mzuri wa kufanya mabadiliko, sasa kwa
kushirikiana na wataalam wetu wa ndani ikiwemo Chuo Kikuu Ardhi , tunaendelea
kujenga majengo mapya ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo
Mahakama ya Mwanzo Kigamboni, Mkuranga, Kibaha na Kawe ambazo hizi zitakamilika
ifikapo Juni mwaka huu” Amesisitiza.
Bw.
Katanga ameongeza kuwa mpango uliopo ni kuhakikisha kuwa majengo yaliyopo
yanakarabatiwa sanjali na ujenzi wa majengo mapya katika Mahakama zote 133 nchi
nzima.
Aidha,
amebainisha kuwa Mahakama inaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa watumishi
wake ikiwemo ununuzi wa mabasi ya kusafirishia watumishi, magari madogo na
Pikipiki ili kuwawesha watumishi wa Mahakama kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu Solanus Nyimbi akizungumza na wadau
hao amewataka wafanye kazi kwa kushirikiana katika kuwahudumia wananchi ili
kuongeza imani yao kwa Mahakama.
Amezitaka
Taasisi na wadau wanaohusika na utoaji wa Haki kujikita katika kushughulikia
matatizo ya wananchi ili kufanikisha dhana ya Utoaji Haki kwa Wakati ili kwenda
na mpango uliowekwa na Mahakama wa kuondoa mrundikano wa mashauri mahakamani na
ule wa kuzifuta kesi zilizokaa muda mrefu.
Naye
Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Lugalema Kahyoza ametoa wito kwa
Taasisi za Utoaji wa Haki kukutana mara kwa mara ili kujadili na kutatua
changamoto zinazoukabili Utoaji wa Haki nchini.
Washiriki wa kikao
cha Mrejesho wa Wadau walioshiriki katika utoaji wa Elimu ya Sheria kwa
wananchi Februari 1 hadi 3, 2016 katika viwanja vya Mnazi mmoja,
wakifuatilia kikao hicho jijini Dar es salaam.
Mmoja wa washiriki wa
kikao hicho akichangia mada.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni