Ijumaa, 1 Aprili 2016

KAMATI YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA YAKUTANA NA MHE.JAJI MKUU

Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania akimkaribisha mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama walipotembelea ofisini kwake.

Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria. Lengo likiwa ni kujitambulisha na kupata maelezo mafupi juu ya Mahakama ya Tanzania.



Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria yamtembelea ofisini kwake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Mohamed Chande Othman kwa lengo la kujitambulisha na kupata maelezo mafupi ya maendeleo ya Mahakama. Akiitambulisha Kamati hiyo kwa Mhe.Jaji Mkuu,Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe.Mohamed Mchengerwa alimueleza Mhe Jaji Mkuu kuwa, waliona ni vyema wakafika ofisini kwake na kupata taarifa fupi ya maendeleo ya Mahakama badala ya kukutana na watendaji wa Mahakama tuu. “Tuliona tukutembelee kujitambulisha na kupata taarifa fupi kuhusu maendeleo ya Mahakama’’ alisisitiza Mhe.Mchengerwa.

   Kwa upande wake,Mhe Jaji Mkuu aliwashukuru Kamati hiyo kumtembelea na kusema kuwa mahusiano yaliyopo kati ya Kamati na Mahakama ni ya kihistoria. ‘’Kama mnavyofahamu Kamati yenu ni kiungo muhimu kwa utekelezaji wa shughuli za kimahakama, imekuwa ikipitia miswada mingi ya sheria zilizopitwa na wakati ‘’ alisema Mhe.Jaji Mkuu.

     Jaji Mkuu wa Tanzania aliifahamisha Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kuwa, kwa miaka minne mfululizo hali ya utendaji wa Mahakama imeimarika baada ya kujiwekea mikakati ya kumaliza mashauri ya zamani. Hii imetokana na Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kujipangia kiwango cha kusikiliza mashauri kwa mwaka. ‘’ Kwa sasa, mfano kila Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo anatakiwa kusikiliza mashauri 260 kwa mwaka na wale wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mashauri 250’’ alisisitiza Jaji Mkuu.

   Kuhusu miundombinu Mhe.Jaji Mkuu alisema kuwa kwa muda mrefu Mahakama inasumbuliwa na tatizo la miundombinu inayorahisisha watu kupata haki. ‘’Nielize tuu kwa sasa kuna Mikoa 10 haina kabisa kanda ya Mahakama Kuu, na kuna Wilaya 22 hazina kabisa Mahakama za Wilaya hii inaathiri utoaji wa haki katika maeneo hayo’’ alisema Jaji Mkuu.

 Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria itakutana na Uongozi wa Mahakama ya Tanzania Jumamosi tarehe 9 Aprili 2016 kujadili taarifa ya maendeleo ya Mahakama.



Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria wakiwa katika mazungumzo na Mhe. Jaji Mkuu walipotembelea ofisini kwake kwa ajili ya kujtambulisha na kupata maelezo mafupi ‘brief notes’ juu ya Mahakama ya Tanzania.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani) walipozuru ofisini kwake. Pamoja na mambo mengi Mhe. Jaji Mkuu amewaeleza wajumbe hao kuwa Mahakama ya Tanzania ipo katika maboresho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumaliza kesi za muda mrefu Mahakamani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni