Jumatano, 24 Agosti 2016

MAHAKAMA YA ARDHI NA MIKAKATI YA KUONDOSHA MASHAURI YA MUDA MREFU



Na Mary Gwera
Mahakama ya Tanzania
‘Ardhi ni mali, ardhi ni uhai, ardhi ni uchumi,’ haya ni maneno yaliyosemwa na Mhe. Gad Mjemmas aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa migogoro ya ardhi inazidi kushika kasi kila kukicha.

Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa ardhi kwa maana ya kuwa na madini ndani yake, matumizi ya barabara, nyumba na miundombinu mingine kumekuwa na uhitaji mkubwa wa ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama kilimo, ujenzi na kadhalika.

Mhe. Jaji Mjemmas anaendelea kufafanua kuwa kufuatia migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiongezeka kila kukicha, Serikali iliona kuna haja/umuhimu wa kuundwa Tume ya Shivji iliyokuwa ikitambulika kama ‘Presidential Commission of Inquiry into Land Matters’ lengo la Tume hii ilikuwa ni kuja na mikakati ya jinsi gani ya kutatua migogoro ya ardhi.

Pamoja na mikakati mingi waliyokuja nayo, Tume hii pia ilipendekeza ianzishwe Divisheni maalum ya Mahakama kwa ajili ya kushughulikia mashauri ya ardhi, yaanzishwe pia Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya pamoja na vijiji hii yote ililenga katika kutatua migogoro ya ardhi.

Hata hivyo; Mhe. Jaji Mjemmas aliongeza kuwa kufuatia ongezeko la mashauri na changamoto mbalimbali, Mhe. Jaji Mkuu alitoa waraka wa kuruhusu kesi za ardhi kusikilizwa na Jaji yeyote wa Mahakama Kuu ili kuweza kupunguza msongamano wa mashauri.

Jaji Mfawidhi huyo, aliainisha mikakati mbalimbali ambayo Mahakama ya Ardhi imejiwekea katika kuondoa mlundikano wa mashauri katika Mahakama hiyo.

”Mpaka kufikia mwaka jana 2015, divisheni hii ya ardhi ilikuwa na mashauri yenye umri kati ya miaka mitano (5) hadi kumi (10) 526, hivyo katika hili sisi Majaji 9 wa Mahakama ya ardhi pamoja na Wasajili tulijiwekea mikakati thabiti ya kufikia lengo la kumaliza mlundikano huu,” alisema Jaji Mjemmas.

Kuainisha matatizo ya kesi hizo: Katika hili Mhe. Mjemmas, alisema waliainisha matatizo ya kesi  hizo kwa kuchambua jalada kwa jalada ili kujua nini tatizo la kila kesi, pia walifanya uhakiki wa majalada (stock taking) kujua jala husika lipo kwa nani na kuwashirikisha Mawakili kujitoa ili kuweza kufanikisha  zoezi la kumaliza mashauri hayo.
Mhe. Jaji Gad Mjemmas, aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu- Divisheni ya Ardhi (katikati), Mhe. Frank Mahimbali, Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi (kushoto) na Bw. Leonard Magacha, Mtendaji, Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi wakiwa katika kikao pamoja na wadau wa Mahakama, lengo likiwa ni kupata maoni ya pamoja ya kuboresha huduma, katika kikao hicho walikubaliana kushirikiana kwa kufanya kazi kwa pamoja kuondoa kero mbalimbali.
 Mmoja wa wadau wa Mahakama (Mawakili) akieleza jambo katika kikao maalum kati ya Mahakama ya Ardhi pamoja na wadau wake (Mawakili, wadaawa n.k), kikao hicho kililenga katika kuainisha changamoto zilizopo katika usikilizaji wa Mashauri ya ardhi na mikakati ya kuzitatua ili kuondokana na mlundikano wa mashauri ya ardhi.
Kuandaa vikao maalum ‘special session’; “ili kuweza kujikita katika kushughulikia mashauri haya, tuliandaa vikao maalum kuanzia Machi 16, 2015 hadi Aprili 30, 2015 lengo ili kufikia malengo tuliyojiwekea ya kumaliza mlundikano wa mashauri,” alifafanua, Jaji Mjemmas.

Kuendelea kuwatumia Majaji kutoka nje ya Kituo; Katika hili Mhe. Jaji Mjemmas anaendelea kueleza kuwa, ili kuongeza nguvu na kasi ya kumaliza mashauri haya, Mahakama hii iliwatumia Majaji kutoka katika Mahakama nyingine ili kuongeza kasi ya kumaliza mashauri hayo.

Kujitolea kufanya kazi muda wa ziada: ili kuweza kufanikisha zoezi hili, Majaji walijitoa kwa kufanya kazi  muda wa ziada  kwa kushirikiana na Mawakili ili kuwezesha kufanikisha zoezi hili.

Kufuatia kujitoa kwa dhati kwa Wahe. Majaji, walifanikiwa kumaliza kesi 216 kati ya 526 kufikia Mei, mwezi mmoja baada ya kuanza kwa zoezi hilo la kumaliza mashauri ya muda mrefu.
Kwa upande wake, Mhe. Frank Mahimbali, Msajili ya Mahakama ya Ardhi, anaeleza kuwa  kwa mwaka jana jumla ya mashauri 1602 yalifunguliwa katika Mahakama hiyo, na kuongeza kuwa kila Jaji alikuwa na wastani wa usikilizaji wa mashauri 177.
“Mahakama hii ina jumla ya Majaji 9, kufuatia idadi hii kila Jaji alikuwa na wastani wa usikilizaji wa kesi 177,” alisema Mhe. Mahimbali.
Hata hivyo, Mhe. Mahimbali alisema kuwa kasi ya ufunguaji wa Mashauri imekuwa ikiongezeka sambasamba na usikilizaji wake akitolea mfano kuwa kwa mwaka huu, Januari mpaka Machi jumla ya mashauri ya ardhi 404 yalifunguliwa  na kuongeza kuwa hadi kufikia Aprili jumla ya mashauri 392 yalisikilizwa.
“Kwa mwaka huu Januari hadi Machi jumla ya mashauri 404 yalifunguliwa yaliyosikilizwa ni 392, kasi ya usikilizaji wa mashauri imeongezeka maradufu, ari ya usikilizaji mashauri kwa Wahe. Majaji imepanda,” alisema Mhe. Mahimbali. 

Kwa upande wake Bw. Machumu Essaba, Mkurugenzi Msaidizi Tehama, anasema kuwa kwa mwaka jana kwa mujibu wa takwimu, Mahakama Kuu zote nchini zilikuwa na wastani wa kusikiliza na kuamua mashauri mbalimbali ya ardhi kwa asilimia 125 ikiwa na maana kwamba Mahakama Kuu zote nchini zina uwezo wa kusikiliza na kuamua mashauri ya ardhi yanayofunguliwa kwa asilimia 100 na kutolea maamuzi kwa yaliyokuwepo kwa asilimia 25.
“Kanda iliyoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha kuondoa mashauri yaliyofunguliwa ni Bukoba, Songea, Dodoma, Moshi, Sumbawanga.
Nyingine ni Tanga, Dar es Salaam, Iringa, Arusha, Tabora, Mtwara, Mbeya, Mwanza na Shinyanga.
Hata hivyo; Kanda iliyoongoza kwa kuondosha mashauri ya ardhi ni Bukoba ambayo ilikuwa na kiwango cha juu cha umalizaji `mashauri 226 ikiwa na jumla ya Majaji 4, Songea mashauri 176 Majaji 2, na Dodoma mashauri 164 Majaji 4.
Mkurugenzi huyo Msaidizi alipongeza jitihada zinazofanywa na Waheshimiwa Majaji katika kuondosha mashauri hayo ya ardhi, na kuongeza kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga inaonekana kuwa chini kwa kuondosha mashauri kwa sababu imeanza kazi mwishoni mwa mwaka jana. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni