Mahakama ya Tanzania inakusudia
kuongeza idadi ya Majaji katika kanda yake ya Mwanza ili kuongeza msukumo wa
kumaliza kesi za mauaji kutokana na kanda hiyo kuongoza kwa kuwa na kesi nyingi
za mauaji nchini.
Akizungumza wakati wa ziara
yake ya kukagua shughuli za kimahakama katika kanda ya Mwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Mohamed Chande Othman amesema ataongeza idadi ya majaji katika kanda hiyo
ili kesi hizo za mauaji zimalizike kwa wakati.
Jaji
Mkuu akizungumza na Majaji wa Kanda ya Mwanza alipotembelea Mahakama Kuu
Mwanza.
Jaji Mkuu pia ameiagiza Mahakama
Kuu Kanda ya Mwanza kuzipa msukumo maalum kesi za mauaji ili kuhakikisha
zinamalizika mapema na kupunguza mlundikano wa kesi katika mahakama za
Tanzania.
Awali akisoma taaarifa ya
hali halisi ya kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Mfawidhi wa kanda
hiyo Mhe. Robert Makaramba alisema kanda ya Mwanza ndiyo inayoongoza kwa kuwa
na kesi nyingi za mauaji nchini ambapo hadi kufikia Aprili mwaka huu kuna jumla
ya kesi 512 za mauaji.
Pamoja na mkakati wa Jaji
Mkuu kuongeza idadi ya majaji ili kumaliza kesi hizo, Jaji Mfawidhi wa kanda
hiyo alisema wameshachambua kesi hizo za mauaji ambapo Jaji Kiongozi Mhe.
Shaban Lila pia aliahidi kuwaongezea jumla ya majaji 11 ili waweze kusaidia
kusukuma kesi hizo.
Jaji Makaramba alisema kati
ya mwezi Juni na Julai jumla ya vikao 11 vinatarajiwa kukaa ili kusikiliza kesi
123 zilizopangwa kusikilizwa. Alisema kati ya kesi hizo, 35 ni zile
zitakazosikilizwa kwa mara ya kwanza na kesi 88 ni zile zitakazosikilizwa mpaka
mwisho.
Alisema endapo vikao hivyo
vitafanyika kama ilivyokusudiwa vitasaidia kupunguza kesi zilizopo mahakamani
kwa miaka mingi.
Hadi kufikia mwezi April
mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ina jumla ya kesi 2771 za aina zote
zikiwemo zile za madai ya kawaida, madai ya Ardhi na za jinai. Ili kuongeza
kasi ya usikilizwaji wa kesi hizo, kila Jaji amepangiwa kusikiliza kesi 346.
Kanda hiyo ina Majaji nane (8).
Jaji Mkuu wa Tanzania
ameanza ziara katika Kanda ya Mwanza inayohusisha mikoa ya Geita, Mwanza na
Mara ambapo atakagua shughuli mbalimbali za kimahakama katika kanda hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni