Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania
(wa kwanza kushoto) akipata taarifa fupi ya Mahakama ya Tanzania Kanda ya
Songea kutoka kwa Mhe. John S.Mgetta Jaji Mfawidhi kanda ya Songea
(aliyesimama), mara baada ya kuwasili Mahakama Kuu kanda ya Songea.
Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania (kushoto) akipata taarifa fupi
kutoka kwa Bw. George M.Sabianus Afisa Tawala, wakati akiangalia
mazingira ya ofisi katika maktaba ya Mahakama Kuu Songea.
Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania
akipanda mti wa kumbukumbu katika Mahakama kuu Kanda ya Songea.
Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania
(wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja Majaji wa Mahakama Kuu songea, Msajili,
Mtendaji na Mahakimu wa Mahakama za Wilaya mbalimbali mara baada ya kupanda mti
wa kumbukumbu Mahakama Kuu kanda ya Songea.
Mhe. Hussein Katanga Mtendaji Mkuu Mahakama ya
Tanzania (mwenye koti la blue),Mhe. Katarina Revocatti, Msajili Mkuu Mahakama
ya Tanzania (wa tano kushoto) katika picha ya pamoja na Watendaji na Watumishi
wa Mahakama ya Tanzania wakati wa ziara
kanda ya Songea.
Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania
(katikati) Mhe. Hussein Katanga Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania (kulia) wakipata taarifa fupi ya
ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na wadau mbalimbali, vyombo vya usalama kutoka
kwa Mkuu wa Mkoa wa Songea Mhe. Said T. Mwambungu wakati wa ziara mkoani
Ruvuma.
Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania akiweka sahihi katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Mahakama ya Wilaya ya Songea.
Mahakama
ya Tanzania ni moja kati ya Taasisi iliyopo katika mchakato wa kuboresha huduma
zake. Katika kufanikisha azma hii jitihada/maboresho mbalimbali yameendelea kufanyika
ili kuwezesha Mhimili huu muhimu kuwa na mazingira rafiki ya utoaji haki kwa wananchi.
Hivi
karibuni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman alitembelea katika Mahakama
za mikoa ya Iringa, Njombe pamoja na Ruvuma, lengo la ziara ikiwa ni kukagua na
kujionea hali ya utendaji wa Mahakama na mwenendo wa uendeshaji wa mashauri.
Katika
ziara yake Mhe. Jaji Mkuu alipata nafasi ya kutembelea Mahakama Kuu Songea,
Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mahakama ya Wilaya Songea. Mahakama ya Wilaya
Mbinga, Mahakama ya Wilaya Nyasa inayotarajiwa kuanza kazi hivi karibuni na
baadhi ya Mahakama za Mwanzo.
Mhe.
Jaji Mkuu aliongozana na Watendaji wengine wa Mahakama katika ziara yake ambao ni;
Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Msajili Mkuu pamoja na Mtendaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania. Wote walipata fursa ya kujionea hali halisi ya miundo mbinu ya
Mahakama ikiwa ni pamoja na kupata taarifa za Mahakama hizo kutoka kwa Jaji Mfawidhi/Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hizo.
Akisoma
taarifa yake mbele ya Mhe. Jaji Mkuu, Mhe. John Mgetta, Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu Kanda ya Songea alisema kuwa Kanda yake ina Mahakama Kuu moja (1), Mahakama
ya Hakimu moja (1) ya Mahahakama za Wilaya tano (5) ambazo ni Songea, Namtumbo,
Tunduru, Mbinga na Mahakama ya Wilaya Nyasa.
Hata
hivyo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. John Mgetta alikiri Mahakama
yake kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi hususani Makarani na ubovu wa
majengo ya Mahakama, kwani hayatoshi na ni machakavu.
Mhe.
Jaji Mkuu, Kanda ya Songea inakabiliwa na uhaba wa watumishi, hususani makarani.
Ukiachia mbali changamoto hii tunakabiliwa pia na uchakavu wa miundombinu ya majengo.
“Mhe. Jaji Mkuu, majengo mengi yanayotumiwa na
baadhi ya Mahakama mfano Mahakama Hakimu Mkazi na Wilaya za Songea pamoja na
Mahakama nyingi za Mwanzo ni ya kuazima. kwa ujumla hali ya majengo ya Mahakama
katika Kanda hii si ya kuridhisha, Mahakama nyingi zina majengo mabovu sana,
hasa Mahakama za Mwanzo, ama yanahitaji ukarabati mkubwa au kubomolewa na
kujengwa upya,” alieleza Mhe. Jaji Mgetta.
Licha
ya kukabiliwa na changamoto kadhaa, Mahakama Kanda ya Songea ni moja ya Kanda
inayoongoza nchini kwa umalizaji wa Mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama
mkoani humo.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Tehama, Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba alisema kwa
mujibu wa Takwimu za uondoshaji wa Mashauri nchini, Kanda ya Songea ndio inayoongoza
kwa kasi kubwa ya kumaliza kwa wakati kesi zinazofunguliwa.
“Napenda
nikiri kuwa Kanda ya Songea ndio Kanda inayoongoza kwa uondoshaji wa Mashauri,
hii inatokana na jitihada zifanywazo na Majaji na Mahakimu wa Mahakama katika kanda
hiyo,” alisema Essaba.
Aliongeza
kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Songea ina jumla ya Majaji wawili tu na kuongeza kuwa
kila Jaji anawastani wa mzigo wa kazi (work load) wa kesi 215 kwa kila mmoja.
Alisema;
uwezo wao wa kumaliza mashauri yanayofunguliwa (clearance rate) ni 154% na kila
kesi iliyofunguliwa ilimalizika kwa wakati kwa asilimia 100% huku wakiendelea
kutoa maamuzi ya kesi za zamani kwa asilimia 54%.
Kwa
upande wa Mahakama ya Mkoa/Hakimu Mkazi, Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema Mahakama
hiyo haina kesi yenye Zaidi ya miezi 18 Mahakamani na kuongeza kuwa Mahakama hiyo
ina jumla ya Mahakimu wanne (4) wenye wastani wa mzigo wa kazi wa kesi 117 na uwezo
wao wa kuondoa mashauri yanayoingia ni asilimia 112, na kuongeza kuwa utendaji huu
unarudisha Imani ya Mahakama kwa wananchi.
Bw.
Essaba aliendelea kueleza juu ya utendaji wa Mahakama katika Kanda ya Songea, kwa
kuongeza kuwa kuna jumla ya Mahakama za Wilaya nne (4) Mahakama zote zikiwa na jumla
ya Mahakimu sita (6) na kila mmoja ana wastani wa mzigo wa kazi ‘workload’ wa kesi
186 na uwezo wao wa kuondoa kesi zinazofunguliwa ni asilimia 135 na kupelekea kumaliza
mlundikano wa mashauri katika Mahakama hizo.
Bw.
Essaba alimaliza kwa kuongelea juu ya Mahakama za Mwanzo zilizopo Kanda ya Songea
ambazo jumla yake ni 45 na kuongeza kuwa Mahakama hizo zina jumla ya Mahakimu
52 ambapo kila mmoja ana mzigo wa kazi wa kesi 157 na uwezo wao wa kuondoa kesi
zinazofunguliwa kwa Mahakama zote za Mwanzo ni 104.
“Hakuna
kesi/shauri lolote lililokaa kwenye Mahakama hizo zaidi ya mwaka mmoja, kwa ujumla
Kanda ya Songea ni moja ya kielelezo cha utendaji uliotukuka katika Mahakama ya
Tanzania,” alisisitiza Essaba.
Hata
hivyo; Mahakama ya Tanzania kwa ujumla wake ipo katika mchakato wa maboresho, ulioanza
muda wa takribani miaka mitatu sasa wa kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na
kuondosha mashauri ya muda mrefu Mahakama na kutoruhusu Mashauri kukaa Mahakamani
Zaidi ya miaka miwili (2).
Kwa
upande wake Mhe. Jaji Mkuu, aliupongeza uongozi wa Mahakama Kanda ya Songea kwa
jitihada zao za dhati katika kuhakikisha wanatoa haki kwa wakati, na kuongeza kuwa
hali hii inawapa Imani wananchi na kuifanya Mahakama kuwa kimbilio lao katika upatikanaji
wa haki.
Kwa
upande wao Watendaji walioambatana na Mhe. Jaji Mkuu katika ziara yake walisema
wamefarijika sana na kasi ya Kanda ya Songea kwa uondoshaji wa Mashauri na kudai
kuwa hali hii imesababisha hata idadi ya wafungwa/mahabusu gerezani kupungua.
“Binafsi
nimefarijika sana na mabadiliko tuliyoyaona Songea, idadi yawafungwa imepungua ghafla
na wananchi walio wengi wanaonekana kufurahia na kusifu jitihada hizi za Mahakama
mkoani Ruvuma,” alisema Mhe. Katarina Revokati, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania.
Pamoja
na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika kuboresha huduma za Mahakama nchini,
Mhe. Jaji Mkuu aliwasihi watumishi kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia misingi
na kanuni zilizowekwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni