Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Mohamed Chande Othman akisaini kitabu cha wageni alipowasili kwenye Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Magesa Mulongo (wa pili kushoto), na wa kwanza kushoto
ni Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Mwanza Mhe. Robert Makaramba, kulia ni Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Musoma (RAS) Mhe. Eldan Anyosisye.
Mkuu wa Mkoa wa Mara
Mhe. Magesa Mulongo akimkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman katika Mkoa Mara.
Mahakama ya Tanzania inakusudia
kuanzisha Mahakama Kuu katika mkoa wa Mara ambapo ujenzi wa jengo la mahakama hiyo
unatarajiwa kuanza wakati wowote mwaka huu.
Akizungumza mjini Musoma
katika ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za kimahakama katika kanda ya Mwanza, Jaji
Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman alisema mkoa wa Mara unayo haki
ya kuwa na Mahakama Kuu kwa kuwa nia ya Mahakama ni kusogeza huduma karibu
zaidi na wananchi.
Alisema mahakama hiyo
itajengwa kwa haraka na itamalizika katika kipindi cha mwaka moja kwa kuwa fedha
kwa ajili ya ujenzi huo tayari imeshatengwa ambapo nyingine imetokana na msaada
waliopewa kutoka Benki ya Dunia.
Alisema kuanzishwa kwa
mahakama hiyo katika Mkoa wa Mara kutawapa fursa wananchi wa Mara ya kupata
huduma kwa karibu zaidi na pia itasaidia kupunguza kesi zilizoko mahakamani kwa
haraka.
Awali akimkaribisha Jaji
Mkuu ofisini kwake alipomtembelea, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo
alimwomba Jaji Mkuu kuanzisha Mahakama Kuu katika mkoa wake kwa kuwa asilimia
55 ya kesi zote za mauaji katika Mahakama kuu kanda ya Mwanza zinatoka katika mkoa
wa Mara hivyo mkoa huo unayo haki ya kuwa na Mahakama Kuu.
Pamoja na mkoa huo kuwa na
kesi nyingi za mauaji, Mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa wa Mara pia unakabiliwa
na kesi nyingi zinazohusu masuala ya ardhi kwa kuwa ni asilimia 38.3 tu ya eneo
zima la mkoa huo ndiyo eneo linalotuwa kwa ajili ya makazi ya watu na shughuli
za maendeleo
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu
na Makazi ya mwaka 2012, Mkoa wa Mara una wakazi zaidi ya milioni 1.3.
Alisema Mkoa wa Mara una
eneo lenye kilometa za mraba 30,150 ambapo asilimia 36 ya eneo hilo ni maji wakati
asilimia 25.7 ni eneo lenye mapori na hifadhi za Taifa ikiwemo mbugaya wanyama
ya Serengeti.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa
aliisifu Mahakama ya Tanzania kwa kufanya kazi yake kwa weledi ya kuzimaliza kesi
zilizohusu mapigano ya koo zilizokuwepo katika siku za nyuma mkoani humo kwa kuwa
zimesaidia maeneo ya mkoa huo kuwa salama hivi sasa na hayaonyeshi dalili za
kujirudia. Aliongeza kuwa eneo la haki likitulia hata masuala ya utawala yakuwa
rahisi.
Jaji mkuu Leo amehitimisha
ziara yake katika kanda ya Mwanza yenye mikoa ya Mara, Geita na Mwanza ambapo
alikuwa akikagua shughuli mbalimbali za kimahakama katika kanda hiyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Mohamed Chande Othman akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mkoa wa Mara wakati akikagua shughuli za Kimahakama Mkoa wa Mara.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Mohamed Chande Othman akikagua kiwanja kitakachotumika kujenga Mahakama
Kuu mkoani Mara.
Baadhi ya Watumishi wa
Mahakama za Mkoa wa Mara wakimsikiliza Jaji Mkuu ambaye hayupo pichani
alipozungumza nao mjini Musoma.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Mohamed Chande Othman (katikati) katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi
Kanda ya Mwanza, Naibu Msajili na Mahakimu wa Mkoa wa Mara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni