MAHAKAMA YATEGEMEWA KUTENDA HAKI-JAJI WAMBALI
Na
Lydia Churi- Mahakama
Majaji wa Mahakama Kuu nchini
wametakiwa kufanya kazi yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo wakati wote kwa
kuwa watanzania wanaitegemea Mahakama kuwatendea haki kwa sawa na kwa wakati.
Akifungua Mkutano wa
Majaji Wafawidhi na Majaji waliosikiliza kesi mbalimbali za Uchaguzi wa Mwaka
2015 unaojadili mrejesho wa namna kesi za uchaguzi zilivyoshughulikiwa leo
jijini Arusha, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mheshimiwa Ferdinand
Wambali alisema watanzania wana imani na Mahakama hivyo ni muhimu kwa Majaji
hao kutenda haki wakati wote.
Alisema Majaji hao
wamekutana ili waweze kupata nafasi ya kujadili changamoto mbalimbali zilizojitokeza
wakati wa kusikiliza kesi zilizohusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kubadilishana
mawazo namna ya kuzimaliza kwa haraka kesi zihusuzo uchaguzi kwa siku za
mbeleni.
Alisema jumla ya kesi
53 za Ubunge zilizotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilifunguliwa katika Mahakama
Kuu kanda za Dar es salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Moshi, Mtwara na Mwanza.
Kanda nyingine ni Shinyanga, Songea, Sumbawanga, na Tanga.
Jaji Wambali alisema
kati ya kesi hizo, kesi 31 zilimalizika katika hatua za awali na kesi 22
ziliendelea. Mpaka sasa kesi 19 zimemalizika. Aliongeza kuwa kesi tatu bado
ziko mahakamani.
Jaji Wambali alisema ni
jambo la kujivunia kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwa kesi zote 196 zilizotokana
na uchaguzi wa madiwani zilimalizika mapema katika Mahakama mbalimbali za Hakimu Mkazi nchini.
Alisema katika kipindi
cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa uchaguzi Mkuu nchini, zaidi ya asilimia 94
ya kesi za uchaguzi zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu zimemalizika wakati asilimia
100 ya kesi zote za udiwani zimemalizika.
Jaji Kiongozi
amewapongeza Majaji na Mahakimu wote kwa kumaliza kesi kwa ufanisi na kwa
wakati licha ya changamoto mbalimbali wanazozipitia Watumishi hao wa Mahakama wakati
wanaposikiliza kesi zainazotokana na uchaguzi.
Aidha Jaji Kiongozi alishukuru
shirika la Umoja wa Mataifa-UNDP kwa kufadhili mafunzo mbalimbali ya Majaji na
Mahakaimu yaliyotolewa kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Mkutano wa
siku nne wa Majaji Wafawidhi pamoja na Majaji waliosikiliza kesi za uchaguzi ulioanza
leo jijini Arusha umefadhiliwa na shirika hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni