Jumanne, 13 Desemba 2016

BAADHI YA MAJAJI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA WASHIRIKI KATIKA MAFUNZO YA KUBADILISHANA UZOEFU JUU YA UENDESHAJI WA MASHAURI YA JINAI


Na, Mary Gwera, Mahakama 
Katika muendelezo wa maboresho ya huduma ya utoaji haki nchini, Mahakama ya Tanzania imeweka kipaumbele katika kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa watumishi wake ikiwa ni pamoja na Majaji, Mahakamu na Watumishi wote kwa ujumla.

Hayo yalisemwa na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu- Kanda ya Dodoma, Mhe. Mwanaisha Kwariko alipokuwa akifungua Mafunzo ya Kubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa Mashauri ya Jinai yaliyoshirikisha jumla ya Majaji 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda mbalimbali nchini.

“Mahakama ya Tanzania imeona ni vyema na muhimu kutoa mafunzo haya kwa Majaji ili kutoa mwanya wa kuendelea kubadilishana uzoefu katika taratibu mbalimbali za ushughulikiaji wa mashauri ya jinai lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi,” alisema Jaji Kwariko.

Aliongeza kwa kusifu jitihada za Uongozi wa Mahakama kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wake wa Kada mbalimbali yote yakilenga katika kuboresho ya huduma ya utoaji haki nchini.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Mafunzo- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eliezer Feleshi, alisema kuwa kuwa suala la kubadilishana ujuzi ni la msingi na Mahakama imeliweka kama kipaumbele katika uendeshaji wake.

Awali; Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala- Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Mratibu wa Programu ya Mapambano dhidi ya Rushwa - Mahakama ‘STACA- Strengherning Tanzania Anti - Corrption Actions’; Programu ambayo inafadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la misaada DFID, Bi. Wanyenda Kutta alisema kuwa mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano (5), 2015/2016 -2019/2020. chini ya nguzo yake ya pili ya Upatikanaji na utoaji haki kwa wakati.

“Katika kubadilishana uzoefu huo Majaji watapata fursa ya kujadili changamoto mbalimbali katika kuyashughulikia mashauri ya jinai na kupata ufumbuzi kwa kutumia uzoefu miongoni mwao kwa kutumia sheria mbalimbali zilizopo, Majadliano haya miongoni mwao yana mchango mkubwa katika kuifanya Mahakama ya Tanzania kufikia kongeza ufanisi  katika utekelezaji wa majukumu yake na hatimaye  kuifikia Dira yake ya  Haki sawa kwa wote na kwa wakati” alisema Bi. Kutta.

Aliongeza kuwa matarajio ya mafunzo haya ni kuongeza ujuzi, uelewa na zaidi ufanisi wa Mahakama kwa ujumla katika jukumu lake la usikilizaji wa Mashauri mbalimbali kwa mujibu wa Mamlaka iliyo nayo.

Mafunzo haya ya siku tano kwa Majaji ni hatua endelevu Mahakama ya Tanzania katika kuwajengea uwezo Watumishi wake wa ngazi zote ili kuwawezesha  kutekeleza majukumu yao kwa  ufanisi  wa kiwango cha hali ya juu.

Aidha kwa mafunzo haya mahsusi chini ya ufadhili wa pamoja kati ya Mahakama na Serikali ya Uingereza chini ya program ya STACA yalitanguliwa na mafunzo kwa Mahakimu 173 yaliyofanyika kuanzia tarehe 14 Novemba – 2 Desemba, 2016.
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Mwanaisha Kwariko (aliyesimama mbele) akifungua rasmi mafunzo ya Kubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa mashauri ya jinai yanayofanyika katika Ukumbi wa Hazina mkoani Dodoma.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akiongea jambo katika mafunzo hayo, kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Iman Aboud, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Mafunzo, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiongea jambo katika ufunguzi wa Mafunzo ya kubadilishana uzoefu wa usikilizaji wa Mashauri ya jinai, ambapo pia alisema Mahakama imejipanga katika kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara.
Mkurugenzi Msaidizi- Utawala, Mahakama ya Tanzania, Bi. Wanyenda Kutta, akiwakaribisha Wahe. Majaji katika Mafunzo hayo, Bi Kutta pia ni Mratibu wa Programu wa Mapambano dhidi ya Rushwa ijulikanayo kama 'STACA'
Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Awadh Mohamed akitoa mada katika mafunzo hayo ya kubadilishana uzoefu juu ya mashauri ya jinai.
Baadhi ya Majaji wakiwa katika mafunzo hayo.
 Wahe.Majaji wakiwa katika majadiliano ya kikundi 'group discussion.'
 Baadhi ya Wahe. Majaji washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja, wa kwanza kulia aliyesimama ni Mkurugenzi Msaidizi- Utawala-Mahakama ambaye pia ni Mratibu wa Programu ya Mapambano dhidi ya Rushwa STACA






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni