Jumanne, 2 Agosti 2016

MAHAKAMA YAPANIA KUBORESHA HUDUMA KUPITIA MPANGO MKAKATI WAKE



Na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania
Mahakama ya Tanzania imeanza maboresho ya huduma zake kwa kujenga uelewa wa pamoja kwa watumishi na wadau wake walioko mikoani ili kuweza kuutekeleza Mpango Mkakati wake.

Hivi karibuni baadhi ya watumishi wa Mahakama walikutana mjini Dodoma na kuandaa Mpango Mkakati wa miaka mitano ambao utakuwa ndiyo msingi wa mabadiliko na maboresho katika sekta hiyo muhimu ya utoaji wa haki nchini. 

Kufuatia maandalizi ya mpango Mkakati huo, hivi sasa Maafisa wa Mahakama walioshiriki kuandaa Mpango Mkakati wapo katika Kanda mbalimbali za Mahakama nchini wakitoa elimu juu ya Mpango Mkakati huo. 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Nurdin Ndimbe, kiu kubwa ya wananchi wengi ni kupata huduma bora, hivyo kazi inayofanyika kwa sasa ni kujenga uelewa wa pamoja kwa watumishi na wadau ili kutekeleza majukumu kama kitu kimoja na hivyo kukidhi mahitaji ya wananchi ambao ndio wateja wakuu wa Mahakama.

“Kwa sasa timu ya Maafisa wa Mahakama wanatoa elimu ya Mpango Mkakati huu wenye mipango dhabiti yenye lengo la kubadili taswira ya Mahakama hususani katika utoaji wa huduma zake” alisema Bw. Ndimbe.

Bw. Ndimbe anaongeza kuwa katika Mpango Mkakati huo wa miaka mitano 2015/2016-2019/2020 una nguzo kuu tatu, ambazo  ni Utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali,  Upatikanaji na utoaji haki kwa wakati na Kurejesha imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Mawasiliano anaendelea kufafanua kuwa kazi inayofanyika kwa sasa kati ya nguzo hizo ni kushirikisha watumishi pamoja na wadau mbalimbali wa Mahakama juu ya Mkakati huo ili kuwa na uelewa wa pamoja katika uetekelezaji wake.

Alifafanua zaidi kuwa katika nguzo hii ya tatu ya Kurejesha imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau inalenga katika kuweka mfumo wa utoaji haki sawa kwa wote wenye kuaminiwa na jamii.

Mbali ya utoaji elimu, Bw. Ndimbe amefafanua zaidi kuwa Maafisa hao pia wamepata fursa ya kugawa mabango, vipeperushi, vijitabu pamoja na simu kwa Mahakama mbalimbali pamoja na ofisi za Wakuu wa mikoa, vyenye jumbe za kudhibiti ukiukwaji wa taratibu za Mahakama, hususan  kudhibiti vitendo vya rushwa.

“Tumepata nafasi ya kukabidhi vifaa tofautitofauti kwa Mahakama zetu zenye jumbe tofauti za kudhibiti vitendo vya rushwa pamoja na tabia nyingine zisizofaa ambazo zipo kinyume na maadili ya Mahakama, katika  mabango hayo zimewekwa namba mbalimbali za simu za kila mkoa zitakazowawezesha wananchi kutoa malalamiko na maoni yao” alifafanua.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni