Jumapili, 26 Juni 2016

WATUMISHI WA MAHAKAMA YA TANZANIA MKOANI LINDI WATAKIWA KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI

Watumishi wa Mahakama wa mkoa wa Lindi wakiwa kwenye Mafunzo kuhusu upatikanaji wa Taarifa na Mbinu za Kuhudumia wateja yaliyoandaliwa na  Mahakama ya Tanzania kwa Kushirikiana na Taasisi ya Vyombo vya Habari kusini mwa Afrika (MISA-TANZANIA). Mafunzo haya yanafanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Watumishi wa mahakama mkoa wa Lindi waliohudhuria mafunzo kuhusu upatikanaji wa taarifa na mbinu za kuhudumia wateja wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa Afrika (MISA- TANZANIA) ambaye pia ni mkufunzi wa mafunzo hayo Simon Berege( katikati) katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania waliopo katika mkoa wa Lindi wametakiwa kuboresha huduma zao kwa wananchi ili kuhakikusha taswira ya muhimili huo wa nchi inakuwa nzuri wakati wote.

Akifungua mafunzo ya siku mbili kwa watumishi wa mahakama mkoa wa Lindi  kuhusu upatikanaji wa taarifa na mbinu za kuhudumia wateja kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Mtwara, Afisa Tawala Amata Kinyenya aliwaambia watumishi hao kuwa, Mahakama haina budi kuwa na taswira chanya wakati wote ili iweze kutenda haki.
Alisema mazungumzo hayo ni muhimu kwa watumishi wa Mahakama kwa kuwa yanalenga kuimarisha utendaji kazi hasa katika kuwahudumia wateja wake ambao ni wananchi wanaofika kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma za kimahakama.

Afisa Tawala huyo alisema Mahakama ya Tanzania imeamua kuanza kutoa mafunzo hayo kwa watumisho wa ndani ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwani endapo watumishi hawatatoa huduma ipasavyo mtazamo wa Mahakama utakuwa ni hasi kwa jamii.

Aidha, mafunzo hayo ya siku mbili yanajumuisha watumishi wa Mahakama zaidi ya 30 kutoka katika Wilaya zote za Mkoa wa Lindi ambazo ni Nachingwea, Liwale, Ruangwa, Kilwa na Lindi mjini.

Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi na Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TANZANIA) imekuwa ikitoa mafunzo kuhusu upatikanaji wa taarifa na mbinu za kuhudumia wateja kwa watumishi wa kada mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania katika mikoa mbalimbali nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni