Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman (katikati), Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza Mhe. Robert Makaramba (kushoto), Naibu Msajili wa Mwanza Mhe. Eugenia Rujwahuka (kulia), wakiwa kwenye mkutano na watumishi wa Mahakama wa Mkoa wa Geita.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman amezitaka Mahakama za mkoa wa Geita kuhakikisha zinamaliza kesi kwa
wakati ili kutekeleza lengo lililowekwa na Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza na watumishi wa Mahakama jana mkoani Geita,
Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania ilijiwekea malengo ya kumaliza kesi
katika mahakama zake kwa wakati kulingana na aina ya mahakama.
Alisema kwa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya
pamoja na Mahakama za Mwanzo lengo lilikuwa
ni kumaliza kesi zote ndani ya mwaka mmoja ili kuwafanya wananchi kuendelea
kuwa na imani na mahakama zao kwa kuwa ni zaidi ya asilimia 90 ya wananchi
wanahudumiwa na mahakama hizo.
Jaji Mkuu alisema kwa Mahakama za Mwanzo ambazo ziko 970
nchini kote lengo lilikuwa ni kuhakikisha hazikai na kesi kwa zaidi ya miezi
sita kwa kuwa ndizo Mahakama zinazohudumia wananchi wengi zaidi.
Alisema ili kuziwezesha Mahakama kutekeleza lengo walilojiwekea,
tayari Mahakama ya Tanzania imeajiri Mahakimu wapya 107 ambao watasambazwa kwenye
Mahakama zote za Mwanzo nchini kwa ajili yakwendakutoa huduma ya msingi ya
mahakama ya kutenda haki kwa wananchi wa Tanzania.
Akizungumzia suala la utoaji wa nakala za hukumu, Jaji
Mkuu amezitaka Mahakama za mkoa wa Geita kutoa nakala hizo mapema iwezekanavyo
ili kutoa haki ya kukata rufaa kwa wananchi ambao hawakuridhishwa na hukumu
walizopewa katika kesi zao.
Alisema Mahakama ya Tanzania itaongeza idadi ya Makatibu
Mahususi na kuongeza vifaa katika Mahakama zake ili kuongeza kasi ya uchapaji
wa nakala za hukumu. Alisema asilimia 80 ya bajeti inayotolewa kwa muhimili huo
imetengwa kwa ajili ya kuendesha kesi katika mahakama za Mwanzo, Wilaya na zile
za Hakimu Mkazi.
Jaji Mkuu anaendelea na zaira yake katika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza ambapo anatembelea mikoa Mwanza, Geita na Mara ili kukagua shughuli za kimahakama katika kanda hiyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akipanda mti kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita wakati wa ziara ya kukagua shughuli za Kimahakama katika Kanda ya Mwanza.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akimwagilia mti
baada ya kuupanda kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita wakati wa ziara ya kukagua
shughuli za Kimahakama katika Kanda ya Mwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni