MHE. JAJI MKUU AFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI
MBEYA, AWATAKA WATUMISHI WA MAHAKAMA MKOANI HUMO KUFANYA KAZI YA UTOAJI HAKI
KWA UADILIFU.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman, amefanya ziara ya
kikazi ya kutembelea na kukagua shughuli za Mahakama katika Kanda ya Mbeya.
Ziara ya Mhe. Jaji Mkuu katika kanda hii imelenga kujionea hali ya
utendaji kazi wa Mahakama katika mkoa huo ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha
Watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kuboresha huduma
ya utoaji haki nchini.
Katika ziara yake Mhe. Jaji Mkuu aliambatana na Maafisa na Watendaji
kadhaa wa Mahakama kutoka Makao makuu ili kujionea hali ya utendaji kazi ikiwa
ni pamoja na kubainisha na kufanyia kazi changamoto ambazo watumishi
wanakumbana nazo katika utendaji kazi wa kila siku.
Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye alipata nafasi
ya kukagua na kuongea na Watumishi wa ngazi mbalimbali za Mahakama katika mkoa
huo.
Katika kikao alichofanya na Watumishi wa Mahakama mkoani humo ikiwa ni
pamoja na Wahe. Majaji na Mahakimu, Mhe. Jaji Mkuu alisisitiza mara zote juu ya
utendaji kazi kwa kujituma ili kubadili taswira ya Mahakama kwa wananchi ambao
ndio wadau muhimu wa Mahakama.
Akiongea na Watumishi wa Mahakama wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Jaji Mkuu
alieleza kufurahishwa na kasi ya usikilizaji na umalizwaji wa mashauri katika Mahakama
za Mwanzo mkoani humo.
Awali; katika taarifa yake kwa Mhe. Jaji Mkuu, Mhe. Noel Chocha, Jaji
Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, alimtaarifu Mhe. Jaji Mkuu juu ya
mkakati waliojiwekea wa kumaliza mashauri ya aina yoyote kwa kipindi
kisichozidi miezi sita.
Aidha Mhe. Jaji Mkuu alitumia ziara hiyo ya kikazi kuwaeleza Watumishi
juu ya mikakati ambayo Mahakama imejiwekea katika kuhakikisha kuwa huduma ya
utoaji haki inaboreshwa nchini.
“Kwa hivi sasa Mahakama ya Tanzania imejiwekea mikakati/vipaumbele
ambavyo vinalenga kuboresha huduma ya utoaji haki nchini, na malengo haya
inabidi yafanyiwe kazi na kila mmoja wetu kwa maana ya kila Mtumishi na mdau wa
Mahakama awajibike katika kufikia malengo yetu ya kuboresha huduma ya utoaji
haki nchini.” Alisema, Mhe. Jaji Mkuu.
Uimarishaji wa ukusanyaji wa takwimu; hili pia ni eneo ambalo limewekwa kama
kipaumbele katika maboresho Mahakamani, Mhe. Jaji Mkuu alisema Mahakama pia
imejipanga vyema kuhakikisha inakuwa na takwimu sahihi za kesi mbalimbali
zilizopo katika Mahakama mbalimbali nchini ili kuangalia ni sehemu ipi
inayohitaji nguvu zaidi katika kushughulikia mashauri/kesi za muda mrefu.
Uboreshaji wa Miundombinu: miundombinu hii ni pamoja na majengo ya
Mahakama, vitendea kazi n.k, Mhe. Jaji Mkuu alisema pia katika kuboresha huduma
zake Mahakama imejipanga katika kuboresha miundombinu yake ikiwa ni pamoja na
kujenga majengo ya Mahakama na kukarabati majengo yaliyochakaa.
“Tatizo kubwa ambalo Mahakama inakabiliana nalo ni uchakavu wa
miundombinu yake, kwa hili tuko mbioni kuhakikisha Mahakama inakuwa na
miundombinu bora zaidi, tumejipanga kuboresha ikiwa ni pamoja na kujenga Mahakama
Kuu katika mikoa yote ambao haina majengo, taratibu zinaendelea na kwa mwaka
huu tumepanga kuanza ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa ya Kigoma na
Musoma/Mara.
Uboreshaji wa hali ya Wafanyakazi wa Mahakama; Hili pia ni moja kati ya eneo ambalo limepewa
kipaumbele katika maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama; Mhe.
Jaji Mkuu aliwaeleza Watumishi wa Mahakama Mbeya kuwa uboreshaji huu unaangalia
upatikanaji wa stahili za Watumishi kwa wakati ikiwa ni pamoja na nauli za
likizo, madeni mbalimbali, uboreshaji wa mishahara ya watumishi suala ambalo
linaendelea kufanyiwa kazi.
Aidha Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa suala Maadili na nidhamu pia
limewekewa kipaumbele, alisema kuwa kuna baadhi ya Watumishi wa Mahakama hawana
nidhamu na maadili katika utendaji kazi, hali hii imesababisha kuwa Mahakama
nzima kutupiwa lawana juu ya utendaji kazi wake.
“kuna baadhi ya Watumishi ya watumishi wa Mahakama hawana maadili na
nidhamu hali hii inachafua taswira nzima ya Mahakama, lazima tuongeze uadilifu,
Watanzania wanataka Watumishi wanaotoa haki, wanaoaminika ili kila mwananchi
aridhike,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni