Waziri wa Katiba na Sheria
Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe ameishauri Mahakama ya Tanzania kufikiria uwezekano
wa kukifanyia mabadiliko chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuanza kutoa
shahada ya Sheria pasipo kukigeuza chuo hicho kuwa chuo kikuu.
Akihutubia wakati wa
sherehe za Mahafali ya 16 ya chuo hicho katika mji Mdogo wa Lushoto leo, Dkt.
Mwakyembe amesema kutokana na mabadiliko makubwa ya kisera ni vema chuo hicho
kikaanza kutoa Shahada ya Sheria pasipo kuwa chuo kikuu ili kibaki na jukumu
lake la msingi la kutoa mafunzo ya kisheria.
Alisema wizara yake
imejipanga kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kuhakikisha chuo hiki kinafanya
kazi yake ya kutoa mafunzo endelevu kwa watumishi na wadau wote wa Mahakama kwa
ufanisi mkubwa.
Alisema serikali ina nia ya
dhati ya kuhakikisha kuwa chuo hiki kinaendelezwa ili kiweze kutekeleza
majukumu yake na kuongeza kuwa ofisi yake iko wazi kwa chuo hiki ili kujadili
changamoto mbalimbali zinazokikabili na kuzitatua inapowezekana.
Aidha, katika Mahafali
hayo, Waziri Mwakyembe pia amewataka wahitimu wa chuo hicho kutojishirikisha na
vitendo vya rushwa pindi watakapopata kazi ili waweze kutenda haki kwa jamii.
Aliwapongeza wahitimu hao
kwa hatua waliyofikia na kuwataka pindi watakapoajiriwa kujiepusha na rushwa
ili mahakama iwe na mtazamo chanya mbele ya wananchi. “Ikimbieni rushwa siku
zote ili muweze kuwa waadilifu na kutenda haki katika kazi zenu pindi
mtakapoajiriwa”, alisema Mhe. Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe pia
aliwataka wahitimu hao kuwa wabunifu na kuendelea kujifunza mambo mapya kila
siku ili waende na wakati uliopo sasa na kutokidhalilisha chuo chao kwa
kutokuwa wabunifu.
Naye Mkuu wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto Mheshimiwa Jaji Kihwelo aliitaja baadhi ya mikakati
ya kukiendeleza chuo hiki katika kipindi cha mwaka ujao kuwa ni kukifanya chuo
hiki kiweze kutoa mafunzo endelevu kwa watumishi wa Mahakama na kuhimiza
matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Katika Mahafali hayo,
Waziri wa Katiba na Sheria pia alizindua Tovuti ya chuo, nembo ya chuo
iliyorekebishwa pamoja na matumizi ya mtandao wa Serikali (Government Mailing
System) kwa ajili ya chuo hicho.
Jumla ya wahitimu 343
walitunukiwa vyeti vya Stashahada na Astashahada ya Sheria kwenye mahafali hayo
ambapo wahitimu 208 walipata Stashahada ya Sheria na wengine 135 walipata
Astashahada ya Sheria.
MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA MAHAFALI YA 16 YA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO
Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo mara baada ya kuwasili katika
chuo hicho kwa ajili ya Mahafali. Waziri Mwakyembe alikuwa Mgeni Rasmi kwenye Mahafali
hayo yaliyofanyika jana Lushoto.
Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa kwenye Maandamano tayari kwa kuanza
Mahafali ya 16 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyika jana.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho Jaji Mstaafu wa Mahakama ya
Rufani Mhe. John Mrosso akifuatiwa na Mkuu wa chuo hicho Mhe. Jaji Dkt. Paul
Kihwelo.
Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa kwenye Maandamano tayari kwa
kuanza Mahafali ya 16 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyika
jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho Jaji Mstaafu wa Mahakama ya
Rufani Mhe. John Mrosso na katikati ni Katibu Mkuu wa wizara ya Katiba na
Sheria Prof. Sifuni Mchome.
Wahitimu wa
Stashahada ya Sheria katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakiwa katika
Mahafali hayo jana katika mji mdogo wa Lushoto.
Wahitimu wa
Astashahada ya Sheria katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakisubiri
kutunukiwa katika Mahafali hayo jana katika mji mdogo wa Lushoto
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Katarina Revokati (katikati) akiwa kwenye Mahafali hayo.
Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa ni Mgeni Rasmi kwenye
Mahafali hayo akiwatunuku Stashahada na Astashahada wahitimu wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (hawapo pichani) jana wakati wa Mahafali hayo.
Waheshimiwa Majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga na Moshi, Jaji Imani Abood (kushoto) na Jaji Aishieli Sumari (kulia) wakiwa kwenye Mahafali hayo jana katika mji mdogo wa Lushoto.
Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wa tano kutoka kulia waliokaa) ambaye
alikuwa ni Mgeni Rasmi kwenye Mahafali hayo akiwa katika picha ya pamoja na
wajumbe wa Baraza la chuo mara baada ya Mahafali hayo.
Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa ni Mgeni Rasmi kwenye
Mahafali hayo akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa Astashahada ya Sheria
mara baada ya Mahafali hayo.
Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa ni Mgeni Rasmi kwenye
Mahafali hayo akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa Stashahada ya Sheria
mara baada ya Mahafali hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni