Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman , akionesha nakala ya
kitabu cha Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) wa Mahakama ya Tanzania,
alipokuwa katika Mkutano kati yake na Waandishi wa Habari uliofanyika mapema
leo katika Ofisi za Mahakama ya Rufani (T), lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kutoa
taarifa juu ya uzinduzi rasmi wa Mpango huo utakaofanywa na Waziri Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Kassim M. Majaliwa kwa niaba ya Mhe. Rais, mnamo tarehe
21.09.2016, katika jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali,
kulia ni Mhe. Katarina Revocati, Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Jaji Mkuu akiwa na Waandishi wa
Habari katika Mkutano huo.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa
katika Mkutano huo ambapo Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania alikuwa akitoa taarifa juu
ya uzinduzi wa Mpango Mkakati huo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari walioshiriki katika
Mkutano huo, miongoni mwa mambo aliongelea ni pamoja na uzinduzi rasmi wa Mradi
wa Maboresho wa huduma utakaotekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB).
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa
kazini.
Aidha; Mhe.Jaji Mkuu
alizungumzia juu ya Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama, ambao ni mradi
shirikishi baina ya Serikali, Mahakama ya Tanzania pamoja na Benki ya Dunia
(WB).
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim M. Majaliwa keshokutwa Septemba
21, mwaka huu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano 2015/16- 2019/20 wa Mahakama
ya Tanzania wenye lengo la kuboresha huduma zake na kuzisogeza karibu
na wananchi ili wazifikie kwa urahisi.
Kauli hiyo ilitolewa leo tarehe 19 Septemba,
2016 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Mohamed
Chande Othman, wakati akizungumza
na waandishi wa habari leo katika Ukumbi wa maktaba ya Mahakama ya Rufani(T),
ambapo amesema Waziri Mkuu huyo
atazindua mpango huo, kwa niaba ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Mafuguli.
Jaji Mkuu alisema uzinduzi
huo utafanyika jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, lililopo barabara
ya Magereza jirani na ofisi za halmashauri ya Mji wa Kibaha kuanzia saa 2.00
asubuhi. Mpango Mkakati huu ni matokeo ya tafiti
mbalimbali zilizofanywa na Mahakama na wadau wake na kutoa mapendekezo ya
kuboresha utoaji wa huduma.
Mapendekezo
hayo ni pamoja na kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa
rasilimali, kuwezesha upatikanaji na utoaji wa haki kwa wakati na kurejesha
imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama na upatikanaji
wa haki kwa makundi maalum ya wahitaji kama vile watoto, walemavu na wanawake.
Kupitia
Mpango Mkakati utakaozinduliwa, Mahakama imejipanga kuendelea kuleta mabadiliko
makubwa ya utendaji ndani ya miaka 5 ijayo (2015/16-2019/20) katika utoaji
huduma zenye viwango na weledi wa hali ya juu kwa kuongozwa na Dira“Haki
sawa kwa wote na kwa wakati”.
Aliongeza kwamba asilimia 47 ya Watanzania bado
hawajafikiwa na huduma za Mahakama Kuu nchini. Hivyo asilimia hiyo ni sawa na
idadi ya watu milioni 21, katika kuhakikisha wananchi hao wanafikiwa Serikali
na Mahakama imewekeza nguvu ya
rasilimali fedha ili kuhakikisha kuwa huduma ya utoaji haki inamfikia kila
mwananchi.
Mhe. Jaji Mkuu
alizungumzia pia kuhusu umuhimu wa mradi huo, ambapo alisema unalenga
kuimarisha na kujenga miundombinu ya Mahakama ya Tanzania.
IMETOLEWA
NA KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni